Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-31 15:14:46    
China yaimarisha udhibiti wa tumbaku

cri

Ofisa wa wizara ya afya ya China tarehe 29 aliwaambia waandishi wa habari kuwa, tangu mkataba wa jumla wa udhibiti wa tumbaku uanze kutekelezwa nchini China mwezi Januari mwaka huu, serikali ya China imezidi kuimarisha udhibiti wa tumbaku kwa mujibu wa mkataba huo, na kuwahamasisha wananchi watilie maanani madhara ya afya yatokanayo na matumizi ya tumbaku.

Mkataba wa jumla wa udhibiti wa tumbaku ni mkataba wa kwanza wa kimataifa uliotungwa chini ya uongozi wa Shirika la afya duniani. Lengo lake ni kuzuia ueneaji wa tumbaku duniani, hususan katika nchi zinazoendelea. Nchi zaidi ya 100 ikiwemo China zimeshasaini mkataba huo.

China imerekebisha sheria husika, ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuutekeleza mkataba huo. Hapo awali katika sheria na taratibu mbalimbali za China, kulikuwa na vipengele kuhusu kupiga marufuku uvutaji sigara katika maeneo yanayotumika na watu wengi na kuweka vizuizi kwa matangazo ya biashara ya tumbaku. Lakini baadhi ya vipengele hivyo vimepitwa na wakati na vingine havilingani na mkataba huo.

Naibu mkuu wa idara ya afya ya akina mama na watoto na huduma ya afya ya mitaani iliyo chini ya wizara ya afya ya China Bw. Zhang Bin alisema kuwa "Hivi sasa tunaharakisha marekebisho ya sheria na taratibu zilizopo na kutunga sheria na taratibu mpya, ili mkataba wa jumla wa udhibiti wa tumbaku uweze kutekelezwa vizuri."

Ofisa huyo alifafanua kuwa, katika mswada wa marekebisho ya utaratibu wa usimamizi wa afya katika maeneo yanayotumika na watu wengi ambao umewasilishwa kwenye baraza la mawaziri la China, vipengele kuhusu kupiga marufuku uvutaji sigara katika maeneo yanayotumika na watu wengi imebadilishwa. Na katika sheria ya usimamizi wa matangazo ya biashara ambayo bado inarekebishwa, kuna vipengele vya kuzuia kampuni za tumbaku zisifanye ujanja katika matangazo ya biashara wa kughiribu wateja ili wanunue sigara.

Aidha China imeongeza nguvu katika kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya tumbaku.

Tarehe 31 May ni siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani. Harakati mbalimbali za kuwaelimisha wananchi kuhusu madhara ya tumbaku kwa afya zilifanyika na zitafanyika kabla na baada ya siku hiyo katika sehemu mbalimbali nchini China. Vile vile China ilishiriki kwenye shindano la kimataifa la kuacha uvutaji sigara la mwaka 2006. Hadi kufikia tarehe mosi May, Wachina zaidi ya elfu 90 walikuwa wamejiandikisha kushiriki kwenye shindano hilo.

Mbali na hayo, China imeanzisha vituo 48 vya majaribio vya mitaani vinavyowashawishi wakazi waache uvutaji sigara. Pia inahamasisha hospitali na shule ziwe maeneo yasiyo na uvutaji sigara. Na maeneo mbalimbali yanayotumika na watu wengi zikiwemo idara za elimu na afya, yanapewa kipaumbele kuchukuliwa hatua za kudhibiti uvutaji sigara.

Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 ya Beijing pia itakuwa michezo isiyo na uvutaji sigara kama michezo iliyopita ya Olimpiki.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 29 May, idara husika ya China ilitoa taarifa ya uvutaji sigara na hali ya afya ya China mwaka 2006. Taarifa hiyo ambayo inahusu udhibiti wa tumbaku na kinga na matibabu ya kansa ya mapafu, inadhihirisha kuwa, uvutaji wa sigara unasababisha idadi ya watu wanaopata kansa ya mapafu na watu wanaokufa kutokana na ugonjwa huo kuongezeka kwa haraka nchini China.

Katika siku zijazo wizara ya afya ya China itatoa taarifa kuhusu uvutaji sigara na afya kwa mwaka, na taarifa ya kila mwaka itahusisha masuala tofauti. Hatua hiyo inalenga kuwafahamisha wananchi wazingatie madhara ya afya yatokanayo na tumbaku.

China ni nchi inayozalisha na kutumia tumbaku kwa wingi kabisa duniani, ambapo idadi ya uzalishaji wa bidhaa za tumbaku na idadi ya watu wanaovuta sigara kila moja inachukua theluthi moja ya ile ya dunia. Kwa hiyo udhibiti wa matumizi ya tumbaku una umuhimu na ugumu nchini China. Ofisa wa wizara ya afya ya China Bw. Zhang Bin alisema "Hivi sasa tumeanza tu utekelezaji wa mkataba wa jumla wa udhibiti wa tumbaku, bado tunakabiliwa na matatizo mengi. Udhibiti wa madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku ni kazi ngumu na ya muda mrefu inayohusu watu wengi, pia ni suala la kijamii na kiuchumi, ambalo linahusu kupandisha bei ya tumbaku, kutoza kodi kubwa tumbaku, kupiga marufuku matangazo ya biashara ya uvutaji wa sigara."

Ofisa huyo aliongeza kuwa, kazi ya kudhibiti matumizi ya tumbaku inataka ushirikiano wa karibu wa idara mbalimbali za serikali, pamoja na kushirikisha wananchi wa hali mbalimbali. Hivi sasa idara za afya, usimamizi wa shughuli za biashara na viwanda, na kodi zimeanzisha mfumo wa uratibu wa kudhibiti matumizi ya tumbaku. China pia itatunga mpango wa utekelezaji wa kudhibiti matumizi ya tumbaku nchini kote, ikilenga kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku kwa afya ya wananchi kwa kutumia hatua mbalimbali.

Idhaa ya kiswahili 2006-05-31