Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-05-31 17:36:52    
Udhibiti wa uvutaji sigara ni jukumu kubwa na gumu

cri

Tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu ni siku ya kutovuta sigara duniani ya mwaka wa 19. Kauli mbiu ya siku hiyo mwaka huu ni "tumbaku inaua". Shirika la Afya Duniani linatarajia kuongeza ufahamu wa watu hususan vijana na watoto kuhusu madhara ya tumbaku juu ya afya zao kutokana na harakati za uenezi kuhusu kauli mbiu hiyo.

Takwimu zinaonesha kuwa, hivi sasa sehemu moja ya sita ya watu duniani wanavuta tumbaku na sigara, na kiasi cha watu milioni tano wanakufa kila mwaka kutokana na uvutaji sigara au magonjwa yanayohusiana na uvutaji sigara. Endapo uvutaji sigara hautadhibitiwa, idadi ya watu watakaokufa katika karne hii kutokana na uvutaji sigara itaongezeka kwa maradufu kuliko ile ya karne iliyopita. Kiasi cha kuugua saratani ya mapafu kwa wavutaji sigara ni mara 10 hadi 20 ya watu wasiovuta sigara, wakati uwezekano wa kuugua saratani ya kioo ni mkubwa mara 2 hadi 3 kuliko watu wasiovuta sigara, na kiasi cha wavutaji wa sigara wanaopata matatizo katika mishipa inayopitisha kuwa ni kikubwa kwa mara 2 hadi 8 kuliko watu wasiovuta sigara. Licha ya hayo, madhara ya kupumua hewa yenye moshi wa sigara kwa watu wasiovuta sigara ni makubwa zaidi, watu wanaopumua hewa yenye moshi wa sigara kwa saa 1 kila siku ni rahisi kupatwa matatizo ya mishipa ya damu. Na idadi ya wanawake wanaoishi pamoja na wavutaji sigara wanaougua saratani ya mapafu ni kubwa mara 6 kuliko watu wasiovuta sigara.

Pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia, watu wanatambua zaidi madhara ya sigara kwa afya na uhai wa binadamu, lakini tatizo kubwa ni kwamba idadi ya watu wanaovuta sigara haipungui bali inaendelea kuongezeka. Vyanzo vya kutokea hali ya namna hiyo ni vingi, lakini chanzo muhimu ni kufanya hila kwa kampuni za sigara hususan kampuni za sigara za nchi zilizoendelea kutokana na kuvutiwa na faida nono. Katika karne iliyopita, kampuni hizo zilizalisha aina mpya "nyepesi", "laini" na zenye kiasi kidogo cha moshi, ili kuwarubuni wavutaji sigara kuwa sigara za aina hizo ni salama. Shirika la afya duniani kwenye tovuti yake limesema, aina zote za sigara zinaleta madhara kwa afya za watu kwa viwango mbalimbali, na limezitaka serikali za nchi mbalimbali zifanye usimamizi mkali kuhusu aina mbalimbali za sigara.

Hivi sasa nchi nyingi zimechukua hatua kali za kuzuia uvutaji sigara. Ireland, Hispania na Norway zimepiga marufuku kuvuta sigara kwenye majengo ya umma. India nayo imebuni sheria kuhusu kupiga marufuku matangazo ya biashara ya sigara. Australia, Brazil, Canada, Singapore na Thailand zinaagiza kuwa maneno ya " uvutaji sigara unadhuru afya" lazima yachapishwe kwenye paketi za sigara. Mchakato wa kununua sigara kwenye mashine nchini Japan ni kuwa mnunuzi anatakiwa kupitisha kwanza leseni ya uendeshaji gari, kisha akaweza kutoa fedha na kupata sigara, kufanya hivyo watoto wanaweza kukataliwa. Nchini Malaysia, watu wazima kutuma watoto kuwanunulia sigara ni kitendo cha makosa ya kisheria, ambayo anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 2. Katika miaka ya karibuni, idara husika za serikali ya China pia zimechukua hatua za kudhibiti uvutaji sigara, zikiwa ni pamoja na kuanzisha harakati za majengo ya umma, ofisi, viwanda na kampuni zisizo na wavutaji sigara, pamoja na miji isiyo na matangazo ya biashara ya sigara. Zaidi ya hayo, idara hizo zinatoa pigo kubwa kwa biashara haramu ya sigara na kuwauzia sigara watoto. Aidha, China inajitahidi kuifanya michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 iwe michezo isiyo na watu wanaovuta sigara.

Mkutano wa kwanza wa nchi zilizosaini "Mkataba wa Kanuni za Udhibiti wa Uvutaji Sigara" ulifanyika kati ya tarehe 6 na 17 mwezi Februari mwaka huu huko Geneva. Mkutano huo ulizitaka nchi mbalimbali zichapishe onyo kuhusu madhara ya sigara kwenye paketi za sigara ndani ya miaka 3, kutokomeza matangazo ya biashara ya sigara na kutoruhusu utoaji misaada wa kampuni za sigara ndani ya miaka 5.

Watu wanaona kuwa udhibiti wa uvutaji sigara ni jukumu kubwa na gumu, na pia ni suala la kijamii na kiuchumi linalohusiana na sera za serikali. Nchi zote ziwe tajiri au maskini, zinatakiwa kuimarisha udhibiti wa uvutaji sigara kwa kuendana na hali halisi ya nchi zenyewe.

Idhaa ya Kiswahili 2006-05-31