Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-01 16:11:27    
Harakati ya kuokoa lugha ya Kiman yatekelezwa nchini China

cri

Kabila la Waman ni kabila kubwa la tatu nchini China, ambalo lina watu milioni 10. Lakini hivi sasa watu wanaofahamu kuongea lugha ya Kiman hawazidi 100. Kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu, uzungumzaji sanifu wa Kiman utatoweka kabisa ndani ya miaka mitano au kumi ijayo kama hatua za haraka hazijachukuliwa. Katika mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki ya China ambapo wanaishi watu wengi wa kabila la Waman, harakati inayolenga kuokoa lugha ya Kiman imeanza kutekelezwa.

Kijiji cha Sanjiazi mkoani Heilongjiang kina wakazi wengi wa kabila la Waman. Kijiji hicho pia ni mahali pekee ambapo mila na desturi nyingi za kabila hilo zimehifadhiwa vuziri. Kati ya wanakijiji zaidi ya elfu moja, Waman huchukua asilimia 60. Lakini watu wanaoweza kuongea Kiman sanifu hawazidi 20, na wengi wao ni wazee wenye umri wa miaka 70 na 80.

Mliyosikia ni mazungumzo ya Kiman kati ya mwanakijiji Meng Shujing na dada yake. Mjukuu wa mzee Meng Shujing, Bw. Shi Junguang alitafsiri kwa Kichina anasema, "Bibi yangu aliuliza mlo wa leo usiku, na shangazi yangu akamjibu tutakula wali na mboga."

Bw. Shi Junguang alizaliwa na kukua kwenye kijiji hicho. Anatoka kabila la Waman, lakini alijifunza lugha ya Kichina. Mwaka 2000 kijana huyo alihitimu kutoka sekondari na kurudi kwenye maskani yake kushughulisha na kilimo, ambapo wazo moja lilimjia akilini, yaani kujifunza lugha ya Kiman kutoka kwa bibi yake, na kuhifadhi lugha hiyo ambayo iko hatarini kutoweka kabisa. Bw. Shi Junguang alisema "Natambua kuwa lugha hii itapotea, lakini kama sijifunzi na bali kuiacha ipotee, basi nitahuzunika sana. Kwa sababu mimi natoka kabila la Waman, baba yangu, mama yangu, babu na bibi zangu, wote ni Waman, nina damu kamili ya Waman. Kwa hiyo inanibidi nibebe wajibu."

Baada ya hapo, mzee Meng Shujing alimfundisha mjukuu wake lugha ya Kiman, na kijana huyo aliweka kumbukumbu ya misamiati, sentensi na maneno yanayotumika sana kwenye lugha hiyo kwa kutumia chombo cha kurekodi.

Hivi sasa, Bw. Shi Junguang amehifadhi kaseti nyingi, na amezishughulikia na kuweka kumbukumbu za maandishi. Ingawa bado hawezi kuongea Kiman sanifu na kuwa mkalimani, kijana huyo sasa anaongoza miongoni mwa vijana wa kijiji hicho katika lugha ya Kiman.

Naibu mkuu wa wilaya ya Fuyu mkoani Heilongjiang Bw. Zhao Jinchun alieleza maoni yake, akisema "Tunaweza kusema kijiji hicho ni mahali pekee duniani ambapo lugha ya Kiman inahifadhiwa. Lakini iwapo wazee wa kijiji hicho wakifariki dunia, lugha hiyo itapotea. Itakuwa vigumu sana kufanya juhudi za kuiokoa lugha hiyo ama kuifufua."

Waman walianzisha enzi ya Qing, ambayo ni enzi ya kifalme ya mwisho katika historia ya China, kwa hiyo lugha ya Kiman ilikuwa imeenea sana katika kipindi cha enzi ya Qing. Baada ya kuangushwa kwake, watu wanaofahamu lugha hiyo na wanaojifunza lugha hiyo walipugua hatua kwa hatua. Lakini nyaraka mbalimbali za enzi ya Qing, kwa mfano mikataba, taratibu na nyaraka za siri zinahifadhiwa kwa lugha ya Kiman. Hivi sasa kutokana na kukosa watu wanaofahamu lugha hiyo, nyaraka nyingi za kihistoria haziwezi kutafsiriwa.

Kuhusu hali hiyo, Bibi Zhao Aping ambaye ni mkuu wa Taasisi ya lugha ya Kiman ya Chuo kikuu cha Heilongjiang alisema, "Kuna matukio kadhaa ya kihistoria ambayo hayapo katika nyaraka za Kichina hakuna, lakini yapo katika nyaraka za Kiman. Baadhi ya mikataba na nchi za nje ilipotungwa, iliandikwa kwa Kiman badala ya lugha nyingine."

Bibi Zhao alieleza kuwa, kuokoa lugha ya Kiman kuna umuhimu na thamani kubwa kwa utafiti wa historia ya China.

Hivi sasa kijiji cha Sanjiazi kimekuwa makao makuu ya kufundisha na kutafiti lugha ya Kiman. Katika miaka ya hivi karibuni, wataalamu wa lugha kutoka China na nchi za nje walitembelea kijiji hicho mara nyingi, ambapo waliweka rekodi kwa kamera na chombo cha kunasa sauti, na waliwauliza wazee wa kijiji hicho maneno na sentensi za lugha ya Kiman.

Mwaka 2005 serikali ilianzisha shule inayotumia lugha ya Kiman katika kijiji hicho, ambayo ilikuwa ni ya kwanza ya namna hiyo hapa nchini China.

Kwa kuwa shule hiyo haina walimu wa kutosha, naibu mkuu wa wilaya Bw. Zhao Jinchun anayefahamu lugha ya Kiman alifanya kazi za kutunga vitabu vya masomo, hata yeye mwenyewe amebeba kazi fulani ya ualimu. Bila kujali hali ngumu ya kusoma, watoto wa kabila la Waman wa huko wana hamu kubwa ya kujifunza. Mtoto mmoja alisema "Nina hamu ya kujifunza Kiman, kwani mimi natoka kabila la Waman. Kama nisipojifunza, lugha ya Kiman itapotea."

Mwaka 2000 Chuo kikuu cha Heilongjiang kilianzisha masomo ya shahada ya pili ya lugha ya Kiman. Mpaka hivi sasa, wanafunzi wa awamu nne wamehitimu masomo hayo. Na mwaka 2005, chuo kikuu hicho kilianzisha masomo ya shahada ya kwanza ya lugha ya Kiman. Hivi sasa harakati ya kuokoa lugha ya Kiman nchini China inaendelea kutekelezwa.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-01