Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-01 16:18:57    
Mgeni anayefanya kazi ya utangazaji wa vipindi vya Kichina

cri

Kijana huyo alikuja China kutokana na fursa moja ya bahati miaka minane iliyopita, na uamuzi huo ulibadilisha kabisa maisha yake.

Miaka minane iliyopita, Bw. Doran alihitimu kutoka chuo kikuu, yeye na marafiki zake walikwenda Australia kwa likizo. Katika hoteli moja mjini Sydney, walikutana na Mchina ambaye aliwashauri Bw. Doran na marafiki zake wawili Waingereza, wakafanya kazi ya kufundisha katika shule ya sekondari mjini Liaoyang, mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China.

Bw. Doran na marafiki zake walikubali pendekezo hilo. Walifika Liaoyang mwezi Machi, wakati huo kulikuwa na theluji kubwa. Hiyo ndiyo picha waliyopata mara ya kwanza kuhusu China.

"Hatukufahamu hali ya hewa ya China, hasa hatukujua hali ya hewa ya eneo la kaskazini mashariki ya China wakati wa mwezi wa Machi. Tulidhani labda inafanana na ya Australia. Kumbe tulikaribishwa na theluji kubwa na hali joto ilikuwa nyuzi 20 chini ya sifuri, tukaduwaa."

Siku alizokuwa akifanya kazi ya ualimu katika mji wa Liaoyang zinampa kijana huyo kumbukumbu nzuri. Katika shule hiyo, ama walimu wenzake, au wanafunzi wake, wote walimpenda sana mwalimu huyo mwenye sura ya kimagharibi. Wanafunzi wake walimpa jina la Kichina lisemalo Dong Mohan, maana yake ni kumtakia awe na mwenye moyo mkubwa na hamu kubwa kwa elimu.

Katika kipindi hicho, Bw. Doran alivutiwa na msichana mmoja, anayeitwa Li Ying, ambaye alikuwa anafundisha lugha ya Kiingereza katika shule hiyo.

Hapo mwanzo Bw. Doran alikuwa amepanga kukaa nchini China kwa mwezi mmoja tu, lakini alikaa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja. Baada ya kukamilisha mkataba wake wa ualimu, alirudi nyumbani nchini Ireland. Lakini moyo wake ulikuwa umetekwa kabisa na China na msichana yule Mchina. Akaamua kuja tena China. Na safari hii alijiandikisha katika Chuo kikuu cha lugha cha Beijing na kusoma Kichina kwa miaka mitatu na nusu.

Kijana huyo ana kipaji katika kujifunza Kichina, katika kipindi kifupi tu aliweza kuongea vizuri lugha hiyo inayochukuliwa kuwa ni moja ya lugha ngumu duniani.

Hivi sasa Bw. Doran anafanya kazi ya utangazaji wa Kichina katika Idhaa ya Kichina ya Radio China Kimataifa na katika Radio ya Beijing. Kuhusu kazi hiyo, kijana huyo alisema kazi ya utangazaji inamsaidia sana.  "Kazi ya utangazaji katika vipindi hivyo viwili inanivutia sana kwani inanipa fursa nyingi zaidi za kuwafahamu Wachina wa kawaida, hususan maisha ya wale wanaoishi katika miji mikubwa."

Katika kipindi cha "maoni ya wageni" cha Radio China Kimataifa, Bw. Doran anashirikiana na watangazaji wenzake wawili, ambao ni Bw. Julian anayetoka Ufaransa na Bibi Li Xin kutoka mji wa Tianjin, China. Katika kipindi hicho, watangazaji hao watatu wakitumia Kichina, wanaeleza maoni yao kuhusu masuala mbalimbali zinazozungumzwa sana kwenye jamii ya China, kujadiliana kwa mitizamo tofauti ya Kimashariki na Kimagharibi.

Mtangazaji mwenzake Bibi Li Xin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kwa vile walivyokulia katika mazingira na utamaduni tofauti kabisa na Doran na Julian, wana maoni tofauti juu ya masuala mbalimbali. Ndiyo maana maoni yao yanagongana mara kwa mara kwenye kipindi hicho, hata siku nyingine wanabishana vikali. Hata hivyo tofauti hizo hazileti matatizo kwa ushirikiano mzuri kwenye kazi kati yao. Bibi Li Xin alieleza kuwa, Bw. Doran anapendeza kama mvulana alivyo mkubwa.

"Wakati wa kuandaa kipindi chetu, busara na ucheshi wake unajitokeza mara kwa mara. Siku nyingine anaonekana kama ni mtoto, anaongea kama anavyofikiria, anakuambia mawazo yake bila kuficha, na siku nyingine mtindo wake huo ni wa kupendeza sana."

Bibi Li Ying ambaye Bw. Doran alivutiwa naye wakati alipofanya kazi ya ualimu mkoani Liaoning, sasa ni mke wake, familia hiyo pia ina mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu. Ili kumtunza vizuri mtoto wao, Bibi Li Ying ameacha kazi yake kwa muda. Sasa akiulizwa kazi ya mke wake, Bw. Doran anamjibu kwa ucheshi kuwa, "anajiburudisha" nyumbani.

Wakati wa mapumziko, Bw. Doran anapenda kubaki nyumbani kusoma vitabu, na kucheza na mwanae.

Katika siku za kazi, anaamka saa 12 asubuhi na kwenda kazini katika radio kwa basi na subway. Mbali na hayo, kijana huyo anafanya mahojiano mara kwa mara kwenye televisheni. Kwa hiyo ana pilikapilika siku zote.

Wachina wanapenda kuwaita wageni Lao Wai, maana yake ya Kichina ni mgeni. Lakini Bw. Doran hafurahii kusalimiwa namna hii, na pia hafurahii kusalimiwa na Wachina kwa Kiingereza. Anapenda kula chakula cha Kichina kinachopikwa na mke wake, na ni nadra kwake kula kwenye mikahawa ya chakula cha kimagharibi. Anaona anapoishi hapa China, inafaa kufuata mila na desturi za Wachina. Kijana huyo atokaye Ireland anasema anapenda kuishi hapa Beijing kama wakazi wengine wa Beijing.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-01