Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-01 20:04:06    
Kwanini Marekani imekubali kuwa na mazungumzo na Iran

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleezza Rice tarehe 31 mwezi Mei alitangaza kuwa, kama Iran itaacha kusafisha uranium na urudishaji nishati ya nyukilia, Marekani itafikiria kushirikiana nayo na kuwa na mazungumzo kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya, na pia kutatua suala la nyukilia la Iran. Mchambuzi mmoja amesema, kitendo cha Marekani kukubali kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Iran kuhusu suala la nyukilia kwa masharti fulani, kunaonesha kutokea kwa mabadiliko makubwa katika msimamo wa Marekani kuhusu utatuzi wa mvutano kati yake na Iran.

Bi Rice siku hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa siku hiyo na wizara ya mambo ya nje, alisema, endapo Iran itaacha kusafisha uranium na urudishaji wa nishati ya nyukilia kwa njia ya kuweza kukaguliwa, Marekani inakubali kushiriki kwenye mazungumzo ya suala la nyukilia kati ya nchi tatu za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Iran. Wakati huo huo, bibi Rice alisisitiza kuwa, Marekani inatambua haki ya Iran ya kutumia nishati ya nyukilia kwa njia isiyo ya kijeshi, lakini ni lazima Iran iache mpango wake wa kutengeneza silaha za nyukilia. Alisema, endapo Iran inakubali kuacha mpango wake wa nyukilia, Marekani inakubali kuboresha uhusiano na Iran, na mazungumzo kuhusu suala la nyukilia yatakuwa mwanzo wa kuboresha uhusiano kati ya nchi mbili.

Katika kipindi kilichopita, ingawa serikali ya Marekani ilisisitiza mara nyingi kuwa utatuzi wa suala la nyukilia la Iran kwa njia ya kidiplomasia ni chaguo la kwanza la Marekani, lakini Marekani imekuwa ikishikilia kutofanya mazungumzo ya ana kwa ana na Iran kuhusu suala la nyukilia, ikisema kuna njia nyingi za upashanaji habari kati ya Marekani na Iran, na hakuna tatizo la mawasiliano kati yao. Marekani inaona kuwa kitu muhimu kabisa ni Iran kuacha mpango wake wa nyukilia. Kwa upande mwingine Marekani ilikuwa inatafuta uwezekano wa jumuiya ya kimataifa kuiwekea Iran vikwazo, na bila kuondoa uwezekano wa kuishambulia kijeshi.

Lakini ni kwanini sasa Marekani inakubali kwa masharti kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na Iran kuhusu suala la nyukilia? Vyombo vya habari vinachambua kuwa shinikizo kubwa kutoka nchini Marekani na kutoka nje, ni sababu muhimu iliyoifanya Marekani irekebishe sera yake kwa Iran.

Kwanza, nchini Marekani uungaji mkono wa umma kwa rais Bush umepungua hadi 31% kutokana na vita vya Iraq na kufikia kiwango cha chini kabisa tangu ashike wadhifa wa urais, bei kubwa ya mafuta na kashfa za kisiasa. Kutokana na kukabiliwa na shinikizo kubwa, Bush hanabudi kuwa na mafanikio katika suala la nyukilia la Iran ili chama chake cha Republican kipate ushindi kwenye uchaguzi wa kipindi cha kati wa bunge la Marekani utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Pili, jumuiya ya kimataifa inataka sana Marekani ishiriki kwenye mazungumzo na Iran. Russia na China siku zote zinataka suala la nyukilia la Iran litatuliwe kwa njia ya kidiplomasia. Nchi tatu za Umoja wa Ulaya hivi karibuni ziliona kuwa endapo Marekani haitashiriki kwenye mazungumzo ya suala la nyukilia la Iran, basi haziwezi kupata mafanikio katika kutatua suala hilo kwa njia ya kidiplomasia. Hivyo baada ya Marekani kueleza uwezekano wa kushiriki kwenye mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na Iran, mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya kidiplomasia na sera za usalama Bw. Javier Solana alitoa taarifa ya pongezi mara moja.

Tatu, kwa kufikiria maslahi yake yenyewe, Marekani haitaki kuibana Iran kupita kiasi au kuishambulia kijeshi. Kwanza endapo Iran itatumia silaha ya "Mafuta", bei ya mafuta ya ghafi duniani itapanda sana, kiasi cha kukwamisha maendeleo ya uchumi wa dunia, ambapo uchumi wa Marekani pia utaathiriwa; Pili, Iran ikiwashawishi waislamu wa madhehebu ya Shia kunyanyuka kupinga ukaliaji wa jeshi la Marekani, jeshi la Marekani nchini Iraq litaingia matatani sana.

Baada ya kufanya makadirio kuhusu faida na hasara, hatimaye Marekani imefanya marekebisho kuhusu sera zake za suala la nyukilia la Iran.

Idhaa ya Kiswahili 2006-06-01