Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-02 16:43:12    
Bara la Afrika litavutia uwekezaji mwingi kutoka China

cri

Kutokana na nchi za Afrika kufungua mlango zaidi siku hadi siku kwa nchi za nje, na kuongezeka kwa mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika, makampuni mengi zaidi ya China yatawekeza vitega uchumi barani Afrika.

Kwenye kongamano la kwanza la uwekezaji la Afrika lililofanyika tarehe 22 mwezi Mei hapa Beijing, mtaalamu mmoja wa mambo ya Afrika alisema, zamani sehemu kubwa ya mawasiliano ya kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika ilikuwa uwekezaji wa kiserikali na biashara zilizofanywa na watu binafsi, hivyo kiwango cha mawasiliano ya kiuchumi kati ya China na Afrika kilikuwa kidogo, lakini katika kipindi cha miaka mitano au minane ijayo, makampuni mengi ya China yatakwenda kuwekeza barani Afrika.

Mkurugenzi wa idara ya utafiti wa uchumi duniani katika kituo cha ushirikiano wa kimataifa cha kamati ya maendeleo na mageuzi ya China Bwana Chi Changsheng alisema, katika miaka ya karibuni, hali ya kisiasa ya nchi za Afrika imekuwa nzuri siku hadi siku, uchumi wake umepata maendeleo mazuri, na mazingira ya uwekezaji yameboreshwa, hivi sasa nchi za Afrika zimekuwa sehemu inayovutia uwekezaji mwingi duniani.

Bw. Chi Changsheng alisema, katika hali hiyo, makampuni ya China yatakuwa na nafasi nyingi za kujiendeleza katika nchi za Afrika.

Serikali ya China inachukua hatua mbalimbali kuwahimiza wanakampuni wa China kuwekeza barani Afrika, ambazo ni pamoja na kuwarudishia ushuru wa bidhaa zinazosafirishwa nje na kulegeza masharti ya kupeleka nje fedha za kigeni. Hivi sasa wanakampuni wa China wameanzisha makampuni zaidi ya 6000 ya ubia katika nchi za Afrika.

Mkuu wa kundi la mabalozi wa nchi za Afrika nchini China, ambaye pia ni balozi wa Cameroon nchini China Bwana Ele Edian kwenye kongamano hilo alitoa mwaliko kwa makampuni ya China kuwekeza barani Afrika. Alisema makampuni ya China yanakaribishwa sana kuwekeza vitega uchumi katika sekta za miundo mbinu barani Afrika, utafutaji na uchimbaji wa madini, uchukuzi na nishati.

Kwenye kongamano hilo, nchi za Afrika zilileta miradi zaidi ya kumi kuvutia uwekezaji wa China, ambayo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba wa Cameroon, kuanzisha kiwanda cha kutengeneza vifaa vya nyumbani cha Ethiopia, kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mazao ya nyama cha Tanzania, kiwanda cha kusaga unga wa ngano cha Eritrea na miradi ya uchimbaji wa madini, usindikaji wa mazao ya kilimo na kuendeleza rasilimali ya misitu ya nchi nyingine barani Afrika.

Balozi wa Kongo Brazzaville Bwana Pierre Pasi alitoa pendekezo kwa serikali ya China kutunga sera za kuyahimiza makampuni yenye uwezo ya China kuwekeza barani Afrika, na nchi za Afrika zitatoa miradi mizuri kwa makampuni ya China, ili kusukuma mbele uhusiano wa kibiashara kati ya China na nchi za Afrika.

Wataalamu waliohudhuria kongamano hilo waliona kuwa, makampuni ya China hasa makampuni binafsi ya China yanaweza kujiendeleza huko Afrika, lakini ni lazima yawe na tahadhari wakati wa kutoa uamuzi. Kwanza wanatakiwa kufahamu hali halisi ya mazingira ya uwekezaji ya huko, kuchagua vizuri mradi itakayowekezwa ili kupunguza hatari ya kupata hasara.

Katika miaka ya karibuni, biashara kati ya China na nchi za Afrika imekuwa ikiongezeka haraka, China imekuwa mshirika wa tatu wa biashara wa nchi za Afrika ikizifuata Marekani na Ufaransa. Kuanzia mwaka 2000 hadi sasa, thamani ya biashara kati ya China na nchi za Afrika imeongezeka mara tatu, mwaka jana ongezeko hilo lilifikia asilimia 37, na jumla ya thamani ya biashara kati ya China na nchi za Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 40 hivi.

Kongamano hilo lililofanyika kwa siku moja liliendeshwa kwa pamoja na shirikisho la wakala la kimataifa na kampuni inayotoa ushauri wa kibiashara ya Afekose ya Beijing. Kongamano hilo ni moja ya shughuli muhimu za wiki ya Afrika zilizofanyika hapa Beijing, wanadiplomasia kutoka ofisi ya Umoja wa Afrika nchini China, mabalozi wa nchi za Afrika nchini China, maofisa wa kiserikali na wanakampuni zaidi ya 100 wa China walihudhuria kongamano hilo.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-02