Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tano wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama na Ujerumani tarehe mosi Juni walikutana huko Vienna na kufikia makubaliano kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran. Kwa kuwa hivi karibuni Marekani ilisema iko tayari kufanya mazungumzo na Iran kwa masharti, kwa hiyo mkutano huo wa nchi sita na matokeo yake yanazingatiwa sana.

Baada ya mkutano, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza kwenye mkutano na waandishi wa habari alisoma taarifa fupi akisema, nchi sita zimetoa "mapendekezo yenye maana muhimu", na mada ya mapendekezo hayo ni kuwa, kama Iran ikisimamisha shughuli za kusafisha uranium, Baraza la Usalama litaacha kujadili suala la nyuklia la Iran, la sivyo baraza hilo litachukua hatua nyingi mfululizo. Aliihimiza Iran "ichague njia sahihi". Lakini hakudokeza mapendekezo halisi, inasemekana kuwa hii ni kwa sababu mapendekezo hayo bado hayajawasilishwa kwa Iran.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa habari zilizodokezwa na pande mbalimbali, mapendekezo hayo ni pamoja na kwamba, endapo tu Iran itasimamisha shughuli za afisha uranium, pande husika zitaanzisha ushirikiano wa mambo mengi ya kiuchumi na kiteknolojia na Iran, kuipatia Iran uhakikisho wa usalama, na kuisaidia Iran kujenga kinu cha maji mepesi na nishati ya nyuklia. Lakini kama Iran iking'ang'ania shughuli za kusafisha uranium, Baraza la Usalama litaiadhibu Iran kwa mujibu wa kifungu cha 41 ibara ya saba ya "Katiba ya Umoja wa Mataifa", ikiwa ni pamoja na kusimamisha kutoa viza kwa maofisa wa Iran, kuwapigia marufuku kushiriki kwenye mikutano ya kimataifa, kuzuia mali za Iran katika nchi za nje na kusimamisha usafirishaji wa silaha na mafuta yaliyosafishwa. Lakini mapendekezo hayo hayakutaja kifungu cha 42 kwenye ibara hiyo inayohusu "kuruhusu kutumia nguvu za kijeshi kwa nchi inayoadhibiwa kama kuna ulazima", yaani mapendekezo hayo yameondoa uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi kwa Iran.
Kutokana na shinikizo kutoka pande mbalimbali na kwa ajili ya kupata uungaji mkono kutoka pande husika, hasa Russia na China, waziri wa mambo ya nje wa Marekani tarehe 31 Mei alisema, ikiwa Iran itaacha shughuli za kusafisha uranium Marekani itakubali kufanya mazungumzo na Iran pamoja na wajumbe wa nchi tatu zinazowakilisha Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Katika siku hiyo, rais Bush wa Marekani pia alisema, kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia ni muhimu sana. Ishara ya Marekani kwa Iran zinaonesha wazi kuwa Iran haitakiwi kumiliki silaha za nyuklia, na Iran lazima ithibitishwe kwamba kweli imesimamisha shughuli za kusafisha uranium, na kwa msingi huo tu ndio Marekani itafanya mazungumzo na Iran.
Msimamo huo wa Marekani umekaribishwa na Umoja wa Ulaya, Russia na China. Vyombo vya habari vinaona hii inamaanisha kwamba kwa mara ya kwanza Marekani imeitambua serikali ya Iran baada ya kuvunja uhusiano wa kibalozi na Iran kwa miaka 26, na kuonesha kwamba Marekani haina budi kutatua suala la nyuklia la Iran kwa sera zisizo za upande mmoja, na hii pia inadhihirisha mabadiliko makubwa ya sera za Marekani kwa Iran. Kama Marekani na Iran, nchi hizo mbili muhimu zinazohusika moja kwa moja na suala la nyuklia la Iran zitafanya mazungumzo uso kwa uso, basi uwezekano wa kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia hakika utakuwa mkubwa zaidi.
Kabla ya nchi hizo sita kukutana, waziri wa mambo ya nje wa Iran alipozungumzia msimamo wa Marekani wa kufanya mazungumzo kwa masharti, alisema Iran iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani. Alisema, Iran inakubali kufanya mazungumzo na pande zote husika kwa uwazi, haki na bila ubaguzi wowote. Aliongeza kuwa hakuna ushahidi wowote unaonesha kwamba Iran inataka kutengeneza silaha za nyuklia. Lakini Iran haitasimamisha shughuli za kusafisha uranium kama Marekani inavyoitaka.
Wachambuzi wanaona kwamba mapendekezo hayo yaliyotolewa na nchi tano wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalma na Ujerumani yakilinganishwa na mapendekezo yaliyotolewa na Umoja wa Ulaya au Russia yanavutia zaidi, na Iran hakika itayazingatia kwa makini.
Kutokana na hali hiyo, ingawa tofauti bado zipo, lakini pande husika, hasa Iran na Marekani, zimeonesha matumaini ya kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo. Watu wanatumai kwamba mapendekezo yaliyopatikana katika mkutano wa nchi sita huko Vienna yatasukuma pande zote kupiga hatua imara katika utatuzi wa suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia.
Idhaa ya kiswahili 2006-06-02
|