Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-05 14:11:54    
Mji mdogo wa kale uitwao Pingyao na mahoteli mengi yaliyopo mjini humo

cri

Mji mdogo wa kale uitwao Pingyao mkoani Shanxi, kaskazini ya China ni mji wenye vivutio vingi vya utalii. Mji huo ni mji wa wilaya ya kale unaohifadhiwa kikamilifu zaidi nchini China, ambao umeorodheshwa kuwa mali ya urithi duniani. Hivi sasa mji huo uliokuwa kimya umepata umaarufu nchini China na nje, ambao umekuwa mahali pa kutengenezea filamu za televisheni, pia unawavutia watalii wengi wanaoendesha magari kwenda kwenye mji huo kutalii.

Mji wa Ping Yao uko katika sehemu ya katikati ya mkoa wa Shanxi, China, kilomita 90 ya kusini ya mji Taiyuan, mji mkuu wa Mkoa wa Shanxi Mji huo ni mji mdogo wa kale unaohifadhiwa kikamilifu zaidi kuliko mingine nchini China. Mji huo ulijengwa zaidi ya miaka 2700 iliyopita, ulikuwa na ustawi mkubwa zaidi katika enzi za Ming na Qing. Majengo mengi ya hivi sasa mjini humo ni mabaki ya enzi hizo mbili.

Tukipanda kwenye ukuta wa kale wa mji Pingyao tunaweza kuelewa zaidi hali ya mji huo. Mji wa Ping Yao una umbo la mraba, na eneo la kilomita 2.25 tu. Barabara iliyonyooka toka kusini hadi kaskazini inapita katikati ya mji na inakutana na barabara nyingine iliyonyooka kutoka mashariki hadi magharibi kwenye kitovu cha mji. Barabara hizi mbili ndio mawasiliano pekee katika mji huo. Paa za rangi ya manjano za makazi ya maofisa wa kifalme na mahekalu na paa zenye rangi za kijivujivu za nyumba za wananchi wa kawaida, zinaonyesha wazi matabaka za watu katika jamii ya zamani nchini China.

Katika mji huo kuna barabara 4, njia 8 na vichochoro 72 ambavyo vinapitana, lakini mipangilio inaonekana wazi. Nyumba nyingi za makazi ya raia zilijengwa katika Enzi ya Ming na Qing ambapo hadi sasa zimefikia miaka zaidi ya 600, nyumba zina safu kadhaa ambazo mtindo huo ni kama ua wenye nyumba pande nne mjini Beijing, lakini unaonekana wenye mafumbo zaidi, kati ya mabaki ya nyumba hizo zaidi ya 4000, hadi sasa zilizobaki nzima ni zaidi ya 400. Makazi katika mji wa Ping Yao ni nyumba zilizojengwa kwenye pande nne zikiacha uwazi katikati, huu ni mtindo wa ujenzi wa kaskazini mwa China, ambao huwa na mstari katikati, na pande mbili za mstari huo zinalingana, aghalabu nyumba huwa na safu mbili au hata tatu kutoka nje hadi ndani. Karibu na nyumba kuna ukuta mrefu kiasi cha mita 8 hivi bila ya dirisha ili kukinga upepo wenye mchanga. Kwenye milango na madirisha kuna michongo makini ikionesha upendo au matumaini mema ya wenye nyumba.

Nyumba hizo zilizobaki zimeonesha ustawi wa Enzi ya Ming na Qing za China ya kale, hivi sasa nyumba hizo nyingi zimekuwa mahoteli yanayowapokea watalii, watalii wengi wanapenda kukaa katika mahoteli hayo ambayo yote ni majengo yenye mitindo asilia ya zama za kale.

Tukizungumzia mahoteli ya mjini Pingyao, kwanza tungetaja hoteli ya Tianyuakui. Hoteli hiyo iko umbali wa mita mia kadhaa tu toka katikati ya mji wa Pingyao, hoteli hiyo imeonesha mtindo wa ujenzi wa nyumba zilizojengwa katika zama za kale. Tianyuankui ilikuwa nyumba ya mfanyabiashara ambayo ilijengwa zaidi ya miaka 200 iliyopita, ambapo mji huo ulikuwa katika kipindi cha ustawi wa uchumi, wafanyabiashara wote waliokuwa mjini humo, kila mmoja wao alikuwa na nyumba ya kuishi inayofanana na nyumba hiyo.

Tukiingia ndani ya hoteli ya Tianyuankui, tutajihisi mara moja harufu nzito ya zama za kale. Kwenye ua wa nyumba hiyo, kuna sakafu iliyojengwa kwa matofali ya rangi ya kijivu, kwenye ukumbi wa nyumba kuna meza ya mraba na viti virefu vilivyotengenezwa kwa mbao, ambavyo vinaonesha umaalum wa zamani za kale. Na taa nyekundu za kichina zinaning'inia mlangoni, kwenye madirisha kuna michongo ya sanaa za ukataji wa karatasi, yote hayo yameonesha desturi za maisha ya wakazi wa mkoa wa Shanxi, na kwenye milango na mihimili ya madirisha ya mbao kuna nakshi zilizochongwa kwa ustadi mkubwa, hali ya kifahari na utajiri ya maisha ya mfanyabiashara wa zama za kale imeonekana dhahiri. Mtalii Bwana Wang Da aliyekaa kwenye hoteli hiyo kwa siku kadhaa alisema:

Kila kitu ni kigeni kwangu katika chumba cha hoteli hiyo, kuna samani ya mbao ya mtindo wa enzi za Ming na Qing, michoro na maandiko ya kichina yalibandikwa kwenye ukuta wa chumbani, vilevile kuna televisheni ya rangi na chombo cha kurekebisha joto, chumba ni safi sana, na kinachotuvutia ni kitanda cha zamani, kitanda hicho ni kikubwa kilichojengwa kwa matofali, kuna nafasi za kulala kwa watu watano hivi, tunaona raha sana. Niliwahi kuishi pia katika hoteli nyingine iitwayo Yide iliyoko karibu na Hoteli Tianyuankui, naona Hoteli Yide pia ni hoteli yenye mtindo wa kipekee.

 

Mahoteli hayo mawili Yide na Tianyuakui yalijengwa katika enzi moja, mahoteli hayo mawili yalikuwa makazi ya Bwana Hou Wangbing ambaye alikuwa mwenye benki wa zama alizokuwa anaishi. Makazi hayo yana nyumba 6, na kila nyumba ina vyumba kadhaa za kuwapokea wageni, ndani ya vyumba kuna samani nzuri, kwenye samani hizo kuna nakshi na michoro ya rangi za kupendeza, ambazo zinaonesha utajiri wa bwana wa makazi hayo. Mwalimu Xu Linjie wa Chuo kikuu cha Beijng ametembelea Mji wa Pingyao mara kadhaa, kila mara anachagua kukaa kwenye Hoteli ya Yide. Alisema, mahoteli ya mjini Pingyao kwa jumla ni yenye mtindo wa namna moja, lakini kila hoteli ina hali yake ya kupendeza. Kwa mfano, Hoteli ya Yide inaonesha zaidi utamaduni wa mji wa Pingyao. Alisema:

Katika hoteli hiyo, kila kitu cha zama za kale kinahifadhiwa vizuri, kwa mfano mawe ya aina mbalimbali yaliyosalia kwenye ua yanatuvutia sana, nilipokaa katika hoteli hiyo, kila siku nilitembea kwenye ua, niliona kama nilitembelea kwenye maonesho ya vitu vinavyoonesha mila na desturi za wakazi wa mji wa kale.

Na Makazi ya Yamenguanshe yaliyobaki ya zamani ni sehemu iliko hoteli ya vijana ya hivi sasa mjini Pingyao. Katika zama za kale, makazi hayo yalikuwa yanawapokea maofisa waliofika mjini humo. Makazi ya Yamenguashe yako kwenye kiini cha mji wa Pingyao ni karibu sana na Jumba la maonesho la wilaya. Katika hoteli hiyo kuna baa yenye mtindo pekee, ambapo mbali na vitu vya lazima ndani ya baa, pia kunaandaliwa vitabu na video ya filamu. Wateja wakiingia baa, wanaweza kuona wamefika kama nyumbani kwao, kila kitu kwenye baa wanaweza kukitumia kama wanavyopenda. Mhudumu wa baa hiyo Bi. LuoYaping alimwambia mwandishi wetu wa habari kwamba, zamani baa hiyo ilikuwa ukumbi mkubwa wa kuandalia tafrija, akisema:

Zamani za kale maofisa wakuu waliokuja Pingyao waliandaliwa tafrija kwenye ukumbi huo, ukumbi huo ulionekana ni mkubwa sana katika zama za kale.

Wasikilizaji wapendwa, hivi sasa wakati miji mingi ya kale ya utamaduni inapoharibika kutokana na maendeleo ya shughuli za biashara, mji mzima wa kale Pingyao unahifadhiwa vizuri na kuwaonesha watalii maendeleo yasiyo ya kawaida ya utamaduni, jamii na uchumi wake, kweli ni jambo la kufurahisha.

Idhaa ya Kiswahili 2006-06-05