Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-05 17:56:42    
Mgongano kati ya Fatah na Hamas kufikia kikomo

cri

Ofisa wa kundi la chama cha ukombozi wa taifa cha Palestina (Fatah), tarehe 4 alisema endapo kundi la Hamas hakitakubali mapendekezo ya kisiasa ya kuanzisha nchi kwenye ardhi ya Palestina inayokaliwa, mwenyekiti wa mamlaka ya taifa ya Palestina Bw. Mahmoud Abbas ataamua ufanyike upigaji kura kuhusu mapendekezo hayo. Siku hiyo waziri mkuu wa serikali ya Palestina Bw. Ismail Haniyeh akitoa hotuba alisema, hatua hiyo inayochukuliwa na Abbas si halali. Mchambuzi alisema mambo hayo yanaonesha kuwa mgongano wa kisiasa kati ya Abbas na Hamas unakaribia kufikia kileleni kabisa.

Tarehe 11 mwezi Mei viongozi wa vyama husika vya Palestina waliotiwa kizuizini na Israel, walisaini "makubaliano ya gerezani" yenye madhumuni ya kuanzisha nchi ya Palestina sambamba na Israel kwenye mpaka kati ya pande hizo mbili uliokuwepo kabla ya vita ya mashariki ya kati ya mwaka 1967. Endapo Hamas inakubali masharti hayo ya kisiasa, inamaanisha kuwa itabadilisha wazo lake la kimsingi la kisiasa, na kuitambua Israel. Tarehe 25 mwezi Mei, Bw. Abbas alitangaza kuwa endapo chama cha Hamas hakitakubali "makubaliano ya gerezani" kuhusu mustakabali wa taifa ndani ya siku 10, ataamua kufanya upigaji kura wa watu wote kuhusu makubaliano hayo ndani ya siku 40.

Wachunguzi wa suala la Palestina walisema Bw. Abbas ameweka tumaini kubwa kuhusu pendekezo la upigaji kura akitaka kuondoa mgongano ndani ya Palestina kwa kutumia njia hiyo, kupunguza vikwazo vya kiuchumi na upinzani wa kisiasa wa nchi za magharibi juu ya Palestina, na kuanzisha mazingira ya kurejesha mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel. Kwa kukabiliwa na pendekezo hilo, kundi la Hamas limebanwa katika hali ya kutoweza kwenda mbele wala kurudi nyuma.

Kwanza, "makubaliano ya gerezani" yalisainiwa kwa pamoja na viongozi wa vyama husika vya Palestina waliofungwa gerezani na Israel wakiwemo viongozi wa Hamas, ambao wanachukuliwa na watu wa Palestina kuwa ni mashujaa katika mapambano dhidi ya Israel, wanaheshimiwa sana na watu, na pendekezo lao la kisiasa linaonesha wazo la jamii ya Palestina. Kura za maoni ya watu zilizopigwa hivi karibuni zinaonesha kuwa 90% ya watu wa Palestina wanaunga mkono makubaliano hayo ya gerezani. Hivyo ni vigumu kwa Hamas kuyakataa.

Pili, hivi sasa mapambano ya kisiasa kati ya Fatah na Hamas yamepamba moto. Wakati huo huo, uhusiano kati ya Palestina na Israel umefikia kiwango cha chini kabisa, vikwazo vya kiuchumi na upinzani wa kisiasa wa nchi za magharibi umeifanya Palestina kukaribia kupooza kabisa. Katika mazingira hayo, watu wengi wanachukulia pendekezo alilotoa Bw Abbas la kufanya upigaji kura kuwa njia muhimu ya kujinasua kwa Palestina. Kura za maoni zinaonesha, 70% ya waungaji mkono wa chama cha Hamas wanavutiwa na upigaji kura za maoni, hata chama cha Islamic Jihad chenye msimamo mkali hivi karibuni pia kilisema kitaunga mkono upigaji kura za maoni.

Aidha kura za maoni zilizopigwa hivi karibuni zinaonesha kuwa hivi karibuni uungaji mkono kwa Bw. Abbas na Fatah unaongezeka kwa haraka, wakati uungaji mkono kwa Hamas unapungua siku hadi siku na kufikia 29% kutoka 42%. Licha ya hayo maandamano yalifanyika kwa mfululizo katika miji mbalimbali ya Palestina, yakidai serikali inayoongozwa na kundi la Hamas ilipe mishahara ya miezi kadhaa inayodaiwa, na kufanya chama cha Hamas kukabiliwa shinikizo kubwa kabisa la kisiasa.

Wachunguzi wanaona, kundi la Hamas bado lina wasiwasi kuhusu pendekezo la kufanya upigaji kura za maoni. Waziri mkuu wa serikali ya Palestina Bw Ismail Haniyeh alisema tarehe 4 kuwa pendekezo la kufanya upigaji kura za umma si halali, lakini alisema anakubali kumaliza mgogoro kwa mazungumzo na Bw Abbas.