Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-06 15:38:03    
Sekta ya uchapishaji nchini China yastawi katika miaka ya karibuni

cri

Ukipata nafasi ya kutembelea maduka ya vitabu nchini China utaona aina nyingi za vitabu vikiwa ni pamoja na vitabu vya utamaduni, historia, sayansi ya jamii, kimaisha, ufahamu wa mambo, pamoja na mambo yanayopendwa na watu hivi sasa. Vitabu hivyo vinahusu kuimarisha afya kwa wazee, elimu ya watoto kwa wazazi, hadithi za watoto, michoro ya katuni na michoro inayokosoa.

Jengo la vitabu la Beijing ni moja ya maduka makubwa ya vitabu nchini China kwa uuzaji wa rejareja, kila siku duka linapofunguliwa asubuhi, wanunuzi wengi wanamiminikia ndani kama maji ya mto yanavyoingia katika bahari ya vitabu. Watu licha ya kuweza kupata vitabu wanavyotaka, wanaweza pia kuhisi mabadiliko ya soko la vitabu.

Bw. Wang Heng, ambaye aliingia dukani kununua vitabu, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa siku hizi, majalada ya vitabu yamekuwa tofauti sana na yale ya zamani.

"Maendeleo makubwa! Vitabu vya hivi sasa ni vizuri sana, iwe katika uchapishaji au utengenezaji wake umepiga hatua kubwa, siyo tu kuwa vimechapishwa vizuri bali vimepambwa vizuri, na ni tofauti sana na vile vya miaka michache iliyopita."

Msichana Li Fen alibabaika mbele ya vitabu vya aina nyingi, alisema,

"Hivi sasa kuna vitabu vingi vya aina mbalimbali, msomaji anaweza kupata kitabu chochote anachotaka."

Katika miaka ya karibuni mauzo ya jengo la vitabu la Beijing yanadumisha ongezeko la 20% kwa mwaka, na mauzo ya mwaka jana yalifikia Yuan za renminbi milioni 440. Takwimu zinaonesha kuwa, vitabu vya aina elfu 220 vilichapishwa nchini China mwaka 2005, vikiwa ni ongezeko la karibu 8% kuliko mwaka uliopita na ni mara zaidi ya 10 ikilinganishwa na vile vya mwaka 1978.

Ustawi wa soko la vitabu wa hivi sasa ni tofauti kabisa na hali ya kuzorota kwa uchapishaji katika sehemu mbalimbali nchini kati ya miaka ya 80 na 90 ya karne iliyopita. Wakati ule mengi ya mashirika ya uchapishaji ya serikali hayakuwa na wazo la kupata faida, na vitabu vilivyochapishwa havikuweza kukidhi mahitaji ya watu.

Ili kuendana na utashi wa uendelezaji wa uchumi wa kimasoko, tokea mwishoni mwa karne iliyopita China ilizindua mageuzi ya soko la uchapishaji, ambapo mashirika ya uchapishaji ya China yalianza kubadilisha mifumo yao na kujitahidi kuchukua nafasi muhimu ya soko hilo, na yaliibuka mashirika mengi ya uchapishaji yenye uwezo wa ushindani katika sekta ya uchapishaji. Kampuni ya uchapishaji ya China iliasisiwa rasmi mwaka 2002 baada ya kuunganisha mashirika zaidi ya 10 ya uchapishaji ya nchini. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya uchapishaji ya China Bw. Yang Muzhi alipozungumzia wazo lao la kuanzisha kampuni hiyo alisema,

"Lengo letu lilikuwa ni kustawisha mfumo wa sekta ya uchapishaji na kuwa na uvumbuzi ili kuanzisha kampuni moja yenye nguvu na hamasa. Baada ya jitihada za miaka mitatu hadi mitano, kampuni yetu itatia fora na kuwa kama "manowari inayobeba ndege" katika sekta ya uchapishaji nchini China."

"Manowari inayobeba ndege" hiyo yenye rasilimali kubwa katika sekta ya uchapishaji ilionesha nguvu zake kubwa mara tu baada ya kuingia sokoni, na ilichapisha vitabu vingi vya kiwango cha juu kielimu. Mwaka 2004, kampuni ya uchapishaji ya China ilichapisha mkusanyiko wa utamaduni wa China ukiwa ni pamoja na vitabu vya fasihi, historia, falsafa, sayansi, sanaa, vitabu vya kuongoza na vitabu vya tafsiri za vitabu vya nchi za nje, mkusanyiko huo wa utamaduni wa China ni wa kwanza kwa ukubwa hivi sasa nchini China. Hivi leo, kampuni hiyo ya uchapishaji inachukua zaidi ya 7% ya nafasi ya soko la uchapishaji nchini China.

Sawa na kampuni ya uchapishaji ya China, katika harakati za mageuzi nchini China yaliibuka mashirika mengi mapya ya uchapishaji yenye nguvu kubwa ya ushindani katika soko la uchapishaji. "Taarifa ya soko la uuzaji bidhaa kwa rejareja" inaonesha kuwa wastani wa ongezeko la mali za kampuni 7 ikiwemo kampuni ya uchapishaji ya China umefikia 24% kwa mwaka, na kuongoza katika sekta ya uchapishaji nchini China.

Baada ya kujiimarisha kwenye masoko ya nchini, kampuni za uchapishaji za China zinatumia mkakati wa kujiendeleza katika nchi za nje na kushiriki kwenye ushindani duniani. Maonesho ya Frankfurt yanayofanyika kila mwaka ni maonesho ya vitabu na soko la hakimiliki ya kielimu la kwanza kwa ukubwa duniani kwa hivi sasa. Asilimia 75 ya biashara ya hakimiliki ya kielimu inafanyika katika mji huo, na ni jukwaa la kuonesha maendeleo ya sekta ya uchapishaji ya nchi mbalimbali. Katika miaka iliyopita, maonesho ya vitabu ya China yalikuwa yanatembelewa na watu wachache sana kutokana na uchache wa vitabu na shughuli za biashara. Lakini katika maonesho ya vitabu ya mwaka huu, vitabu vingi vilivyooneshwa ni vipya kabisa, ambavyo vitabu vya kichina na Kiingereza, pamoja na vitabu vyenye lugha hizo mbili kwa pamoja ni aina zaidi ya elfu mbili, na kuwa maonesho yaliyovutia watu kwa wingi.

Katika maonesho ya miaka iliyopita, haki za uchapishaji ilizonunua China kutoka nchi za nje zilikuwa mara kumi kuliko haki za uchapishaji za China zilizonunuliwa na nchi za nje, na hakukuwa na uwiano kabisa. Katika maonesho ya vitabu ya mwaka huu, China ilinunua haki za uchapishaji 881, lakini haki za uchapishaji za China zilizonunuliwa na nchi za nje zilifikia 615, ikilinganishwa na hali ya maonesho ya mwaka uliotangulia, ambayo China ilinunua haki za uchapishaji 1,400, na haki za uchapishaji za China zilizonunuliwa na nchi za nje zilikuwa mia 1 na kidogo tu, hatua ambayo imepunguza pengo lililopo na kuongeza nafasi ya vitabu vya Chika katika soko la kimataifa.

Mkurugenzi wa ofisi ya sera na sheria ya idara kuu ya habari na uchapishaji ya China Bw. Wang Tao alisema, "Hii ni hali ya kufurahisha, ambayo haikutokea katika miaka mingi iliyopita, lakini maendeleo hayo yametokana na nini? Maendeleo hayo yanatokana na kuimarika kwa uwezo wa uvumbuzi kwa mashirika ya uchapishaji ya China. Katika biashara ya haki za uchapishaji, kama wewe huna uwezo wa uvumbuzi, ukitaka kuuza vitabu vyako watu hawataki kununua vitabu vyako. Hatua za maendeleo za sekta ya uchapishaji ya China zinaonesha kuwa sekta ya uchapishaji ya China imeimarika na uwezo wake umekuzwa katika harakati za mageuzi na uvumbuzi."

Katika muda usio mrefu wa miaka zaidi ya 10, sekta ya uchapishaji ya China imebadilika kufuata utaratibu wa uchumi wa soko huria kutoka utaratibu wa uchumi wa kimpango, hususan ni kwamba imefikia hatua ya kuweza kushindana na kampuni za nchi za nje katika soko la kimataifa. Kutokana na mabadiliko hayo, tumeona kuimarika kwa sekta ya uchapishaji ya China, pia tumeona ustawi wa soko la vitabu. Pamoja na kuendelezwa zaidi kwa mageuzi ya sekta ya uchapishaji, sekta ya hiyo ya China hakika itakuwa na mustakabali mzuri zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-06