Mkutano wa 6 wa Baraza la wakuu wa Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai unatazamiwa kufanyika huko Shanghai, China kuanzia tarehe 15 mwezi huu. Katibu mkuu wa jumuiya hiyo Bwana Zhang Deguang alisema tarehe 6 kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa, mkutano huo ni tukio muhimu katika mchakato wa maendeleo ya jumuiya hiyo, pia ni jambo kubwa katika sehemu ya Ulaya na Asia na katika maisha ya kisiasa duniani. Mkutano huo hakika utapata mafanikio mema.
Bwana Zhang alisema, huu ni mkutano wa kuadhimisha miaka 5 tangu Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai ianzishwe, pia ni mkutano wa kawaida wa wakuu wa jumuiya hiyo. Alisema:
Kwenye mkutano huo, nchi wanachama wa jumuiya hiyo zitakumbusha na kujumuisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita, na maarifa yaliyopatikana katika shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo, kuthibitisha malengo ya kuanzisha ushirikiano katika sekta mbalimbali siku zijazo, na kubadilishana maoni kuhusu masuala makubwa ya kimataifa na kikanda.
Bwana Zhang alidokeza kuwa mkutano huo utapitisha azimio muhimu na kutoa maagizo muhimu kuhusu kuzidisha ushirikiano kwenye sekta za usalama na kusukuma mbele ushirikiano katika sekta za uchumi, biashara na utamaduni.
Alipojumuisha maarifa ya maendeleo katika miaka mitano iliyopita tangu jumuiya hiyo ianzishwe, Bwana Zhang alisema kupata maendeleo ya haraka kwa jumuiya hiyo kutokana na sababu tatu, kwanza nchi wanachama zimeshikilia nia na kanuni za jumuiya hiyo; pili nchi wanachama zimeshikilia bila kulegea kanuni za kutolenga nchi nyingine ya tatu, kutolenga sehemu nyingine na kutofungamana na upande wowote; tatu, nchi wanachama zinashikilia moyo wa kufanya juhudi za ushirikiano kwa kufuata hali halisi. Alisema:
Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai siyo klabu ya kupiga soga, tangu ianzishwe viongozi wa nchi wanachama wanatilia maanani moyo wa kufanya juhudi za ushirikiano kwa kufuata hali halisi, tena kutafuta matokeo halisi na ufanisi halisi.
Bwana Zhang alisema katika miaka mitano iliyopita, jumuiya hiyo haikutoweka, kubomolewa au kudhoofishwa kama baadhi ya watu walivyobashiri, sababu muhimu ni kuwa nchi wanachama siku zote zinashikilia "Moyo wa Shanghai" unaoonesha kwa jumla nia na kanuni za Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai. Alisema:
Tunatilia maanani zaidi umuhimu wa Moyo wa Shanghai. Tunauchukulia moyo huo kama dawa ya kuunganisha nchi wanachama, kama chanzo cha kukusanyika na kama chemchem ya moyo, moyo huo unahusiana na mtizamo wetu wa pamoja kuhusu usalama, ustaarabu na maendeleo, kweli ni silaha ya jumuiya hiyo ya kujipatia mafanikio, vilevile ni uhakikisho wa kuifanya jumuiya hiyo iweze kujiendeleza katika dunia na kanda zinazokabiliwa na mabadiliko na changamoto mbalimbali.
Alipozungumzia mafanikio halisi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai katika sekta za uchumi na biashara, Bwana Zhang alisema jumuiya hiyo imeanzisha umoja wa mabenki, ili kutoa msaada wa kifedha kwa miradi ya ushirikiano wa kiuchumi. Mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo utakaofanyika hivi karibuni pia utaanzisha kamati ya wanakampuni wa Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai, ili kusaidia kuanzisha ushirikiano halisi wa kiuchumi.
Bwana Zhang Deguang alisema, Jumuiya ya ushirikiano ya Shanghai itapiga hatua imara na kufuata njia iliyochagua yenyewe kusonga mbele kwa ari kubwa. Jumuiya hiyo ni jumuiya ya aina mpya ya ushirikiano wa kikanda, ambayo ina mustakbali wake mpaka wa maendeleo, hadhi yake haiwezi kuchukuliwa na nyingine yoyote. Nchi zote wanachama zina imani kubwa juu ya hiyo.
|