Katibu wa kamati ya usalama ya Iran, ambaye ni mwakilishi wa kwanza katika mazungumzo ya suala la nyukilia, Bw. Ali Lirijani tarehe 6 huko Teheran, mji mkuu wa Iran alisema, mpango mpya wa mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 6 kuhusu utatuzi wa suala la nyukilia la Iran ni wenye hatua mwafaka. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Bw. Tony Snow siku hiyo alisema, mwitikio huo wa Iran ni wa kufurahisha, unaonesha kuwa Iran itajadili kwa makini mpango huo mpya wa utatuzi wa suala la nyukilia la Iran.
Hayo ni maneno yaliyosemwa na Bw. Larijani huko Teheran wakati alipokuwa na mazungumzo na kukabidhiwa mpango mpya na Bw. Javier Solana, mjumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia sera za kidiplomasia na usalama, ambaye hivi sasa anafanya ziara nchini Iran. Bw. Lirijani alisema mazungumzo yao ni yenye ufanisi, Iran itatoa majibu rasmi baada ya kufanya utafiti kuhusu mpango huo mpya. Alisema ziara ya Bw. Solana inaonesha nia ya nchi za Umoja wa Ulaya ya kutaka kutatua suala hilo kwa njia ya mazungumzo, ambayo inastahili kupongezwa. Bw. Solana alisema mazungumzo kati yake na viongozi wa Iran ni mazuri na yenye ufanisi.
Tarehe 1 mwezi huu, wawakilishi wa nchi 6 za Marekani, Russia, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani walikuwa na mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje huko Vienna na kufikia maafikiano. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Bibi Margaret Beckett kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mazungumzo alisema, wawakilishi wa nchi 6 wamekubali katika mazingira ambayo Iran inaacha kwa muda shughuli za kusafisha uranium, kutoa mpango unaoivutia Iran ukiwa ni msingi wa kurejesha mazungumzo kati ya Umoja wa Ulaya na Iran, wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liahirishe kuchukua hatua kuhusu suala la Iran. Habari zinasema mpango huo unaunga mkono mpango wa matumizi ya nyukilia yasiyo ya kijeshi wa Iran, ukiwa ni pamoja na kujenga kinu cha nyukilia cha maji mepesi nchini Iran kutokana na mradi wa ushirikiano, na kujenga zana za kuweka akiba ya nishati ya nyukilia ili kuhakikisha mahitaji ya Iran kuhusu nishati ya nyukilia yanatoshelezwa. Mpango huo pia unaiunga mkono Iran ijiunge na shirika la biashara duniani, WTO. Marekani nayo iko tayari kuiuzia Iran teknolojia ya kilimo na ndege za abiria.
Kutokana na Marekani kutumia sera za kuweka vikwazo na uhasama dhidi ya Iran katika muda mrefu uliopita, tena msimamo wake ulikuwa mgumu siku zote, hivyo jitihada za pande mbalimbali husika kuhusu suala la nyukilia la Iran hazikupata mafanikio, na mgongano kati ya Marekani na Iran katika kipindi fulani ulikuwa mkali. Kutokana na jitihada ya jumuiya ya kimataifa, hususan za Russia, China na Ujerumani za kutatua suala la nyukilia la Iran kwa njia ya kidiplomasia, na Marekani kukabiliwa na shinikizo kutoka ndani na nje, ilirekebisha sera zake, ikakubali kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana kwa masharti ya Iran kuacha shughuli za kusafisha uranium. Mabadiliko ya Marekani yameleta uwezekano kwa jumuiya ya kimataifa wa kutatua suala la nyukilia la Iran kwa njia ya amani.
Wachambuzi wanaona kuwa kutolewa kwa mpango wa nchi 6 kunathibitisha kanuni ya kupewa kipaumbele kwa mazungumzo ya kidiplomasia kuhusu suala la nyukilia la Iran, na kuleta maendeleo mazuri kwa majadiliano ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la nyukilia la Iran katika muda wa karibu mwezi mmoja. Matokeo hayo yamepatikana kwa shida. Kutatua suala la nyukilia la Iran kwa njia ya kidiplomasia kunaendana na maslahi ya pande zote mbili za Marekani na Iran, pia ni mahitaji ya maendeleo na amani ya dunia kwa hivi sasa. Iran ikiwa ni nchi inayohusika moja kwa moja na suala la nyukilia la Iran, mwitikio wake kuhusu mpango mpya wa nchi 6, na vitendo vya Marekani vinaonesha kuwa mpango mpya wa nchi 6 umeleta fursa mpya kwenye utatuzi wa suala la nyukilia la Iran kwa njia ya kidiplomasia.
|