Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-07 20:42:58    
China yatia mkazo katika kinga na udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu

cri

Maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu yamewahi kuenea kote duniani na mamilioni ya watu walikufa kutokana na ugonjwa huo. Katika miaka ya 50 ya karne ya 20, kutokana na maendeleo ya matibabu na dawa na kuboreka kwa mazingira ya afya, hali ya maambukizi ya ugonjwa huo imedhibitiwa kiasi. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na baadhi ya nchi kupuuza kazi ya kinga na udhibiti wa ugonjwa huo, kupunguza fedha zinazotengwa kwa ajili ya kazi hiyo, pamoja na ongezeko la idadi ya watu na idadi ya watu wanaohamahama, maambukizi makubwa yanawezekana kuibuka tena.

Tukizungumzia ugonjwa wa kuambukiza, tungefikiria magonjwa ya homa ya mafua na homa ya manjano (hepatitis), ni wachache tu wanaweza kufikiria ugonjwa wa kifua kikuu. Ugonjwa wa kifua kikuu unatokana na vijidudu vya kifua kikuu kwenye mapafu. Ugonjwa huo uliwahi kuibuka nchini China na kuathiri vibaya usalama wa maisha ya watu wa China. katika miaka ya 50 hadi 60 ya karne iliyopita, serikali ya China iliimarisha kazi ya kinga na udhibiti wa ugonjwa huo, na kuchukua hatua nyingi za kukinga na kutibu ugonjwa huo, hali ya maambukizi ya ugonjwa huo ikadhibitiwa kiasi.

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na sababu mbalimbali, maambukizi ya ugonjwa huo yameanza kutokea tena nchini China. naibu waziri wa afya wa China Bw. Wang Longde alisema,

"hivi sasa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu nchini China ni mbaya nchini China, na China ni moja kati ya nchi 22 duniani zilizoathiriwa vibaya na ugonjwa huo, idadi ya wagonjwa wa kifua kikuu nchini China inachukua nafasi ya pili kote duniani baada ya India."

Takwimu zilizofanywa na wizara ya afya ya China zinaonesha kuwa, hivi sasa China ina wagonjwa wa kifua kikuu zaidi ya milioni 4.5, ikichukua asilimia 0.34 ya idadi ya watu wa China. kila mwaka watu wapatao laki 1.3 wanakufa kutokana na ugonjwa huo, idadi hiyo imezidi jumla ya idadi ya watu waliokufa kutokana na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Katika miaka ya 50 ya karne iliyopita, kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kwa njia ya kutoa chanjo ya BCG kuliwahi kuwekwa kwenye mpango wa taifa wa kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, na kila mtoto alipewa chanjo hiyo mara baada ya kuzaliwa. Lakini ni kwa nini bado kunatokea wagonjwa wengi wapya wa kifua kikuu? Wataalamu wameeleza kuwa, hatua za kimsingi za kukinga ugonjwa huo ni kugundua na kutibu mapema ugonjwa huo, ili kupunguza vyanzo vya maambukizi ya ugonjwa huo.

Hivyo hatua ya kwanza ni kujitahidi kugundua mapema wagonjwa wa kifua kikuu. Ili kutafuta wagonjwa wa ugonjwa huo kwenye sehemu mbalimbali, serikali ya China imechukua hatua mbalimbali, zikiwemo kujenga vituo vya kupima ugonjwa huo, kuandaa watu wenye utaalamu na kuimarisha shughuli za kueneza ufahamu kuhusu ugonjwa huo. Mwezi Januari mwaka 2004, China ilianzisha utaratibu wa kutoa taarifa ya magonjwa ya kuambukiza yakiwemo kifua kikuu kote nchini.

Serikali ya China pia inatoa motisha kwa madaktari wa vijijini waliogundua wagonjwa wa kifua kikuu, na kuwahamasisha watoe taarifa kuhusu watu wanaosadikiwa kuwa na ugonjwa huo. Ofisa wa afya wa mji wa Xinmi mkoani Henan Bw. Jin Hongjian alieleza:

"madaktari wa vijijini wana hamu kubwa ya kutoa taarifa wakigundua wagonjwa wa kifua kikuu. Kila mwaka pia tunaenda vijijini kufanya ukaguzi, kama tukigundua wagonjwa wasioripotiwa, tunatoa adhabu kadhaa kwa madakatari hao."

Kutokana na hatua hizo, kiasi cha wagonjwa wa kifua kikuu wanaogunduliwa nchini China kimeongezeka kwa kasi. Mwaka 2003, kiasi hicho kilikuwa asilimia 39 tu, na kiasi hicho kilifikia asilimia 79 katika mwaka 2005.

Mbali na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaogunduliwa, hatua nyingine muhimu ni kuwatibu wagonjwa wa kifua kikuu.

Kuanzia mwaka 2001, China imeanza kutekeleza hatua kwa hatua sera za upimaji na matibabu ya kifua kikuu bila malipo. Ili kuhakikisha fedha zinazotumika katika matibabu ya wagonjwa wa kifua kikuu zinakuwepo, kila mwaka serikali kuu ya China inatenga fedha za yuan milioni 40 kwa ajili ya udhibiti wa ugonjwa huo, na mwaka 2004 serikali iliongeza fedha hiyo kufikia yuan milioni 300. mwezi Januari mwaka 2005, China ilianzisha mfumo wa usimamizi wa taarifa kuhusu kifua kikuu na kujenga kituo cha kuhifadhi mafaili ya kumbukumbu za wagonjwa wa kifua kikuu. Kutokana na misaada ya mfumo huo, idara za afya za China zinaweza kutoa matibabu kwa wagonjwa wa kifua kikuu wanaohamahama.

China inafuata mbinu ya matibabu ya ugonjwa huo iliyopendekezwa na shirika la afya duniani WHO, ambayo wagonjwa wanatakiwa kumeza dawa mbele ya wasimamizi. Bi. Qiu Cuili ni dakatari wa maabara ya kupima kifua kikuu kwenye hospitali moja ya Beijing, pia ni msimamizi wa matibabu ya wagonjwa wa kifua kikuu, alisema:

"ninawaambia wagonjwa wa kifua kikuu waje kwenye kituo cha huduma za afya na kumeza dawa mbele yangu kila siku. Kama wakiacha kutumia dawa hizo, watapatwa na tatizo la vijidudu kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo, tatizo hilo si kama tu litafanya hali ya ugonjwa wake kuwa mbaya zaidi, bali pia litapunguza nguvu ya dawa nyingine kwa mwili wake."

Kama Bi. Qiu Cuili alivyosema, jambo muhimu katika matibabu ya kifua kikuu ni kutosimamisha kutumia dawa. matibabu ya ugonjwa huo yatachukua muda mrefu, Kwa kawaida ni miezi sita, katika kipindi hiki, wagonjwa wakisimamisha mara moja au mbili basi vijidudu vya ugonjwa huo vinakuwa sugu kwa dawa hiyo. kwa wagonjwa wa kawaida, matibabu ya miezi sita yatagharamu yuan mia kadhaa. Lakini kwa wagonjwa ambao vijidudu mwilini mwo ni sugu kwa dawa, matibabu yanakuwa magumu zaidi na tena yanakuwa na gharama kubwa zaidi. Idadi ya wagonjwa ambao vijidudu mwilini mwao vimekuwa sugu kwa dawa nchini China hivi sasa inachukua robo ya idadi yote ya wagonjwa wenye tatizo hilo duniani, hivyo wizara ya afya ya China inataka kubadilisha hali hiyo kwa njia ya kutekeleza utaratibu wa wasimamizi wa matibabu ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Kwa ujumla, kutokana na serikali ya China kutilia maanani kinga na matibabu ya ugonjwa wa kifua kikuu, hali ya udhibiti wa ugonjwa huo nchini China imeboreka kidhahiri. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005, asilimia 91 ya wagonjwa wapya wa kifua kikuu nchini China wametibiwa, na hali hiyo imesifiwa na shirika la afya duniani WHO.