Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-08 20:00:32    
Rais wa Kyrgyzstan afurahia mustakabali wa maendeleo ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai

cri

Rais Kurmanbek Bakiyev wa Kyrgyzstan hivi karibuni katika Ikulu ya Bishkek alipohojiwa na waandishi wa habari wa vyombo 6 vya habari vya China kikiwemo cha Radio China Kimataifa, alijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu mkutano utakaofanyika huko Shanghai wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, pamoja na ziara ya kiserikali atakayofanya hivi karibuni nchini China.

Mkutano wa 6 wa baraza la wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai utafanyika tarehe 15 mwezi huu huko Shanghai, China. Mkutano huo wa wakuu wa nchi wa mwaka huu utafanyika katika siku ya kutimia miaka 5 tangu Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ianzishwe, na siku ya kutimia miaka 10 tangu mfumo wa nchi 5 wa Shanghai uanzishwe, ambao ni muundo ulioko kabla ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai. Licha ya kutoa pongezi kwa maendeleo ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, rais Bakiyev anafurahia mustakabali wa maendeleo ya jumuiya hiyo. Alisema,

"Kuasisiwa kwa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni jambo lenye athari kubwa kwa sehemu ya Ulaya, Asia na hata kwa dunia nzima. Mustakabali wa maendeleo ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni mkubwa, majukumu na malengo ya jumuiya hiyo pia ni mengi. Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai inataka kuinua kiwango cha maisha ya watu wa nchi za wanachama wa jumuiya hiyo, kulinda utulivu wa jamii na siasa wa nchi wanachama na kupanua ushirikiano katika maeneo ya sayansi, teknolojia na elimu kutokana na maendeleo endelevu ya uchumi ya jumuiya hiyo."

Rais Bakiyev alitoa mapendekezo halisi ya kuimarisha na kupanua ushirikiano wa nchi wanachama. Anaona kuwa ushirikiano wa kiuchumi ni kitu muhimu zaidi cha kuimarisha jumuiya hiyo, na kuboresha msingi wa sheria kutachangia kuimarisha na kukuza ushirikiano wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo. Kuanzishwa kwa mfumo mwafaka wa ushirikiano pamoja na nchi za Mongolia, Iran, Pakistan na India, ambazo ni nchi washiriki wa mkutano zikiwa ni wachunguzi, utahimiza harakati za Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kushughulikia mambo halisi zaidi. Rais Bakiyev alisisitiza ushirikiano wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo dhidi ya ugaidi. Alisema,

"Kyrgyzstan inaona, nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai zinatakiwa kujiweka tayari kuhusu tishio la ugaidi duniani na kupambana vikali na shughuli za ugaidi duniani. Mbali na hayo, nchi wanachama zinatakiwa kuimarisha ushirikiano wa ulinzi wa mipakani na idara za usalama za nchi wanachama, na suala linalotakiwa kufuatiliwa zaidi ni kuundwa kwa mfumo wa ushirikiano kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo."

Rais Bakiyev alisema kuimarisha umuhimu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kunaendana kabisa na maslahi ya nchi ya Kyrgyzstan, na pia ni kipaumbele kilichowekwa katika sera za nje za nchi hiyo. Alisema Kyrgyzstan itaendelea kujitahidi kuhimiza maendeleo ya jumuiya hiyo.

Kyrgyzstan ni jirani muhimu wa China, kuna mpaka wenye urefu wa kilomita zaidi ya 1,000 kati ya nchi hizo mbili. Uhusiano wa pande mbili umeendelezwa vizuri sana tangu kuanzishwa uhusiano wa kibalozi wa nchi hizo mbili mwaka 1992. Na rais Bakiyev anafurahia sana maendeleo ya uhusiano wa nchi hizo mbili, hususan maendeleo ya ushirikiano katika mambo ya uchumi na biashara.

Hivi sasa, Kyrgyzstan na China zimekuwa na ushirikiano mkubwa wa pande mbili, hususan ushirikiano kwenye mapambano dhidi ya magaidi, wafarakanishaji na watu wenye msimamo wa siasa kali.

Habari zinasema rais Bakiyev atafanya ziara ya kiserikali nchini China akiwa rais wa nchi, na atatumia fursa hiyo kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.