Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-08 20:37:03    
China yafanya sensa ya pili ya walemavu ili kuwahudumia vizuri zaidi wananchi wenye ulemavu

cri

Mwezi Aprili mwaka huu, sehemu nyingi nchini China zilikuwa zimeingia katika majira ya mchipuko na hali ya hewa ilikuwa inaelekea kuwa joto, lakini mabaki ya theluji bado yalikuwa yanaonekana katika mbuga mkoani Qinghai, magharibi mwa China. Bibi Miao Zirun mwenye umri wa miaka 20 ni mkazi wa wilaya inayojiendesha ya Gangcha ya kabila la Watibet mkoani humo. Siku hizi amekuwa akiendesha motokaa akitembelea nyumba za wafugaji moja baada ya nyingine zilizoenea hapa na pale mbugani.

Alikuwa akiwauliza wafugaji hali ya familia zao, mapato yao pamoja na hali ya afya zao, huku akiweka kumbukumbu.

Bi. Miao Zirun ni mfanyakazi wa kikundi cha sensa ya walemavu ya wilaya hiyo. Yeye na wenzake walikuwa wanafanya kazi ya sensa ya walemavu ambayo ni ya pili kufanyika nchini China. Kazi hiyo ilianza kote nchini tarehe mosi Aprili, miongoni mwa watu milioni 2.6 wanaochukua asilimia 2 ya watu wa China.

Sensa ya kwanza kama hii ilifanyika miaka 19 iliyopita. Lakini kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii pamoja na kuinuka kwa kiwango cha matibabu na afya, yametokea mabadiliko katika mambo yanayohusu wananchi walemavu, kama vile idadi ya walemavu, mahali wanapoishi, hali ya kupona kwa walemavu na hali yao ya ajira.

Naibu mkurugenzi wa ofisi inayoshughulikia sensa hiyo nchini China Bw. Chen Xinmin alisema 

 "Data na takwimu zilizopatikana katika sensa ya kwanza zimepitwa na wakati, hali ambayo inaleta matatizo kwa serikali katika kutunga mpango na sera kuhusu wananchi walemavu pamoja na utekelezaji na upimaji wa mipango na sera hizo, ndiyo maana imeleta shida mbalimbali katika kazi zinazohusiana na walemavu."

Mwandishi wetu wa habari akifuatana na kikundi kimoja cha wakaguzi cha Shirikisho la watu wasiojiweza la China, alitembelea wilaya ya Gangcha mkoani Qinghai, ambapo idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ni ndogo ikilinganishwa na eneo la wilaya hiyo. Umbali mkubwa kati ya makazi ya familia mbili ni zaidi ya kilomita 5. Mbali na hayo, eneo moja la kufanyiwa uchunguzi lipo kwenye uwanda uliopo mita 4,500 juu ya usawa wa bahari. Hali duni ya mawasiliano ilifanya kazi ya ukaguzi iwe ngumu. Kutokana na mabaki ya theluji yaliyokuwa yanayeyuka, wakaguzi walitembea kwa miguu katika njia inayojaa matope na maji, na iliwabidi wachukue tahadhari ili wasianguke.

Hata hivyo walifanya kazi kwa makini bila kujali hali ngumu. Mkaguzi mmoja Bi. Miao Zirun alisema, "Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kutembelea sehemu ya kijijini. Kwa ujumla nilifanya ukaguzi kwa makini bila uzembe. Naona ni jambo zuri kuwahudumia walemavu."

Nyumbani kwa mfugaji Yexin Angjie, wakaguzi walifahamishwa kuwa, bwana na mke wake wote ni walemavu, na mtoto wao mmoja ana matatizo ya kuongea. Kwa hiyo Bi. Miao Zirun aliwashauri wapimwe mwili siku iliyofuata katika kituo cha matibabu kilichoandaliwa na mpango huo wa sensa katika wilaya hiyo.

Katika kituo hicho cha matibabu, mkuu wake Bw. Wang Husheng alimwambia mwandishi wa habari kuwa, kuna wafanyakazi wanane, mbali na yeye mwenyewe, wengine 7 wote ni madaktari hodari kutoka hospitali za wilaya na kata pamoja na kliniki, ambao wanashughulikia matatizo ya kuona, kusikia, kuongea na matatizo mwilini, ubongo na akili. Na shirikisho la watu wasiojiweza la China limetoa zana za matibabu zenye thamani ya RMB elfu 20 kwa kituo hicho.

Bw. Wang alieleza kuwa, makumi ya wafugaji wanaosadikiwa kuwa na ulemavu wanakwenda kupimwa mwili kila siku. Kwa baadhi ya watu ambao hawataki kupimwa mwili, kada wa kijiji na wakaguzi wanafanya kazi kubwa ya kuwashawishi, na kwa wale wenye shida ya kutembea, madaktari wanachukua zana za matibabu na kwenda kuwapima nyumbani kwao.

Alisema  "Wale wanaoshindwa kuja, hata kama wanakaa mbali sana, tunawafuata kwenye makazi yao kwa motokaa. Kwa watu wenye ulemavu wa macho, daktari wa macho anawafuata, huku wale wenye matatizo ya mwili, daktari anayeshughulikia kupima ulemavu wa mwili anawafuata. Kwenye baadhi ya sehemu ambazo motokaa haziwezi kufikia, tunakwenda kwa miguu."

Bw. Wang pia alimwambia mwandishi wa habari kuwa, hivi sasa serikali imechukua hatua mbalimbali za kuwasaidia walemavu, kwa mfano walemavu wanarudishwa gharama za matibabu kwa asilimia 3 zaidi kuliko watu wasio na walemavu. Kila mwaka serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuwafanyia uapsuaji wa kurudisha uwezo wa kutizama watu maskini wenye ugonjwa wa mtoto wa jicho aina ya cataract, na watu wasioweza kusikia wala kuongea pia wanapewa mafunzo ya lugha ya ishara. Baada ya kupata matibabu ya kisasa, kumekuwa na walemavu wengi wanaopona hatua kwa hatua, na kuweza kujitegemea kiuchumi.

Mwandishi wetu wa habari alielezwa kuwa, sensa ya safari hii pia ni zoezi la kuwahudumia walemavu na kuwapatia misaada. Kwa mfano katika mikoa 12 ya sehemu ya magharibi ya China iliyo nyuma kimaendeleo, wananchi wanaothibitishwa kuwa na ulemavu katika sensa hiyo wanapewa mahitaji ya kila siku yakiwemo mablanketi.

Hadi kufikia katikati ya mwezi Mei, kazi ya uchunguzi katika sensa hiyo ilikuwa imekamilika kwa asilimia 70 hadi 80. Walemavu wengi walieleza kufurahia hatua hiyo, huku Bw. Lai Jingqiang mwenye umri wa miaka 63 anayeishi hapa Beijing, alisema, "Serikali inafanya sensa hiyo kwa lengo la kupata ufahamu wa hali ya maisha yetu na kutunga sera zinazohusika. Hatua hiyo inasaidia kuboresha maisha yetu."