Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-09 14:46:00    
Kansela wa China nchini Afrika ya kusini azungumzia ushirikiano wa nishati kati ya China na Afrika

cri

Tarehe 3 mwezi Juni mwaka huu, kansela wa ubalozi wa China aliyeko nchini Afrika ya kusini Bwana Zhou Yuxiao alihojiwa na mwandishi wa habari wa shirika la utangazaji la Uingereza BBC kuhusu uwekezaji kwenye sekta za uchumi na biashara na ushirikiano wa nishati kati ya China na nchi za Afrika, pamoja na uhusiano kati ya China na Sudan.

Bw. Zhou Yuxiao aliainisha kuwa, urafiki kati ya China na nchi za Afrika ulianzia tangu enzi na dahari, uchumi wa pande hizo mbili unasaidiana na kunufaishana, na nchi hizo zote zinakabiliana na jukumu la kuharakisha maendeleo ya uchumi na kuwanufaisha wananchi wake, hivyo ushirikiano wenye usawa kati ya China na nchi za Afrika katika sekta za uwekezaji na biashara, hakika ni wa kunufaishana. Katika miaka ya karibuni, mawasiliano ya kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika yameongezeka haraka, thamani ya biashara inaongezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka 2005, thamani ya biashara kati ya China na nchi za Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 40, ingawa thamani hiyo inaongezeka kwa haraka, lakini inachukua asilimia 3 tu ya jumla ya thamani ya biashara kati ya China na nchi za nje.

Katika miaka ya karibuni uwekezaji wa makampuni ya China katika nchi za Afrika unaongezeka kwa kiasi kikubwa. Kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China, baadhi ya makampuni ya China yamekuwa na uwezo wa kupanua shughuli zao katika nchi za nje, na nchi za Afrika pia zinakaribisha uwekezaji wa China, uwekezaji wa makampuni ya China si kama tu umeleta mitaji kwa nchi za Afrika, bali pia umesaidia kuboresha miundo mbinu, na kuongeza nafasi za ajira barani Afrika. Kwa ujumla ushirikiano wa kusaidiana na kunufaishana umekuwa msingi imara wa uwekezaji na biashara kati ya China na nchi za Afrika. China bado ni nchi inayovutia uwekezaji kwa wingi kutoka nchi za nje duniani, uwezo wa makampuni ya China kuwekeza katika nchi za nje bado ni mdogo. Kwa mfano uwekezaji wa makampuni ya Afrika ya kusini nchini China ni mkubwa zaidi kuliko uwekezaji wa makampuni ya China nchini Afrika ya kusini.

Bw. Zhou Yuxiao alisisitiza kuwa ni jambo la kawaida kwa China na nchi za Afrika kufanya ushirikiano wa nishati wa kunufaishana. Nchi za Afrika zina rasilimali nyingi, kuimarisha ushirikiano na nchi za nje katika sekta ya nishati na rasilimali kutazisaidia nchi hizo kuboresha mazingira yake ya biashara, na kuhimiza ongezeko la uchumi nchini, hii inaambatana na maslahi ya nchi za Afrika.

Bw. Zhou Yuxiao alisema China ina idadi kubwa ya watu, inakabiliwa na changamoto kubwa ya nishati, hivyo ni jambo linaloeleweka kwa China kuingiza rasilimali na nishati kutoka nje. Jambo linalotakiwa kuelewa zaidi ni kwamba, China si kama tu ni nchi inayotumia nishati kwa wingi, bali pia ni nchi inayozalisha nishati kwa wingi, kimsingi inaweza kujitosheleza kwa mahitaji ya nishati. Tegemeo la China kwa nishati ya nchi za nje ni ndogo zaidi kuliko nchi zilizoendelea. Mwaka 2005, Marekani iliagiza tani milioni 640 za mafuta kutoka nje, yaani mapipa 13 ya mafuta kwa mtu mmoja kwa wastani, Umoja wa Ulaya uliagiza tani milioni 670 za mafuta kutoka nje, yaani mapipa 65 kwa mtu mmoja kwa wastani, China iliagiza tani milioni 160, inalingana na mapipa 1.3 kwa mtu mmoja kwa wastani. Hivyo usemi kuhusu tishio la nishati la China hauna msingi wowote.

Alipoulizwa kuhusu uhusiano kati ya China na Sudan na nchi nyingine za Afrika, Bw. Zhou Yuxiao alisema China ni nchi inayowajibika na kufuata kanuni zilizowekwa, siku zote inafuata kwa makini kanuni zilizowekwa kwenye katiba ya Umoja wa Mataifa na utaratibu wa kimataifa wa kukuza uhusiano kati yake na nchi za nje. China siku zote inashikilia kukuza uhusiano wa kawaida na nchi za nje kwa msingi wa kanuni tano za kimsingi za kuishi pamoja kwa amani. China haioni kuwa, kuilaani, kuitenga nchi fulani kutoka jumuiya ya kimataifa, hasa kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi yenye mamlaka ni njia mwafaka ya kuhimiza kuboresha utawala wa nchi hiyo. China siku zote inajitahidi kutumia njia yake pekee kuzihimiza nchi za Afrika ziinue kiwango cha utawala. Kuimarisha mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi kadhaa za Afrika hakumaanishi kuwa, China inaunga mkono kikamilifu sera zote za nchi hizo.

Bw. Zhou Yuxiao pia alijulisha hali husika ya China kufanya ushirikiano na nchi za Afrika katika sekta mbalimbali. Alisema kutokana na waraka wa sera ya China kwa Afrika uliotolewa mwezi Januari mwaka huu, China itazisaidia nchi za Afrika kwa kupunguza madeni yao, kuzipatia mikopo nafuu, kuandaa mafunzo ya nguvu kazi na kuimarisha ushirikiano katika sekta za kilimo, utamaduni na elimu. Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika litafanya mkutano wa wakuu mwezi Novemba mwaka huu hapa Beijing, ambapo viongozi wa China na nchi za Afrika watajadiliana kwa pamoja mpango wa kufanya ushirikiano wa kirafiki kati ya China na nchi za Afrika katika hali mpya, hii itakuwa jambo muhimu sana katika uhusiano kati ya China na nchi za Afrika.

Idhaa ya kiswahili 06-06-09