Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-09 14:52:09    
Waandishi wa habari kutoka nchi za Afrika waionavyo China

cri

Mwezi Machi mwaka huu, wizara ya mambo ya nje ya China iliandaa semina ya habari kwa nchi za Afrika, ambapo waandishi habari wa ngazi ya juu na maofisa wa habari watapao 41 kutoka nchi 23 za Afrika walishiriki kwenye semina hiyo. Licha ya kupewa mafunzo ya darasani, waandishi hao wa habari pia walitembelea Hefei, mji mkuu wa mkoa wa Anhui kusini mwa China, na mji wa Qingdao, mji wa pwani ya mashariki. Waandishi wa habari wa Afrika walisema mambo ya China waliyoshuhudia ni tofauti sana na waliyosikia kupitia vyombo vya habari vya nchi za magharibi.

Tarehe 18 mwezi March ilikuwa siku ya kuzaliwa kwa Bi. Mchuka, ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa taasisi ya utangazaji ya Tanzania. Siku hiyo aliporudi chumbani baada ya kumaliza shughuli za mchana, aliona fungu moja la maua mazuri. Muda mfupi baadaye, aliletewa keki kubwa, ofisa husika wa semina hiyo pamoja na washirika wengine wa semina hiyo walisherehekea siku ya kuzaliwa kwake. Jambo hilo lilimpa mshangao mkubwa na kumfurahisha sana. Alisema, wachina ni watu wazuri sana, na China ni nchi anayopenda kuishi daima.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bi. Mchuka kutembelea China, kabla ya hapo aliwahi kuifahamu China kwa kutazama vipindi vya televisheni vya kituo cha televisheni cha China CCTV vinavyorushwa nchini Tanzania. Katika muda wake nchini China, Bi. Mchuka aliendelea kuandika kumbukumbu kwenye shajara yake kila siku. Alisema baada ya kurudi nchini Tanzania ataandika makala kwenye magazeti na kutengeneza vipindi maalum vya radio ili kuwafahamisha wasomaji na wasikilizaji wa Tanzania kuhusu vivutio vya utalii na mambo yanayotokea nchini China.

Bi. Mchuka alisema ujenzi wa vijiji vya China umempa picha nzuri sana. Alitembelea kijiji kimoja cha mkoa wa Anhui na kuishi kwa usiku mmoja huko. Alishuhudia kwa macho yake mwenyewe jinsi wanakijiji wa China wanavyoishi maisha mazuri. Alisema maisha mazuri ya wanavijiji wa China si kama tu yanatokana na sera bora na utawala mzuri wa serikali ya China, bali pia yanatokana na juhudi walizofanya wakulima wa China.

Bw. Marx Hamata ni naibu mhariri wa gazeti la Times la Namibia. Akiwa mwandishi wa habari amewahi kutembelea nchi na sehemu nyingi, pia amewahi kusoma nchini Uingereza na Ujerumani. Safari hii alipata nafasi ya kukutana na watu wa kawaida wa China. Alisema baada ya kurudi nchini Namibia atawaambia wasomaji wake kwamba, China ni nchi yenye maendeleo, na ni mfano unaostahiki kuigwa.

Bw. Hamata alisema, watu wa Afrika wameathiriwa sana na vyombo vya habari vya nchi za magharibi, ambavyo vinaonesha kuwa China ni nchi isiyofuatana na mkondo wa dunia, nchi inayokwenda kinyume cha utaratibu wa shirika la biashara duniani na nchi isiyoheshimu sheria. Lakini mambo waliyoshuhudia yameonesha kuwa, China imefanya juhudi kubwa katika kuhimiza maendeleo. Kwa nchi nyingi, maendeleo yanamaanisha majengo marefu, lakini kwa China maana ya maendeleo ni kupunguza umaskini na kuanzisha mfumo mzuri wa utoaji huduma za jamii.

Namibia ilipata uhuru mwaka 1990, lakini Bw. Hamata alisema, uhusiano wa kirafiki kati ya China na Namibia ulianza mapema zaidi. Katika miaka zaidi ya 50 iliyopita, China ilijitahidi kuunga mkono harakati za ukombozi wa watu wa Afrika, na kutoa msaada mkubwa usiokuwa na masharti.

Waandishi wa habari wa nchi za Afrika wanatarajia kuimarisha ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika katika sekta mbalimbali kama vile ujenzi wa miundo mbinu, utengenezaji wa madawa, miradi ya maji na vifaa vya kilimo.

Naibu mhariri mtendaji wa gazeti la Daily Nation toleo la Jumapili wa Kenya Bwana John Kakudu Aganda alisema, serikali ya China ina mtizamo mzuri kuhusu ujenzi wa nchi yake, imejenga miradi mingi mikubwa kama vile miradi ya reli, utoaji maji na umeme, na uzoefu wa China wa kujenga nchi unastahili kuigwa kwa nchi za Afrika.

Bw. Aganda alisema mtindo wa China wa kujenga vijiji, miji midogo na nyumba za kuwahudumia wazee ni mzuri. Malaria ni ugonjwa unaowasumbua sana watu wa Afrika, kila mwaka watu wengi wa Kenya wanakufa kutokana na ugonjwa huo, China ina dawa nyingi nzuri za kutibu ugonjwa wa malaria, hivyo ushirikiano kati ya China na Kenya katika sekta hiyo utaokoa maisha ya watu wengi wa Kenya.

Aliongeza kuwa kuanzia mwezi Machi hadi mwezi Mei, Kenya inakuwa inapata mvua nyingi, lakini wakazi wengi wa nchi hiyo wanakumbwa na upungufu wa maji ya kunywa kutokana na kukosa zana na ujuzi wa kukusanya na kuhifadhi maji, hivyo uzoefu wa China wa ujenzi wa miradi ya maji unastahiki kuingwa na Kenya na nchi nyingine za Afrika.

Baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza magari cha China, Bw. Aganda alisema, mitambo midogo ya kilimo na malori madogo yanayotenegnezwa nchini China yanafaa sana kwa wakulima wa Kenya, pia yana bei nafuu, hivyo alitumai kuwa makampuni ya China yanayotengeneza mitambo hiyo yataanzisha viwanda katika sehemu ya Afrika mashariki ili kukidhi matakwa ya wakulima wa huko.

Tanzania ni nchi ya kilimo Bi. Mchuka alisema, Tanzania ina mashamba mengi ya kilimo na nguvu kazi ya kutosha, lakini haina utaalamu wa kutosha wa kilimo. Hivyo kilimo ni sekta nzuri zaidi ya ushirikiano kati ya China na Tanzania, China inaweza kuwafundisha wakulima wa Tanzania namna ya kulima mashamba au kuanzisha miradi ya kilimo wao wenyewe.

Idhaa ya kiswahili 06-06-09