Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-12 16:15:39    
"Siku ya India" yafanyika katika Chuo Kikuu cha Beijing

cri

Katika siku za karibuni Chuo Kikuu cha Beijing kilikuwa na shamrashamra za utamaduni wa India kutokana na siku ya India kufanyika huko.

Siku ya India ni moja ya shughuli za "Mwaka wa Urafiki kati ya China na India 2006" nchini China, ambayo inaandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Elimu kuhusu India katika Chuo Kikuu cha Beijing na Ubalozi wa India nchini China.

Chuo Kikuu cha Beijing ni kituo cha kutafiti na kufundisha elimu kuhusu India nchini China. Mapema mwanzoni mwa karne iliyopita, chuo kikuu hicho kilianzisha utafiti wa falsafa, fasihi na isimu ya lugha ya Kihindi. Mwaka 1946 chuo kikuu hicho kilianzisha idara ya lugha na fasihi za Mashariki, na kutokana na juhudi za wataalamu wa elimu ya India Ji Xianlin na Jin Kemu, utafiti na elimu vimepata maendeleo makubwa. Mwaka 2004 kituo cha utafiti wa elimu kuhusu India kilianzishwa, waziri mkuu wa India Bw. Vajpayee aliyekuwa ziarani nchini China alizindua kituo hicho. Mwezi Aprili mwaka jana, waziri mkuu wa China Wen Jiabao aliitembelea India, China na India zilitangaza kuanzisha ushirkiano wa kiwenzi kwa ajili ya kudumisha amani na ustawi, mawaziri wakuu wa nchi hizo mbili waliamua mwaka 2006 uwe "Mwaka wa Urafiki wa China na India".

Shughuli za Siku ya India zimefanyika kwa siku kumi kuanzia tarehe 22 Mei, shughuli zake zikiwa ni pamoja na mihadhara, maonesho ya picha, tamasha la wanafunzi wa China na India na kongamano lenye mada za "Uchumi wa India na Biashara kati ya China na India" na "Uhusiano wa China na India na Sera za Kidiplomasia za India", na maonesho ya filamu za India zinazowavutia sana Wachina.

Kwenye ufunguzi wa Siku ya India picha zaidi ya mia moja zilizotolewa na Ubalozi wa India nchini China zilioneshwa. Picha hizo zilionesha mila na desturi za watu wa India kutoka pande mbalimbali. Mwanafunzi Cai Yulin alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema, " Siku ya India inatusaidia sana kuifahamu nchi hiyo. China na India ni majirani na zote ni nchi kubwa zinazoendelea, maingiliano ya utamaduni kama hayo yafaa kufanyika mara kwa mara."

Profesa Jian Jingkui wa Kituo cha Utafiti wa Elimu kuhusu India katika chuo kikuu hicho ambaye ni mmoja wa waandaaji wa shughuli za Siku ya India alisema, maingiliano kati ya serikali na wataalamu ni muhimu, lakini maingiliano kati ya raia wa nchi mbili na hasa vijana, pia ni muhimu sana. Alisema, "Uhusiano kati ya nchi mbili utakavyokuwa katika siku za usoni unategemea vijana, tunapowapa vijana wetu fursa ya kufahamu India pia tumeipatia India fursa ya kujionesha. Wanafunzi wa chuo kikuu cha Beijing wanafahamu sana kwamba nchi hizo mbili zikishirikiana vizuri, zitakuwa na ustawi mkuwa."

China na India ni nchi za kale zenye ustaarabu mkubwa, kumbukumbu ya mawasiliano kati ya nchi hizo mbili ilianzia miaka 2000 iliyopita. Karne ya pili kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, wafanyabiashara wa Enzi ya Han ya China walifungua "njia ya hariri" ya kufikia Magharibi, na India ilikuwa nchi muhimu katika njia hiyo, na bidhaa za China zilifikishwa hadi Ulaya kupitia India. Katika karne ya kwanza kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, dini ya Buddha iliingia nchini China na imekuwa sehemu ya utamaduni wa China. Balozi wa India nchini China Bw. Nalin Surie alisifu sana maingiliano ya utamaduni kati ya China na India. Alisema, baada ya karne ya 21 kuanza, nchi mbili kubwa zinazoendelea, China na India, zina fursa nzuri ya kihistoria ya kustawisha ushirikiano. Kwenye ufunguzi wa Siku ya India balozi huyo alisema, "Ni kama India, kwamba China pia ni nchi yenye utamaduni mkubwa wa jadi, na tamaduni za nchi hizo mbili zinafanana katika mambo mengi. Kwa kuwa majirani, nchi hizo mbili zinaweza kusaidiana katika utamaduni, elimu, afya na uchumi, na uzoefu wa nchi moja ni muhimu kwa nchi nyingine."

Balozi huyo pia alisema, maendeleo ya haraka ya uchumi wa China yanamvutia sana. China inapoendeleza uchumi pia inatilia mkazo kustawisha utamduni wake na kuupokea utamaduni kutoka nchi za nje ukiwa ni pamoja na utamaduni wa India. Shughuli za Siku ya India zinasaidia vijana wa China kufahamu India na kuimarisha maingiliano ya kiraia kati ya China na India.

Imefahamika kwamba katika mwaka huu wa urafiki wa China na India, nchi hizo mbili zimesaini miradi ya maingiliano zaidi ya 50 ikiwa ni pamoja na sekta ya siasa, biashara, utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia, na kati ya maingiliano hayo, maingiliano ya utamaduni ni makubwa zaidi yakiwa ni pamoja na kupanga tamasha la filamu, opera ya Kibeijing kuoneshwa nchini India, na kundi la nyimbo na ngoma la India kuonesha michezo yao nchini China.