Mkutano mkuu wa 90 wa shirika la kazi duniani uliofanyika mwezi Juni mwaka 2002, uliamua kuwa tarehe 12 Juni ya kila mwaka iwe siku ya kukomesha ajira ya watoto duniani. Tarehe 12 Juni mwaka huu ni mwaka wa tano wa siku ya kukomesha ajira ya watoto duniani. Kauli-mbiu ya siku ya maadhimisho ya mwaka huu ni "Tushirikiane kukomesha ajira ya watoto". Kutokana na kufanyika kwa mashindano ya soka ya kombe la dunia, ili kuvutia ufuatiliaji wa vyombo vya habari, shirika la kazi duniani litafanya shughuli mbalimbali katika nchi zaidi ya 100 kwa ushirikiano na mashirikisho ya soka katika nchi zaidi ya 100 katika kipindi cha michezo ya soka, na kuanzisha harakati kubwa ya kupiga marufuku ajira ya watoto.
Takwimu za shirika la kazi duniani zinaonesha kuwa, hivi sasa duniani kuna watoto kiasi cha milioni 317 wenye umri wa kati ya miaka 5 na miaka 17, ambao wameajiriwa katika aina mbalimbali za shughuli za kiuchumi, na milioni 218 kati yao ni wafanyakazi watoto ikiwa ni sehemu moja ya sita ya jumla ya idadi ya watoto duniani. Wafanyakazi watoto milioni 126 kati yao, wanafanya kazi zenye athari mbaya kwa ukuaji wao kisaikolojia, afya na hisia, na watoto wengi kati yao wanafanya kazi mbaya kabisa, zikiwemo uuzaji wa dawa za kulevya, kushiriki kwenye vita, ukahaba au kufanya kazi zenye hatari kwenye migodi midogo. Idadi ya wafanyakazi watoto wa bara la Asia inachukua nafasi ya kwanza kuliko ya mabara mengine, wakati kiasi cha wafanyakazi watoto ni kikubwa kwenye sehemu ya kusini mwa Sahara ikilinganishwa na idadi ya watu wa sehemu hiyo.
Hali ya kuwepo kwa ajira ya watoto inatokana na mazingira ya jamii kuwa mabaya, vita na umaskini. Vita ya miaka mingi pamoja na magonjwa vimeua watu wengi, ambapo watoto wengi wamepoteza wazazi wao. Takwimu zinaonesha kuwa, tokea mwaka 1990, kwa uchache kabisa ugonjwa wa Ukimwi umefanya watoto milioni 14 wenye umri chini ya miaka 15 kupoteza wazazi wao, na kulazimika kuajiriwa. Na umaskini umewalazimisha watoto wengi kubeba mizigo ya maisha ya familia zao mapema zaidi.
Tokea miaka mingi iliyopita, jumuiya ya kimataifa ilijitahidi kutafuta utatuzi wa suala hilo, na katika miaka ya karibuni imepata mafanikio ya mwanzo. Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na shirika la kazi duniani inaonesha kuwa idadi ya wafanyakazi watoto imepungua kwa 11% kutoka mwaka 2000 hadi mwaka 2004. Taarifa hiyo inasema, Brazil na China zimeonesha mfano bora katika upande huo. Katika miaka 25 iliyopita, idadi ya watu walioondokana na umaskini na idadi ya watoto waliokwenda shule kwenye nchi hizo mbili ni kubwa zaidi kuliko nchi yoyote nyingine. Ingawa idadi ya watoto wenye umri wa kwenda shule ni kubwa zaidi, na 80% ya watoto hao wako katika sehemu za vijijini, lakini China imefaulu kufanya karibu watu wote wapate elimu ya msingi. Moja ya hatua muhimu iliyochukuliwa na China ni kupiga marufuku kuajiri watoto ambao hawajamaliza elimu ya lazima ya miaka 9. Kanuni hiyo ni ya kipekee miongoni mwa nchi zinazoendelea. Takwimu kutoka idara husika zinaonesha kuwa, idadi ya watoto wenye umri wa miaka kutoka 10 hadi 14, wanaotumikishwa imepungua hadi 12% mwaka 1995 kutoka 48% katika mwaka 1950, tena idadi hiyo inaendelea kupungua. Idadi ya watoto wenye umri kati ya miaka kutoka 5 hadi 9 imepungua kwa 60.9% kutoka mwaka 1992 hadi mwaka 2004, wakati idadi ya wafanyakazi watoto wenye umri wa miaka kutoka 10 hadi 17 imepungua kwa 36.4% nchini Brazil.
Shirika la kazi duniani linaona kuwa ufuatiliaji na uungaji mkono wa serikali ni kitu muhimu sana kwa maendeleo ya harakati za kukomesha wafanyakazi watoto, ambapo elimu ya lazima ni mbinu yenye ufanisi mkubwa zaidi.
Mkurugenzi wa shirika la kazi duniani kabla ya kuwadia kwa siku ya kupiga marufuku ajira ya watoto duniani alisema, uzoefu wa duniani katika miaka mingi iliyopita umethibitisha kuwa, siyo kwamba ajira ya watoto haiwezi kukomeshwa, kitu tunachotakiwa kuonesha katika kupiga marufuku ajira ya watoto ni azma ya binadamu, yaani kila mtoto anastahili kupata haki ya mtoto toka anapozaliwa.
|