Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-13 19:34:30    
Serikali ya Bush yalaumiwa kutokana na tukio la kufa kwa wafungwa

cri

Tukio la kufa kwa wafungwa lililotokea tarehe 10 kwenye gereza la Guantanamo ni tukio la kwanza la kufa kwa wafungwa tangu lijengwe gereza hilo la jeshi la Marekani, ambalo linafuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Hivi karibuni wizara ya ulinzi ya Marekani ilitangaza majina ya wafungwa hao watatu na kusema, wafungwa hao walifariki kwa kujiua. Lakini jamaa za marehemu hao walieleza mashaka yao kuhusu chanzo cha vifo vyao. Kwa upande mwingine, tukio la kufa kwa wafungwa limefanya serikali ya Bush ikabiliwe na shinikizo kubwa.

Wizara ya ulinzi ya Marekani tarehe 11 ilitangaza kuwa, wafungwa wawili kati ya hao watatu waliojiua ni Mani bin Shaman bin Turki al-Habardi na Yasser Talal Abdulah yahya al-Zahrani wa Saudi Arabia, na mwingine ni Ali Abdullah Ahmed wa Yemen, ambao walijinyonga kwa nguo na mashuka ya chumba cha gerezani. Hapo awali, Mani bin Shaman wa Saudi Arabia alifikiriwa kupelekwa katika nchi nyingine baada ya kuthibitishwa kutokuwa na hatia kubwa. Msaudi Arabia mwingine Yasser Talal Abdulah yahya al-Zahrani alitajwa kuwa ni mwanachama muhimu wa kundi la Taliban, na Myemen Ali Abdullah Ahmed ni mwanachama wa ngazi ya juu wa kundi la Al Qaeda.

Jamaa wa marehemu hao walieleza mashaka yao kuhusu vifo vya wafungwa hao. Hivi karibuni jamaa za wafungwa wawili wa Saudi Arabia walisema, jamaa zao walikuwa waislamu kamili, dini ya kiislamu inakataza watu kujiua, hivyo wasingeweza kujiua, bali ni kwamba huenda waliuawa na wengine. Upande wa Marekani haujasema chochote kuhusu mashaka ya jamaa za wafungwa hao waliokufa, na rais Bush alisema anafuatilia sana tukio hilo. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia ilisema inawasiliana na serikali za Saudi Arabia na Yemen.

Kutokea kwa tukio la kufa kwa wafungwa, kunafanya serikali ya Bush ikabiliwe na shinikizo zaidi kutoka nchini na nchi za nje, watu wanataka serikali ya Bush ifunge gereza la Guantanamo.

Mbunge wa taifa anayeheshimiwa sana wa chama cha demokrasia cha Marekani Bw. Jack Reed amekosoa vikali vitendo vya serikali ya Marekani kuhusu suala la Guantanamo. Alisema, "serikali inatakiwa kulifunga haraka gereza la Guantanamo, na inatakiwa kuwa na mchakato wa kuleta ulingano kati ya lengo la kuwatenganisha na umma na lengo la kufahamu nani ni magaidi wa kweli, lakini hadi hivi sasa serikali bado haijapata mafanikio. Mwenyekiti wa kamati ya sheria ya bunge la taifa la Marekani Bw. Arlen Specter pia alitoa malalamiko kuhusu serikali ambayo inawafunga watuhumiwa kwa muda mrefu na kutochukua hatua za kisheria. Alisema watu wengi walifungwa kutokana na tetesi, endapo wafungwa hao ni magaidi, basi wangefunguliwa mashitaka, wala siyo kufungwa bila kikomo. Jumuiya ya kimataifa nayo inataka serikali ya Marekani ifunge gereza la Guantanamo. Kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya uliofanyika tarehe 12, maofisa washiriki wa mkutano waliokosoa tukio la kufa kwa wafungwa, na kutaka serikali ya Marekani ifunge gereza hilo. Mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya nje na ujirani bibi Benita Ferrero-Waldner alisema, tukio hilo limethibitisha tena kuwa gereza la Guantanamo linakiuka sheria za kimataifa, hivyo linatakiwa kufungwa. Kamati ya chama cha msalaba mwekundu duniani siku hiyo ilieleza wasiwasi wake kuhusu hali ya wafungwa walioko katika gereza la Guantanamo, na kutangaza kuwa itapeleka kikundi kimoja huko ndani ya wiki hii.

Hivyo tusijali kama wafungwa hao walikufa kutokana na sababu gani, lakini kuwepo kwa gereza la Guantanamo na vifo vya wafungwa hao watatu, vimefanya serikali ya Bush ambayo inajisifu kuwa ni mlinzi wa haki za binadamu, kushitakiwa kwenye "mahakama ya utu" na kukabiliwa na mashinikizo ya kutoka ndani na nje ya Marekani.