Jengo jipya la Bunge, ambalo lina vifaa vya kisasa kabisa ili kurahisisha mawasiliano kwa wabunge na watendaji wengine, ambalo limeuongezea mji wa Dodoma, Tanzania mandhari nzuri ya kuvutia, limezinduliwa rasmi tarehe 13 Mei na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania.
Jengo hilo litakalogharimu zaidi ya Shilingi. bilioni 30.9 za Tanzania hadi likakapokamilika kabisa, limeelezwa kuwa ni la kwanza kwa ukubwa na ubora ikilinganishwa na majengo mengine ya Mabunge ya nchi za Afrika Mashariki. Ni jengo lenye mvuto kwa nje na ndani na limejaa kila aina ya teknolojia ya kisasa kwa lengo la kurahisisha na kukidhi utendaji kazi wa Spika, wabunge wote kwa ujumla na waandishi wa habari.
Meneja Usimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa jengo hilo, Bw. Karim Mataka, alisema mbali ya jengo hilo kuwa kubwa na bora katika Afrika Mashariki, pia ni la tatu kwa ukubwa na ubora katika Bara la Afrika kwa sasa.
Jengo hilo ambalo lipo upande wa Mashariki mwa mji wa Dodoma, kando ya Barabara Kuu itokayo Morogoro, lina milango mikubwa mitatu ya kuingilia na kutokea kwa Mawaziri, Wabunge na wafanyakazi na kwamba limefungwa mitambo mikubwa mitatu ya kupooza hewa. Kadhalika, lina jenereta mbili kubwa zenye uwezo wa kuzalisha kati ya kilovoti 500 na 800za umeme, mfumo wa mawasiliano ya Bunge, mtambo wa kuchukua picha na sauti wakati majadiliano yakiendelea ndani ya ukumbi na mfumo wa kisasa wa ulinzi na usalama.
Katika lango kuu la kuingilia na kutokea Mawaziri na Wabunge, kumewekwa mitambo maalum ya kukagua silaha na vitu vyovyote vile vya hatari na mbele yake kidogo, kuna lango la kuzuia magari iwapo yatabainika kubeba vitu vinavyoweza kuleta madhara kwa Mawaziri, Wabunge na watu wote wanaotumia jengo hilo.
Kila mlango wa kuingilia katika viwanja vya Bunge, kuna eneo la kuegesha magari hali itakayosaidia usalama wake tofauti na ilivyokuwa katika jengo la zamani. Katika eneo la viwanja vya Bunge, kuna bustani za maua na miti yenye rangi ya kijani inayovutia ambayo imepandwa ili kuweka mandhari nzuri za eneo hilo huku viunga hivyo vya Bunge vikiwa na maporomoko ya maji.
Wakati wa usiku, mandhari ya viunga vya Bunge vinavutia zaidi, hasa kutokana na kuzungukwa na taa nyingi za rangi na aina mbalimbali. Kwenye lango la kuingilia viongozi ndani ya ukumbi wa mikutano, kumewekwa mtambo maalum ambapo ili kuweza kuingia, unapaswa kutumia kadi maalum.
Milango hiyo yote itakuwa na askari na watu wa usalama ambao kazi yao ni kuhakikisha kuwa hakuna kitu cha hatari kitakachoingizwa ndani ya ukumbi huo. Katika eneo hilo kila kundi wa watu yaani wabunge, wananchi na wafanyakazi wa bunge watakuwa na milango yao ya kuingilia na kwenda kukaa kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao'' alisema.
Kadhalika ndani ya ukumbi wa jengo hilo, kuna kifaa maalumu kimewekwa ambacho kazi yake ni kukata minara ya simu ili kuwawezesha wote watakaokuwa ndani ya ukumbi huo kutoweza kupiga simu wala kupokea simu. Ukumbi huo pia una eneo la mita za mraba 1,200 ambalo ni ghorofa moja kwenda chini, eneo hilo litakuwa ni kwa ajili ya wabunge, viongozi mbalimbali na wananchi kupumzika na kubadilishana maoni wakati wa mapumziko. Eneo hilo la chini pia limetengwa katika sehemu kuu mbili, yaani sehemu ya wabunge na viongozi wa serikali na wananchi ambao wametenganishwa na mageti mawili, eneo hilo pia limewekwa vitu vya tamaduni toka makabila mbalimbali ya hapa nchini.
Sanaa za kiutamaduni zilizopo ni pamoja na vigoda vilivyochongwa tangu mwaka 1945, kuna ngoma zilizotengenezwa kwa ngozi, vyanuo, vibuyu vya kimasai, malimba na sanamu mbalimbali. Pia kutakuwa na skrini kubwa mbili na spika kwa ajili ya kutazama na kusikiliza vikao zinavyoendeshwa huko ndani. Katika eneo lote la viwanja vya bunge kumefungwa kamera ambazo zitakuwa zinarekodi kila kitu kitakachokuwa kinaendeshwa kuanzia nje hadi ndani ya ukumbi.
|