Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-13 19:42:16    
Hali ya upungufu wa umeme wa miaka minne mfululizo itabadilika nchini China

cri

Naibu mkurugenzi wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa ya China Bwana Zhang Guobao tarehe 8 hapa Beijing amesema, kutokana na ongezeko la haraka la utoaji wa umeme wa mashine mpya za uzalishaji wa umeme kote nchini, pamoja na utekelezaji wa marekebisho na udhibiti wa uchumi wa taifa, na usimamizi wa ugavi wa umeme unaofanyika kwa kina siku hadi siku, upungufu wa umeme utapungua zaidi nchini China, katika majira ya siku za joto ya mwaka huu haitatokea tena hali ya kukatika kwa umeme.

Katika miaka ya hivi karibuni, kadiri uchumi wa China unavyoendelea kwa haraka na kwa miaka mfululizo, ndivyo mahitaji ya nishati hasa umeme yanavyoongezeka siku hadi siku. Tokea mwaka 2002, upungufu wa umeme ulitokea nchini China, tena upungufu huo ulizidi kuwa mkubwa siku hadi siku. Hasa wakati wa majira ya siku za joto, matumizi ya umeme huwa ni makubwa, ambapo sehemu kadha wa kadha hutokea hali ya kukatika kwa umeme, na viwanda kadhaa vilisimamisha uzalishaji wa bidhaa ili kukwepa wakati wa kilele cha matumizi ya umeme; na maisha ya wakazi wa sehemu hizo pia yameathiriwa kwa kiasi fulani. Hali hiyo ilileta athari mbaya kwa maendeleo ya uchumi na jamii. Lakini mwaka huu hali ya kukatika kwa umeme haitatokea tena katika siku za joto mwaka huu. Bwana Zhang Baoguo alisema:

kutokana na kukamilishwa kwa ujenzi wa viwanda kadhaa vya uzalishaji wa umeme kabla ya majira ya siku za joto, hali ya utoaji na mahitaji ya umeme katika nusu ya pili ya mwaka huu itakuwa ya uwiano kwa ujumla, hali hii itafungua ukurasa mpya katika historia ya maendeleo ya umeme nchini China.

Bwana Zhang amefafanua kuwa, tokea mwezi Juni mwaka 2002 hadi hivi sasa, wastani wa ongezeko la umeme nchini China siku zote ulikuwa zaidi ya asilimia 10, hili ni ongezeko kubwa kuliko lile la thamani ya uzalishaji mali. Kwa eneo la nchi nzima, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu hali ya kukatika umeme bado ilitokea kwa muda mfupi katika sehemu kadhaa katika mikoa kadhaa. Kabla ya kuwadia kwa majira ya siku za joto ambapo matumizi ya umeme yanafikia kileleni, mashine nyingi za uzalishaji umeme zitaanza kazi kote nchini, hivyo katika nusu ya pili ya mwaka huu hali ya kukatika kwa umeme haitatokea kimsingi. Amesema ili kuhakikisha mahitaji ya matumizi ya umeme ya sehemu iliyoendelea kiuchumi ya mashariki ya China, serikali kuu imetoa ugavi mwingine wa umeme kusaidia mkoa wa Guangdong na sehemu nyingine zenye upungufu wa umeme.

Katika miaka ya hivi karibuni, mbali na kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu ya uzalishaji wa umeme, China pia imeharakisha marekebisho ya miundo ya nguvu ya umeme. Bwana Zhang amesema, katika miaka kadhaa iliyopita, sehemu mbalimbali nchini China zilikuwa na juhudi kubwa za kujenga vituo vya kuzalisha umeme kwa nishati ya makaa ya mawe, sehemu kadhaa hata zilikiuka kanuni na kujenga vituo vidogo vya kuzalisha umeme kwa nishati kubwa ya makaa ya mawe na kutoa uchafuzi mkubwa kwa mazingira. Kutokana na utekelezaji wa hatua za marekebisho na udhibiti za serikali, hivi sasa ujenzi wa vituo kama hivyo umesimamishwa.

Siku chache zilizopita serikali ya China imepitisha mpango wa 11 wa maendeleo ya miaka mitano ijayo, mpango huo umeweka lengo kuwa, ifikapo mwaka 2010, matumizi ya nishati yatapungua kwa asilimia 20 kuliko yale ya mwaka 2005. Bwana Zhang akisema, ifikapo mwaka 2010, uwezo wa mashine za uzalishaji umeme kote nchini China utafikia kilowati milioni 800, ambapo sehemu ya magharibi ya China itapanua zaidi kazi ya kupeleka umeme kwenye sehemu ya mashariki ya China, na miundo ya umeme itaboreshwa zaidi, China itajitahidi kuufanya umeme utakaozalishwa kwa nguvu ya maji, nyuklia, gesi na makaa ya mawe yasiyotoa uchafuzi pamoja na nishati ya aina mpya uzidi asilimia 35 ya ule wa jumla.