Tarehe 14 mwezi Juni mwaka huu ni "siku ya kutoa damu kwa kujitolea duniani". Kauli mbiu ya mwaka huu ni "ahadi": Watu wenye afya nzuri waahidi kutoa damu kwa kujitolea mara kwa mara, watu wanaotoa damu kwa kujitolea hivi sasa, waahidi kuendelea kutoa damu mara kwa mara; vitengo vya huduma ya kuwapa damu wagonjwa pamoja na asasi nyingine husika ziahidi kufuata vigezo vya juu kabisa vya tiba katika kila hatua ya mchakato ya kuwapa damu wagonjwa.
Ili kuhimiza watu wengi zaidi watoe damu kwa kujitolea, na kutoa habari na kuhimiza utekelezaji wa mpango wa usalama wa damu duniani, shirika la afya duniani, chama cha msalaba mwekundu, chama cha hilali nyekundu, shirikisho la vyama vya kutoa damu kwa kujitolea duniani na jumuiya ya kuwapa wagonjwa damu duniani, viliamua kuwa tarehe 14 mwezi Juni ya kila mwaka iwe "siku ya kutoa damu kwa kujitolea duniani" tokea mwaka 2004. Lengo lake ni kumkumbuka bingwa wa elimu ya magonjwa ya kurithi wa Austria Bw. Karl Landsteiner, ambaye alikuwa wa kwanza kugundua kuweko aina tofauti za damu kwa binadamu, na kuwa maisha ya mgonjwa yataweza kuokolewa kwa kuongezewa damu ya aina yake, hivyo siku ya kuzaliwa kwa bingwa huyo imethibitishwa kuwa ni "siku ya kutoa damu kwa kujitolea duniani".
Kabla mwaka wa tatu wa "siku ya kutoa damu kwa kujitolea duniani" haujawadia, shirika la afya duniani lilitoa taarifa huko Geneva ikieleza hali kuhusu kutoa damu na matumizi ya damu duniani. Taarifa hiyo inasema hivi sasa katika nchi nyingi duniani, siyo damu zote zinazotumika katika tiba ya wagonjwa, zilitolewa na watu kwa kujitolea, hivyo usalama wa damu wanazopewa wagonjwa hauwezi kuhakikishwa. Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni kwenye nchi 124 unaonesha, ni katika nchi 56 tu ambazo idadi ya watu waliotoa damu kwa kujitolea iliongezeka kidogo katika miaka 2 iliyopita, wakati nchi nyingine 68, idadi hiyo ilikuwa karibu sawa na miaka ya nyuma, au ilipungua katika nchi chache miongoni mwa nchi hizo. Aidha, kutokana na upungufu wa fedha, zana za upimaji na watu wenye ujuzi maalumu, kuna nchi 56 ambazo hazifanyi upimaji kuhusu virusi vya maambukizi vya Ukimwi, ugonjwa wa maini na kaswende vilivyoko katika damu zilizotolewa na watu.
Katika nchi 124 zilizofanyiwa uchunguzi, nchi 49 kati yake zikiwemo nchi 17 zinazoendelea, zimefikia hatua ambayo damu zote wanazopewa wagonjwa katika hospitali, zilitolewa na watu kwa kujitolea. Kiasi cha watu wanaotoa damu kwa kujitolea wa nchi zilizoendelea ni mara 15 kuliko nchi zinazoendelea. Lakini mahitaji ya damu katika nchi zinazoendelea ni makubwa zaidi yakiwa ni pamoja na watoto wenye upungufu wa damu kutokana na ugonjwa wa malaria na akina mama kutokwa damu wakati wa kujifungua. Endapo kuna damu ya kutosha, idadi ya vifo vya waja wazito wanaojifungua itapungua kwa 25%.
Shirika la afya duniani lilisema, katika miaka 2 iliyopita, China, Malaysia, India na Saint Lucia zimepiga hatua kubwa kwenye maendeleo katika kutoa damu kwa kujitolea na usalama wa matumizi ya damu. Toka mwaka 1998 hadi mwaka 2005, kiasi cha damu walizopewa wagonjwa katika hospitali kutokana na damu zilizotolewa na watu waliojitolea kiliongezeka na kufikia 94.5% kutoka 22%. Mwaka jana China ilifanya upimaji kuhusu virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, maini na kaswende vilivyoko katika damu zilizotolewa na watu. Shirika la afya duniani linaona, maendeleo hayo iliyopata China hususan yalitokana na udhibiti wa biashara ya damu, na kuzuia kwa nguvu utoaji damu kwa njia zisizo halali.
Mwaka huu mkutano mkuu wa maadhimisho ya "siku ya kutoa damu kwa kujitolea duniani" utafanyika katika Bangkok, Thailand. Tarehe 14 mwezi Juni, kituo cha mafunzo ya utoaji damu cha shirika la afya duniani na kituo cha damu cha chama cha msalaba mwekundu cha Thailand vitafanya shughuli kubwa za maadhimisho mjini Bangkok, ambazo wawakilishi wa nchi zaidi ya 100 duniani watashiriki.
Idhaa ya Kiswahili 2006-06-14
|