Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-14 20:16:07    
Wanafunzi milioni 9.5 washiriki kwenye mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu nchini China

cri

  

    Wanafunzi milioni 9.5 walishiriki kwenye mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu iliyofanyika kuanzia tarehe 7 hadi 9 Juni nchini China, ili kuwania nafasi milioni 5.3 zinazotolewa na vyuo vikuu mbalimbali. Katika siku ya kwanza ya mitihani hiyo, mwandishi wetu wa habari alikwenda kwenye kituo cha mitihani kilichoko kwenye mtaa wa Shijingshan hapa Beijing, ambapo aliona wanafunzi wengi wakiwa wamekusanyika. Baada ya wanafunzi kuingia kwenye darasa na kufanya mtihani, wazazi wao walikuwa wanawasubiri nje wakiwa na wasiwasi. Bibi Wang Jing anasema:

    "Hivi sasa wazazi na watoto wote wanazingatia sana mitihani hiyo. Watoto walikuwa wamefanya maandalizi kwa ajili ya mitihani hiyo kwa miaka 12 tangu waanze kusoma katika shule za msingi, na wana wasiwasi lakini pia wana matumaini makubwa juu ya mitihani hiyo."

    Mitihani hiyo ni njia muhimu kwa wanafunzi kupata nafasi ya kusoma kwenye vyuo vikuu nchini China, na unafuatiliwa sana na watu. Tangu mitihani ya kujiunga na chuo kikuu irejeshwe mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita baada kusimamishwa kwa miaka kadhaa, wanafunzi wengi zaidi wanaruhusiwa kujiunga na kusoma kwenye vyuo vikuu, na ongezeko hilo limefikia na kufikia asilimia 50 ya hivi sasa kutoka asilimia 5. Hata hivyo bado kuna wanafunzi wengi wasioweza kupata nafasi hiyo ya kujiunga na vyuo vikuu.

    Lakini kwa upande mwingine wanafunzi wanaoweza kujiunga na vyuo vikuu vilevile wanapaswa kufanya chaguo gumu kabla ya kujiunga na vyuo vikuu. Kutokana na utaratibu wa mitihani hiyo, wanafunzi wanaoshiriki kwenye mitihani hiyo wanapaswa kujaza fomu kuhusu vyuo vikuu watakavyotaka kusoma. Katika hatua hiyo, wanafunzi watachagua vyuo na kozi wanazopenda kutokana na matokeo yao ya mitihani. Wanafunzi na wazazi wao wanazingatia sana fursa hiyo ikiwa ni ya pekee itakayoathiri maisha yao katika siku za mbele. Wanafunzi wawili waliozungumza na mwandishi wetu wa habari kuhusu suala hilo wanasema:

    Mwanafunzi mmoja Zhou Ying alisema, anajiandaa kusoma kozi ya sheria kwa kuwa anaipenda kozi hiyo, na wazazi wake vilevile wanaona kuwa hii ni kozi nzuri kwa kutafuta ajira baada ya kuhitimu masomo yake chuoni. Mwanafunzi mwingine Yuan Xin alisema, anataka kusoma kozi ya ualimu kwa sababu anaipenda kozi hiyo, pia atapata siku nyingi za mapumziko baada ya kuhitimu na kuwa mwalimu.

    Hivi sasa wanafunzi wengi wanachagua kozi kutokana na wanavyopenda, lakini vitendo hivyo havikubaliwi na wazazi wao. Wazazi huwachagulia watoto wao kozi kutokana na fursa za kupata ajira. Kutokana na hali hiyo, kozi zinazodhaniwa kuwa zitakuwa na urahisi zaidi wa kupata ajira huchaguliwa na wanafunzi na wazazi wao.

 

    Lakini hali hiyo inaleta matatizo mbalimbali. Mtaalamu wa elimu wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Beijing Bi Zheng Xinrong anasema:

    "Ni bayana kuwa, ongezeko la wanafunzi kwenye vyuo vikuu limeleta shinikizo kwa wanafunzi kupata ajira katika miaka kadhaa iliyopita, hali ambayo iliwafanya wanafunzi na wazazi wao kuchagua kozi zenye nafasi nyingi zaidi za kupata ajira baadaye, lakini kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosomea kozi hizo, kuna uwezekano kuwa wengi kati yao hawatapata ajira yoyote katika miaka kadhaa ijayo."

    Bibi Zheng amesema si njia nzuri kwa wanafunzi kuchagua kozi watakazosoma kwa njia ya kujaza fomu kuhusu uchaguo la kozi tu, kwa sababu wanafunzi na wazazi wao hawafahamu vya kutosha hali ya kozi wanazozichagua na huamua bila ya kuwa na malengo yaliyo wazi. Bibi Zheng anapendekeza kuwa vyuo vikuu, jamii na idara zinazoshughulikia ajira zitoe uelekezaji kwa wanafunzi kuhusu kuchagua kozi, na kuwasaidia wafahamu mwelekeo wa mahitaji ya jamii. Pia amependekeza kwa vyuo vikuu kuandaa kozi kwa njia mwafaka, ili kulingana na mahitaji ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Bi Zheng anasema:

    "Hivi sasa inapaswa kuanzisha mawasiliano kati ya mashirika yanayotoa ajira na watu wanaohitaji ajira, ili kuanzisha utaratibu unaoweza kukabiliana na mabadiliko ya mahitaji ya jamii."

    Hivi sasa, vyuo vikuu kadhaa vimefanya marekebisho kuhusu uwekaji wa kozi, ambapo si kama tu vimeondoa kozi zisizoweza kulingana na mahitaji makubwa ya ajira, bali pia vinaweka mkazo katika kuwaandaa wataalamu wenye ujuzi wa sekta mbalimbali. Chuo Kikuu cha Umma cha China ni moja kati ya vyuo vikuu vikubwa nchini China, ambacho mwaka huu kitaandaa shahada ya pili kwa wanafunzi wanaosoma katika chuo kikuu cha lugha za kigeni. Naibu mkurugenzi wa Ofisi ya uandikishaji ya chuo hicho Bw. Wang Peng ameeleza kuwa, kitendo hicho kina lengo la kuwaandaa wataalamu wanaokidhi mahitaji ya jamii. Bw. Wang Peng anasema:

    "Wanafunzi wasiosoma lugha za kigeni watapata fursa nyingi zaidi kama wanawekewa msingi mzuri wa lugha za kigeni; hali kadhalika wanafunzi wa lugha za kigeni hawatakuwa na uwezo mkubwa wa ushindani kama wanachukua kozi moja tu?na watapata maendeleo makubwa katika jamii kama wataweza kutumia ujuzi waliopata vyuoni katika kazi halisi."

    Ili kufanya vyuo vikuu viweze kuandaa watu wanaolingana na mahitaji ya jamii, wataalamu kadhaa wa elimu pia wanavitaka vyuo vikuu vichukue njia yenye unyumbufu kuwaandikisha wanafunzi. Licha ya mitihani inayoandaliwa na taifa, bali pia vinaweza kuwaandikisha wanafunzi kwa njia zake vyenyewe. Imefahamika kuwa hivi sasa kuna vyuo vikuu zaidi ya 50 vinavyofanya uandikishaji kwa njia zake vyenyewe, lakini idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kwa njia hiyo haizidi asilimia 5 ya idadi ya jumla ya wanafunzi.

    Mtaalamu wa elimu wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Beijing Bibi Zheng Xinrong anasema:

    "Naona kuwa hiyo ni njia nzuri, na wanafunzi wanaweza kuonesha uwezo wao kwa njia nyingine mbalimbali. Aidha wanafunzi wana muda mwingi zaidi wa kupata uwezo mwingine, kwani elimu ya chuo kikuu ina lengo la kuandaa watu wenye uwezo kwenye sekta mbalimbali. "

Idhaa ya Kiswahili 2006-06-14