Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-14 20:20:58    
Mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na Bw. Silverse Anami wa Kenya

cri

Kwanza kabisa tuelezee kwa undani kidogo sheria za hapa Kenya zinazohusu hifadhi ya urithi wa utamaduni.

Kenya ina lengo la kuwahamasisha wakenya wote kulinda utamaduni wetu. Wakoloni walileta utamaduni tofauti, kama dini tofauti, lugha tofauti na mambo mengi tofauti, hivyo ni lazima kwa serikali kurudisha na kulinda vizuri utamaduni wetu wenyewe. Sheria ya Kenya inatambua kuwa watu wa makabila mbalimbali wa Kenya wanapaswa kuhifadhi utamaduni wao, hiyo ndiyo sababu ya serikali kuunda wizara ya utamaduni, vilevile serikali imeweka sheria ya kuwazuia watu wasitumie vibaya hakimiliki za wengine, kama wakitaka kutumia ni lazima walipe.

Tungependa kujua hivi sasa Wakenya wanachukuliaje umuhimu wa urithi wa utamaduni?

Kuna wakenya ambao hawafuatilii utamaduni wao, lakini wakenya wengi wanafuata mila zao, wanapenda mila zao na kujua kuhifadhi utamaduni wao. Na serikali ya Kenya imeweka sheria za kuwasaidia wakenya wote kuhifadhi utamaduni wao. Mwezi Januari mwaka huu viongozi wa nchi mbalimbali za Afrika ambazo ni nchi wanachama wa Umoja wa Afrika walikutana huko Khartoum, na kukubaliana kwamba kuendeleza mambo ya utamaduni kwa njia ya elimu, yaani mambo ya utamaduni yafundishwe mashuleni. Na hivi sasa Kenya ina rasimu ya sera za kiutamaduni, ambayo kama itapitishwa katika baraza la mawaziri itatuongoza wakenya tushirikiane katika kuhifadhi utamaduni wetu.

Kuwaamsha Wakenya ili wajue umuhimu wa hifadhi ya urithi wa utamaduni, ni afadhali kuanzia kwa watoto na vijana, yaani waelimishwe tangu utotoni ili wajue urithi wa utamaduni ni mali ya Kenya, Je serikali ya Kenya imefanya juhudi gani katika upande huo?

Wizara ya utamaduni imefanya mambo mengi ya kuwaelimisha watoto, sio watoto peke yao, bali tunawaelimisha wazazi wao, yaani watu wazima, wazazi wakijua, watoto pia watajua. Jambo la kwanza tunalofanya ni kuwaelimisha wazazi kuwa, ni jukumu lao kuhifadhi utamaduni wetu. Pili ni jukumu lao kuwaelimisha watoto wao utamaduni wetu. Wakipuuza utamaduni wetu, watakuwa kama watumwa, hawatakuwa na msimamo, yaani utambulisho wa taifa letu utakuwa haupo. Aidha, kila baada ya muda fulani tunafanya matamasha ya utamaduni katika kila mkoa, ambapo watu wa makabila fulani wanakuja kuonesha utamaduni wao, na palepale idara kama maktaba zinashiriki katika tamasha hilo na kutekeleza jukumu lao la kuwaelimisha watu. Pia tunaanzisha kamati za lugha katika sehemu mbalimbali nchini, kuhifadhi lugha mbalimbali ili tusipoteze lugha hizo ambazo ni vyombo vya kueleza utamaduni. Vilevile kuna kamati ya mambo ya muziki na mambo ya dansi. Shule na vyuo vikuu vilevile vitafanya matamasha ya utamaduni na matamasha ya muziki kila mwaka.

Hivi sasa tunashuhudia sekta ya utalii ya Kenya ikiendelea kukua kwa kasi sana, na urithi wa utamaduni ukiwa vivutio vikubwa vya kitalii umeipatia serikali mapato makubwa, kama vile Kisiwa cha Lamu, Vijiji vya Wamasai, vitu kama hivyo vikiachwa wazi kwa watalii, vitaharibika kwa kiasi fulani, je, serikali ya Kenya inafanya uwiano namna gani ili kuendeleza sekta ya utalii, na kwa upande mwingine kuhifadhi vizuri urithi wa utamaduni?

Urithi wetu wa utamaduni una maana sana, kwa sababu huo ni maisha yetu, tukipoteza urithi wa utamaduni hatuwezi kuishi maisha mazuri. Kwa hivyo serikali haitakubali utalii uharibu utamaduni. Kutokana na kutaka pesa za haraka, baadhi ya watu hawajali mambo ya utamaduni. Serikali ina njia nyingi za kuhifadhi mambo ya utamaduni na kuendeleza utalii kwa sambamba. Kama nilivyosema kila baada ya muda fulani matamasha ya utamaduni yanafanyika katika kila mkoa, na watalii wanaweza kushiriki kwenda kwenye matamasha hayo na kuona mambo yote ya utamaduni wetu bila kuyaharibu. Aidha tunawashirikisha wataalamu wa utamaduni katika utalii, wataalamu hao watakuwa pale na kuangalia kama mambo ya utamaduni yanahifadhiwa vizuri au la. Pia tumeandaa mkataba wa kuvutia mitaji ya kiutamaduni, lengo lake ni kuhimiza biashara kwa kupitia mambo ya utamaduni, kama kutumia vilivyochongwa, muziki na nyimbo zinazoeleza mambo ya utamaduni na kuendeleza uchumi wetu.