Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-15 16:11:17    
Maisha ya mhamiaji wa kwanza katika mradi wa maji wa magenge matatu yalivyo sasa

cri

Mradi wa magenge matatu katika mto Changjiang nchini China, ni mradi mkubwa kabisa wa maji duniani wenye malengo ya kudhibiti mafuriko, kuzalisha umeme na kuhimiza usafiri wa meli. Ujenzi wa mradi huo ulioanzishwa mwaka 1992 unatarajiwa kukamilika kabisa mwaka 2009.

Kwa mujibu wa usanifu wa mradi wa magenge matatu, limejengwa boma la kuzuia maji lenye urefu wa mita 185 na upana zaidi ya mita 2,300. Kwa hiyo ilibidi wakazi walioishi katika eneo la bwawa la mradi huo wahamishwe. Miongoni mwa mamilioni ya wakazi hao, nyumba ya Bw. Liu Anxing ilikuwa ya kwanza kuzama kwenye maji. Tarehe 20 May, ujenzi wa boma la kuzuia maji ulipokamilika, mwandishi wetu wa habari alimtembelea bwana huyo katika makazi yake mapya.

Hili ni jengo lenye ghorofa mbili, familia ya Bw. Liu yenye watu wanne wanaishi katika jengo hilo lenye ukubwa wa mita 240 za mraba. Mizabibu na mipichi iliyo mbele ya jengo hilo imeanza kuzaa matunda. Mbegu za rapa (rapeseed) zilikuwa zimeanikwa na kukauka mbele ya mlango wa nyumba hiyo, na nguruwe waliokuwa wanafugwa ndani ya zizi. Bw. Liu Anxing alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, "Manufaa hayo yanatokana kuhama, la sivyo ningeweza kupata vipi pesa ya kuweka simu nyumbani?"

Bw. Liu Anxing mwenye umri wa miaka 48 alikuwa anaishi katika kijiji cha Taipingxi, mkoani Hubei, China. Kijiji hicho kilikuwa karibu sana na boma la kuzuia maji katika eneo la bwawa la mradi wa magenge matatu.

Mwezi Machi mwaka 1995, serikali ilifanya mkutano wa hadhara wa kuwahamasisha wakazi wa kijiji cha Taipingxi kuhama. Bw. Liu Anxing alikuwa mtu wa kwanza aliyekubali kwa hiari kuhamia kijiji kingine cha Baishuwan, kilichopo mita 180 juu ya usawa wa bahari. Baadaye wanakijiji wengine wa familia zaidi ya 30 waliiga mfano wake na wakahama kabla ya tarehe iliyopangwa.

Bw. Liu Anxing alisema mwezi Agosti mwaka 1995 alipohamia kutoka kando ya mto Changjiang, serikali ilimpa ruzuku ya RMB karibu Yuan elfu 30, na yeye mwenyewe alichukua akiba yake ya zaidi ya Yuan elfu 10, pesa hizo zilitumika kujenga nyumba hiyo ya saruji yenye ghorofa mbili. Alisema hapo awali aliishi kwa miaka 50 katika nyumba ya kizamani iliyotengenezwa kwa mbao na udongo, ukubwa wake ulikuwa mita za mraba 80 tu. Baada ya kuhama, nyumba waliyohamia ilikuwa ya ghorofa. Kijiji kiligharamia kuweka mabomba ya maji safi na kutengeneza shimo la kuzalisha gesi ya kinyesi katika makazi mapya. Mbali na hayo, makazi hayo yanapakana na barabara ya lami. Licha ya simu, familia hiyo ilinunua televisheni kubwa ambayo inaweza kupokea vipindi vya vituo zaidi ya 10 vya televisheni.

Nje ya nyumba yake, Bw. Liu Anxing alimwoneshea mwandishi wetu wa habari kuwa, nyumba ya zamani imezama ndani ya maji. Alisema, "Tuliacha maskani yetu ya zamani na kuhama kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa magenge matatu, kwa ajili ya taifa, hatuna malalamiko. Lakini ilikuwa ni vigumu kwetu kuacha mashamba yetu yenye rutuba."

Mkurugenzi wa kijiji cha Taipingxi Bw. Wang Yanpin alieleza kuwa, kijiji hicho kina watu zaidi ya 2,300. Miongoni mwao watu 1,900 ni wahamiaji waliotangulia katika utekelezaji wa mradi wa magenge matatu, ambao walihama mwaka 1997. Hali ya makazi imeboreshwa, lakini wahamiaji hao bado wanakabiliwa na tatizo la mashamba. Kwa sababu mashamba yote yenye maji na yenye rutuba yamefunikwa na maji, yaliyobaki ni mashamba makavu, kwa hiyo wahamiaji wengi wanaweza tu kujitosheleza kwa chakula kwa kutegemea kilimo. Hivi sasa kamati ya kijiji hicho ina mpango wa kuanzisha mashamba mengine yenye ukubwa wa hekta zaidi ya 1 milimani, na kujenga gti moja la uchukuzi wa bidhaa. Pia inajitahidi kuvutia uwekezaji na kuwataarifu habari wanakijiji wanaotaka kufanya kazi mijini. Kwa upande wa serikali kuu ya China, pia inaendelea kutoa sera za kuwasaidia wahamiaji hao wajipatie pesa hatua kwa hatua.

Mwezi Aprili mwaka 1992, bunge la umma la China liliidhinisha ujenzi wa mradi wa maji wa magenge matatu. Katika utekelezaji wa kazi ya uhamiaji kati ya mwaka 1993 na mwaka 2005, watu zaidi ya milioni 1.1 waliondoka kutoka kwenye maskani yao na kuhamia katika makazi mapya.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-15