Waziri mkuu wa serikali ya China Bwana Wen Jiabao atafanya ziara rasmi ya kiserekali kuanzia tarehe 17 hadi 24 mwezi huu katika nchi 7 za Afrika, nchi hizo ni Misri, Ghana, Congo Brazaville, Angola, Afrika ya kusini, Tanzania na Uganda. Lengo la ziara yake ni kuzidisha urafiki, kuongeza uaminifu, na kupanua ushirikiano ili kupata maendeleo kwa pamoja.
Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bwana He Yafei alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, ziara hiyo ya waziri mkuu Wen Jiabao ni shughuli kubwa nyingine ya kidiplomasia ya China barani Afrika.
Alisema, wakati wa ziara yake hiyo, kwa nyakati tofauti waziri mkuu Wen Jiabao atajadiliana kwa kina na viongozi wa nchi hizo 7 kuhusu kuendeleza zaidi uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika, kupanga mwelekeo wa maendeleo ya siku zijazo, na kuimarisha urafiki wa jadi kati ya China na Afrika. Uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika ulianzia tangu enzi na dahari, mwaka huu ni mwaka wa 50 tangu China na Afrika zianzishe uhusiano wa kibalozi. Bwana He alisema, China na nchi za Afrika zikiwa nchi zinazoendelea, zinaungana mkono na kusaidiana, na uhusiano wa kirafiki na ushirikiano unaimarishwa na kuendelezwa siku hadi siku katika miaka 50 iliyopita. Alisema:
Mwaka 1956, thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilikuwa dola za kimarekani milioni 12 tu, na mwaka 2005 thamani hiyo iliongezeka na kufikia dola za kimarekani bilioni 39.7, hili ni ongezeko la zaidi ya mara elfu 3 katika miaka 50 iliyopita. Alisema:
Mwaka 2005, uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika ulifikia dola za kimarekani bilioni 1.18, na makampuni zaidi ya 800 ya China yameanzisha shughuli zao barani Afrika.
Katika miaka ya hivi karibuni, maendeleo mapya yamepatikana katika uhusiano kati ya China na Afrika, na ushirikiano kwenye sekta mbalimbali umepata matunda kemkem. Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lililoanzishwa mwaka 2000 limekuwa baraza muhimu la kufanya mazungumzo kati ya China na nchi za Afrika na limekuwa utaratibu wenye ufanisi wa kufanya ushirikiano wa kufuata hali halisi, kuanzishwa kwa baraza hilo kumesukuma mbele kwa nguvu maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika.
Tokea mwaka huu, hatua mbalimbali za kidiplomasia za China kuhusu Afrika zinafuatiliwa sana na watu. Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya China ilitoa waraka wa sera kwa Afrika, ambao umesisitiza kuimarisha urafiki wa jadi, na kupanua ushirikiano wa kunufaishana, pia kuweka lengo la kuanzisha na kuendeleza uhusiano wa aina mpya wa kimkakati na kiwenzi ulio na usawa na uaminifu kwenye mambo ya kisiasa kati ya China na Afrika; mwezi Aprili mwaka huu, rais Hu Jintao alifanya ziara katika nchi tatu za Afrika ambazo niMoroco, Nigeria na Kenya. Na safari hii waziri mkuu wa China atafanya ziara katika nchi 7, hii ni shughuli nyingine kubwa ya kidiplomasia ya China barani Afrika.
China na nchi za Afrika zina maoni ya pamoja na maslahi ya pamoja katika masuala mengi, na pande hizo mbili zote zina matumaini ya kuimarisha na kuzidisha ushirikiano. Wakati wa ziara ya waziri mkuu Wen Jiabao katika nchi hizo 7, China na nchi hizo zitasaini nyaraka nyingi. Bwana He alisema:
Nyaraka hizo zinahusu mambo mengi ya siasa, uchumi na biashara, tiba na afya, sayansi na teknolojia. Ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika unalenga kunufaishana na kupata maendeleo kwa pamoja, hasa tunalenga kuleta manufaa kwa wananchi wa Afrika, kuisaidia Afrika ijiendeleze au kuinua uwezo wake wa kujiendeleza.
Bwana He alisema, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika ni wa pande zote.China imechukua hatua kadhaa za kisera kwa ajili ya maslahi ya nchi za Afrika, kwa mfano kutoa ruzuku kwa makampuni ya China yanayoagiza bidhaa za Afrika, ili kuondoa hali isiyo ya utulivu ya biashara kati ya China na Afrika. Mwaka jana kwenye mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika, Rais Hu Jitao wa China alitangaza kufuta madeni ambayo china inazidai nchi za Afrika. Amesisitiza kuwa, ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye sekta za uchumi na biashara ni pamoja na ushirikiano kwenye sekta ya nishati, lakini hii ni sehemu moja tu ya ushirikiano kati ya China na Afrika.
Bwana He amedokeza kuwa, kwa kupitia ziara ya waziri mkuu Wen Jiabao, China itaendelea kutekeleza sera ya utoaji misaada kwa Afrika bila masharti yoyotete. Ziara hiyo ya waziri mkuu Wen Jiabao imeonesha kuwa, serikali ya China ina matumaini ya kushirikiana na nchi za Afrika katika kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika kwenye sekta mbalimbali.
|