Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-16 20:02:03    
Urafiki kati ya China na Misri kuimarishwa siku hadi siku

cri

Mwaka huu ni mwaka wa 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Misri. Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao ataanza ziara yake nchini Misri kuanzia tarehe 17 mwezi huu, na athudhuria shughuli za kuadhimisha miaka ya 50 ya uhusiano kati ya China na Misri. Misri ni kituo cha kwanza cha ziara yake katika nchi 7 za Afrika. Misri ni nchi ya kwanza katika dunia ya uarabu na barani Afrika kutambua hadhi ya China mpya na kuanzisha uhusiano na China. Baada ya miaka 50, urafiki kati ya nchi hizo mbili bado unaendelea kuimarishwa siku hadi siku.

Dr. Yussef Wali ni naibu katibu wa chama cha National Democratic cha Misri ambacho ni chama tawala cha nchi hiyo, amekuwa mwenyekiti wa shirikisho la urafiki kati ya China na Misri kwa miaka 36 na amekuwa rafiki mkubwa wa watu wa China. Dr. Yussef Wali ameshuhudia historia ya kirafiki kati ya nchi hizo mbili tangu miaka ya 50 ya karne iliyopita. Alisema:

"mwaka 1999 rais Jiang Zemin wa China na rais Hosni Mubarak wa Misri walikubaliana kuanzisha uhusiano wa ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, na mkakati huo bado unaendelea kutekelezwa mpaka leo. Kwenye msingi wa mkakati huo, rais Hu Jintao wa China alitembelea Misri muda mfupi baada ya kushika madaraka. Tukio hilo ni muhimu sana kama waziri mkuu Bwana Zhou Enlai alipofanya ziara nchini Misri miaka ya 50 ya karne iliyopita na kuanzisha uhusiano wa kibalozi kati ya nchi hizo mbili."

Mkutano wa Bandung uliofanyika mwaka 1955 ulikuwa ni mwanzo wa uhusiano kati ya China mpya na nchi za Asia na Afrika. China na Misri zilianzisha uhusiano rasmi katika mwaka wa pili na kuanzisha rasmi historia ya kuungana mikono na kushirikiana kati ya China na nchi za Asia na Afrika zinazoendelea. Katika miaka 50 iliyopita, China na Misri zimeendeleza urafiki mkubwa kwenye msingi wa kunufaishana na kushirikiana. Kama alivyosema Dr. Yussef Wali, urafiki huo umeweka msingi thabiti kwa kuanzishwa kwa uhusiano wa ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili.

Dr. Yussef Wali aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Misri, alikuwa katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu katika miaka ya 90 ya karne iliyopita. Mwaka 1993 alifanya ziara nchini China akiwa katika wadhifa wa katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu na alipokelewa na rais wa wakati huo wa China Bw. Jiang Zemin. Kutokana na juhudi zake, mnamo mwezi Agosti mwaka huo, Umoja wa nchi za kiarabu ulifungua ofisi mjini Beijing na kufungua ukurasa mpya wa mawasiliano ya kirafiki kati ya China na Umoja huo. Dr. Yussef Wali alisema:

"wakati nilipokuwa katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu, umoja huo ulifungua ofisi mjini Beijing, na tukio hilo ni alama dhahiri ya kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano kati ya China na nchi za kiarabu. Urafiki kati ya China na Misri ni imara na utadumu milele."

Katika miaka 50 ya uhusiano, China na Misri si kama tu zinaungana mkono katika mambo ya kimataifa, bali pia zinashirikiana katika mambo ya uchumi, biashara na utamaduni. Dr. Yussef Wali alisema:

"katika miaka ya hivi karibuni, China iliwekeza fedha nyingi nchini Misri, na Misri pia inataka China iongeze uwekezaji nchini humo, hasa katika teknolojia za upashanaji habari, miradi mikubwa ya ujenzi, na sekta ya mafuta, hali hiyo imenufaisha wananchi wa nchi hizo mbili. Katika mambo ya kiutamaduni, China ilifungua kituo cha utamaduni nchini Misri katika miaka kadhaa iliyopita, ambacho ni kituo cha kwanza cha utamaduni wa China barani Afrika. Shughuli nyingi zilizoandaliwa na kituo hicho zimesukuma mbele uhusiano wa kirafiki kati ya China na Misri, na hasa kati ya China na Afrika.