Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-19 19:26:24    
Waziri mkuu wa China afafanua kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika

cri

Waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao tarehe 18 mwezi huu kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika huko Cairo, nchini Misri alifafanua masuala kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika.

Bwana Wen Jiabao alisema, ushirikiano kati ya China na Afrika umekuwa na historia ya nusu karne. Katika nusu karne iliyopita, hata katika hali ambayo China yenyewe ilikumbwa na taabu kubwa, lakini ilitoa uungaji mkono wenye thamani na misaada kwa kadiri iwezekanavyo kwa wananchi wa nchi mbalimbali za Afrika. Katika muda wa miaka 50, misaada ya aina mbalimbali iliyotolewa na China kwa Afrika ilifikia fedha za renminbi yuan bilioni 44.4, ambapo miradi 900 ya ujenzi wa miundo mbinu na majengo ya umma barani Afrika ilitekelezwa. China ilituma madaktari wapatao eflu 16 kwa nchi 43, ambapo waliwatibu wagonjwa milioni 240.

Bwana Wen Jiabao alisema, misaada ya China kwa Afrika inahusu sekta mbalimbali pamoja na misaada kwa maendeleo ya uchumi wa kitaifa ya nchi mbalimbali za Afrika. Alisema:

China inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano na Afrika katika sekta za uchumi na biashara, tunaweka mkazo katika kupanua uagizaji bidhaa za kutoka nchi za Afrika, China itachukua hatua za kuzisaidia nchi za Afrika kuzitambulisha bidhaa zao nchini China; kuunganisha kazi ya misaada ya kiteknolojia na kiuchumi kwa Afrika na ushirikiano kwa kuisaidia Afrika iongeze uwezo wa kujiendeleza; na China itatoa nguvu kubwa kuisaidia Afrika kuwaandaa mataalamu na watu wenye uwezo wa usimamizi .

Hivi sasa China imefuta madeni ya yuan bilioni 10.5 ya nchi 31 za Afrika, na China imepunguza na kusamehe ushuru wa forodha kwa bidhaa za aina 1900 zilizouzwa na nchi 29 za Afrika nchini China.

Bwana Wen Jiabao alisema, kwenye mkutano wa 2 wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika huko Addis Ababa, Ethiopia miaka mitatu iliyopita, China ilitoa lengo la kuzisaidia nchi za Afrika kwa kuwaandaa wataalamu wa aina mbalimbali wapatao elfu 10, na lengo hilo litatimia mwaka huu.

Bwana Wen Jiabao alisema, mwezi Novemba mwaka huu, Mikutano ya Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika na wa wakuu wa China na Afrika itafanyika hapa Beijing, ambapo serikali ya China itaweka mkazo katika kupunguza na kusamehe madeni, kutoa misaada ya kiuchumi, kuwaandaa watu wenye ujuzi na kuhamasisha makampuni ya china yawekeze barani Afrika. Alisema:

Mkutano wa wakuu wa China na Afrika utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu ni mkutano utakaofanyika kwenye msingi wa mkutano wa mawaziri wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, tutachukua fursa hii kuimarisha urafiki na ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na nchi mbalimbali za Afrika.

Alipozungumzia msimamo wa serikali ya China kuhusu uhusiano na ushirikiano kati ya China na Afrika, Bwana Wen Jiabao alisema:

Serikali ya China siku zote inafuata sera ya kuheshimiana, kuwa na usawa na kunufaishana, na kutoingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine, tuna imani kuwa, sehemu mbalimbali na wananchi wa nchi mbalimbali wana haki na uwezo wa kutatua masuala yao yenyewe. China inapenda sana kuona uchumi wa kitaifa wa nchi mbalimbali za Afrika unandelea vizuri, jamii za nchi mbalimbali za Afrika zinatulia, mifumo yao ya sheria ya kidemokrasia inakamilika na wananchi wao wanaishi maisha mazuri.

Waziri mkuu Wen Jiabao amesisitiza kuwa, China inashikilia sera ya kidiplomasia ya amani iliyo ya kujitawala na kujiamulia, China inaendeleza urafiki na ushirikiano na nchi za Afrika, jambo hili halilengi upande mwingine wa tatu, na maendeleo ya uchumi na biashara ya China na Afrika pia hayawezi kuzuia maslahi ya nchi nyingine yoyote.