Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-19 20:08:01    
Maporomoko ya maji ya Huangguoshu

cri

Maporomoko ya maji ya Huangguoshu yako kwenye sehemu ya vivutio vya Maporomoko ya Huangshuo mkoani Guizhou, kusini magharibi ya China. Katika sehemu hiyo, kuna maporomoko 18 ambayo yanaonekana kwenye uso wa dunia, ambayo yameundwa kuwa kundi kubwa la maporomoko. Kati ya maporomoko hayo, Maporomoko ya Huangguoshu ni makubwa zaidi kuliko mengine, na pembezoni mwake kuna maporomoko mengi ya maji ambayo yanaonekana kama ni mikufu mbalimbali ya lulu inayoning'inia kwenye mtiririko wa juu na wa chini wa mto wa sehemu hiyo.

Maporomoko ya maji ya Huangguoshu yana urefu wa mita 74, kama jumba lenye ghorofa zaidi ya 20, maji ya mto yanayokimbia kwa kasi yanaporomoka kuelekea chini kutoka kwenye kilele cha miamba hadi kwenye bwawa la Xiniu, kasi ya maporomoko inawashtusha sana watu, ambapo maji na mawe yanagongana na kutoa sauti kubwa ya ngurumo pamoja na moshi na ukungu, na mawimbi makubwa yanayokwenda kasi mtoni, nguvu yake haizuiliki. Ndiyo maana pembezoni mwa maporomoko ya maji, siku zote kuna mawingu na ukungu, hata watalii walioko nje ya maporomoko kwa mita 50 hadi 60, nguo zao huloweshwa kabisa na mawingu na ukungu huo.

Maporomoko ya maji ya Huangguoshu, neno Huangguo, maanani yake ya kichina na matunda ya kimanjano, hivyo watalii wengi waliofika sehemu ya Maporomoko ya maji ya Huangguoshu, waliuliza swali kama hilo: Je, jina la Maporomoko ya Huangguoshu lilitokana na nini? Je ni kutokana na bustani moja ya matunda? Mwongozaji wa utalii wa sehemu hiyo Bi.Chen Xiujuan alituambia:

Watalii wengi wanadhani kuwa jina la maporomoko ya maji ya Huangshu linatokana na matunda ya kimanjano, lakini kwa kweli ni kutokana na miti ya aina ya ficus indica Huanggerong. Sehemu hiyo ina mwinuko wa chini kutoka usawa wa bahari, na hali ya hewa ni joto, ambayo inafaa kwa ukuaji wa miti ya aina ficus indica, na mingi zaidi ni Huanggerong. Sehemu hiyo pia inazalisha matunda ya kimanjano, Huangguo, ambayo ni kama machungwa, ngozi yake ya kimanjano, ladha ni tamu na chachu. Wakazi wa sehemu hiyo wakitamka neno Huangge, ni kama wanasema Huangguo, hivyo wakazi wa huko waliita miji hiyo kuwa ni miji ya Huangguo, na maporomoko ya maji ya huko yameitwa kuwa ni Maporomoko ya maji ya Huangguoshu.

Yakilinganishwa na maporomoko makubwa maarufu duniani, Maporomoko ya maji ya Huangguoshi siyo makubwa, lakini umaalum wa sehemu ya Huangguoshu ni kuwa, watalii wanaweza kuingia ndani ya pango moja lililoko ndani ya milima, wakaangalia maporomoko ya maji kutoka nyuma yake. Pango hilo liko katikati ya maporomoko, urefu wa pango ni zaidi ya mita 100, na linaenda sambamba na maporomoko. Ndani ya pango kuna madirisha 6 ya pango, kupitia madirisha hayo watu wanaweza kuangalia kwa karibu maporomoko yanayodondoka chini kutoka juu moja kwa moja, hata wanaweza kuyagusa maporomoko ya maji. Hali hii ni ya pekee duniani, kweli ni ya ajabu. Mtalii kutoka Beijing Bi. Han Ye alisema, alipopita kwenye pango hilo, alikumbuka hali iliyosimuliwa kwenye hekaya maarufu ya China ya kale iitwayo: Kwenda magharibi kutafuta msahafu, kwani mhusika Sun Wukong yaani mfalme kima wa hekaya hiyo ndiyo aliishi ndani ya pango moja lenye pazia la maji. Alisema:

Naona Maporomoko ya Huangguoshu ni maporomoko ya maji yanayopendeza zaidi niliyoona, na pango la maporomoko hayo ni pango lenye vivutio zaidi kwenye sehemu hiyo, tulipotazama maporomoko hayo kwa kupitia dirisha la pango, tuliona hali nzuri ya ajabu ya maporomoko hayo, ambapo tulitazama maporomoko ya maji tukiwa ndani ya pango, tuliona kuwa nje ni maji matupu, hivyo maporomoko ni kama pazia la maji la pango hilo. Ndani ya pango hilo nilidhani mimi ni kama kima mdogo niliweza kuhisi hali iliyosimuliwa kwenye hekaya kuhusu mfalme kima Sun Wukong akila na kunywa pamoja na kima wenzake ndani ya pango lenye pazia la maji.

Bi. Han Ye alisema tulipoingia kwenye sehemu ya maporomoko ya maji, hii kwanza inahitaji moyo wa ujasiri, na tukitaka kupita maporomoko hayo makubwa ya maji, kweli tulitakiwa kukaza nia bila woga. Lakini kama ukifika kwenye maporomoko ya maji ya Huangguoshu, usipoingia ndani ya pango lenye pazia la maji, na usipopata nafasi ya kupapasa maporomoko ya maji, kweli huwezi kuona hali halisi ya mvuto wa maporomoko hayo ya maji.

Watalii wakiingia ndani ya pango lenye pazia la maji, wanaweza kuona mandhari nzuri ya ajabu, kwamba kwa kupitia kila dirisha la pango hilo, wanaweza kuona upinde wa rangi juu ya bwawa la Xiniu, si kama tu ni wa rangi zote 7, bali upinde huo unaweza kubadilikabadilika na kusogeasogea kutokana na watu wanavyotembea. Watalii wakiingia kwenye pango hilo la mawe, wakiegemea dirisha na kuangalia maporomoko ya maji na upinde wa rangi mbalimbali, hata wanaweza kupapasa maporomoko ya maji, hii kweli ni furaha kubwa ya ajabu. Mtalii kutoka Japan Bwana Abe alisema:

Hivi sasa duniani kuna maporomoko matatu makubwa zaidi ya maji, niliwahi kwenda kutazama maporomoko ya maji nchini Marekani na Zimbabwe. Baada ya kuangalia Maporomoko ya maji ya Huangguoshu, naona mvuto wa maporomoko hayo hata ni mkubwa zaidi kuliko yale mawili nchini Marekani na Zimbabwe. Kwani watalii wanaweza kupita kwenye pango la mawe kutoka nyuma ya maporomoko hayo halafu kutazama maporomoko moja kwa moja, naona katika nchi nyingine duniani, watu hawawezi kupata fursa ya kutazama maporomoko makubwa namna hii.

Lakini hali ya kusikitisha ni kuwa, kutokana na eneo la Huangguoshu kuwa kwenye sehemu ya kijiografia ya chokaa, ambapo kuna mawe mengi ya chokaa, maji ya huko ni rahisi kutoweka, hivyo imeleta taabu kwa kudumisha kiasi cha maji ya kutosha kwenye sehemu ya Maporomoko ya maji ya Huangguoshu. Hivi sasa kiasi cha maji ya maporomoko hayo kinategemea mvua katika nusu mwaka, na katika nusu mwaka mwingine, maji ya kutosha ya maporomoko hayo yanatolewa kwa kutegemea kazi ya marekebisho ya nguvu za binadamu, hii inaweza kuathiri kwa kiasi fulani mvuto wa ajabu wa maporomoko hayo.