Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-19 20:25:29    
China yatangaza sehemu nyingine elfu moja za hifadhi ya kitaifa ya urithi wa utamaduni

cri

 

Waziri mkuu Wen Jiabao tarehe 25 mwezi uliopita alisaini amri ya kutangaza kundi la sita la sehemu za hifadhi ya kitaifa ya urithi wa utamaduni nchini China. Hii inamaanisha kuwa China imeongeza sehemu 1080 za hifadhi ya kitaifa ya urithi wa utamaduni. Idadi hiyo imekuwa karibu sawa na jumla ya makundi matano yaliyotangazwa katika miaka 50 iliyopita.

Waziri wa utamaduni wa China Bw. Sun Jiazheng katika siku hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, wakati "siku ya urithi wa utamaduni" ilipokaribia, kutangaza kuongeza idadi hiyo kubwa ya sehemu ya hifadhi ya urithi wa utamaduni, kunamaanisha kuwa serikali inatilia mkazo hifadhi ya urithi wa utamaduni.

Mwishoni mwa mwaka jana, serikali ya China iliamua kwamba kuanzia mwaka huu, kila J'mosi ya pili Juni iwe "siku ya urithi wa utamaduni" nchini China. Hivi sasa idara husika zinafanya shughuli za aina mbalimbali kuadhimisha siku hiyo. Bw. Sun Jiazheng alisema, "Kuwekwa kwa siku hiyo kunamaanisha kuwa, kwanza kazi ya kuhifadhi urithi wa utamaduni ni yenye umuhimu, pili kazi ya kuhifadhi urithi wa utamaduni ni ngumu, na tatu ni lazima kazi hiyo iwashirikishe wananchi wote ili kuifanikisha."

Katika miaka ya karibuni, China imekuwa ikiweka mkazo zaidi katika hifadhi ya urithi wa utamaduni na maingiliano ya kiutamaduni. Serikali inatilia mkazo kustawisha mashirika ya utamaduni, na duniani maingiliano ya kiutamaduni yamekuwa sehemu muhimu katika ushirikiano kati ya China na nchi za nje na pia ni mambo muhimu katika maingiliano ya kidiplomasia. Urithi wa utamaduni wa China wenye miaka elfu kadhaa ni raslimali kubwa ya kustawisha maingiliano hayo.

Kwa mujibu wa takwimu, hivi sasa kuna urithi wa utamaduni usioweza kuhamishika zaidi laki nne, na vitu vya kale kwenye majumba ya makumbusho ni zaidi ya milioni 20. Mkuu wa Idara Kuu ya Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni nchini China Shan Jixiang alisema, hivi sasa China iko tayari kufanya uchunguzi wa urithi wa utamaduni kwa mara nyingine kote nchini, ili kuandaa sera za hifadhi ya urithi wa utamaduni. Alisema, "Mwaka 1956 na mwaka 1981, China ilifanya ukaguzi mara mbili kote nchini kuhusu urithi wa utamaduni. Mwaka huu tutafanya ukaguzi kwa dhana mpya na sheria mpya na teknolojia mpya."

Katika siku chache zilizopita, licha ya kutangaza urithi wa utamaduni unaoonekana, serikali ya China pia imetangaza orodha ya majina ya urithi wa utamaduni usioonekana, urithi huo ni wa aina 518 ukiwa ni pamoja na mila na desturi za makabila, na sanaa za kienyeji. Lakini kutokana na upungufu wa uzoefu, kazi ya kuhifadhi utamaduni usioonekana itakuwa ngumu. Naibu waziri wa utamaduni Bw. Zhou Heping alizitaka serikali zote za mitaa zijiandae haraka kufanya kazi hiyo. Alisema, "Tumeanza kuandaa sera za kuhifadhi utamaduni usioonekana pamoja na mpango wa hifadhi, kuweka mafaili kwa maandishi na picha, na kuunga mkono mitaa kujenga majumba ya makumbusho ya mila na desturi za wenyeji na majumba ya makumbusho ya urithi wa utamaduni usioona."

Maendeleo ya haraka ya miaka 20 iliyopita nchini China yamesababisha wimbi la kupanuka kwa miji, wimbi hilo kwa kiasi kikubwa limeathiri vibaya urithi wa utamaduni. Hivi sasa, hali hiyo kimsingi imedhibitiwa. Waziri wa utamaduni, Bw. Sun Jiazheng alisema, serikali imetambua hali hiyo mbaya. Alisema, "Hali ya hifadhi ya urithi wa utamaduni si nzuri, kazi zitakuwa nyingi na ngumu. Serikali inapaswa kutilia mkazo uongozi, na kwa upande mwingine jamii nzima inatakiwa kuwa na mwamko wa kuthamini urithi huo na wananchi wote wanatakiwa wajitokeze kuuhifadhi urithi wetu."

Ingawa kazi ni ngumu, lakini Bw. Sun Jiazheng alisema, kwa kuwa serikali imetambua umuhimu wa kazi hiyo, hakika itachukua hatua za haraka.