Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-22 16:09:58    
Watoto wanaozurura mitaani wapata familia

cri

Li Wen ni mtoto mwenye umri wa miaka 14. Hivi sasa anasoma katika shule ya msingi mjini Zhengzhou, katikati ya China. Mtoto huyo alimweleza mwandishi wetu wa habari ndoto yake akisema, "Nataka kusoma kwenye chuo kikuu na baadaye kufanya kazi ya mwanaanga."

Mtu angemwona mtoto huyo kabla ya hali aliyonayo sasa, angebaini kuwa alikuwa anazurura mitaani tangu kutoroka nyumbani kwao. Lakini hivi sasa Li Wen anakwenda mchana, na kurudi nyumbani jioni, kama walivyo watoto wengine wa umri wake, hiyo ni kutokana na kupata familia moja yenye baba na mama, ambao wote ni watu wanaojitolea, pamoja na ndugu wanne waliokuwa watoto wanaozurura mitaani.

Katika familia hiyo, watu wanaojitolea ambao wanajifanya kama ni baba na mama, wanawapikia chakula watoto, kuwanunulia nguo, kuwasaidia katika masomo na kufuatana nao kwenda katika bustani.

Mwaka 2003 familia ya kwanza ya namna hii ilianzishwa katika mji wa Zhengzhou, nchini China. Sasa watoto 84 waliokuwa wanazurura mitaani wanaishi katika familia 5 za namna hii, ambapo wamejengewa mazingira na maadili mazuri.

Mji wa Zhengzhou ni wa kwanza miongoni mwa miji ya China kutelekeza mpango huo wa kuwasaidia watoto waliokuwa wanazurura mitaani kutokana na hiari yao.

Tangu miaka mitatu iliyopita, serikali ya China ilianza kutelekeza njia mpya ya kuwasaidia watoto waliozurura mitaani. Watoto hao wanapelekwa kwenye kituo cha utoaji misaada na baadaye kurudishwa makwao, hata hivyo watoto kadhaa wanaondoka nyumbani kwa mara nyingine tena.

Mkuu wa kituo cha utoaji misaada cha mji wa Zhengzhou Bw. Wang Wanmin alieleza kuwa, mwaka jana watoto karibu elfu 2 waliokimbilia mji wa Zhengzhou na kuzurura mitaani kama alivyofanya Li Wen, walipata misaada. Takwimu kutoka wizara ya mambo ya raia ya China zinaonesha kuwa, idadi hiyo ilikuwa laki 1 na elfu 50 kote nchini kwa mwaka jana.

Kwa maoni ya Bw. Wang Wanmin, yeye na wenzake wanafanya kazi kubwa ya kuwapa pole na upendo watoto waliozurura mitaani wakitumia mbinu mbalimbali. Lakini jambo asilotarajia ni kuwa, watoto hao wana ndoto kubwa za namna hii.

Profesa Zhang Mingsuo wa chuo cha sayansi ya jamii chini ya chuo kikuu cha Zhengzhou alisema, "Hapo awali idara za mambo ya raia hazikuwafuatilia sana watoto waliozurura mitaani, sembuse kuwalinda na kuwaelimisha. Lakini hivi sasa serikali imebadilisha mtizamo, ikaanza kuwaheshimu na kuzingatia haki yao ya kuishi, kupata maendeleo na elimu na kujiunga na jamii." Profesa Zhang ndiye miongoni mwa waanzishi wa harakati ya uundaji wa familia badia katika kuwasidia watoto hao.

Katika familia bandia anakoishi Li Wen, ana kaka mmoja anayeitwa Xu Yan. Mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miaka 15 anatoka katika kijiji kimoja mkoani Shanxi. Anapenda kutizama filamu na vipindi vya televisheni vinavyohusu mambo ya kijeshi, hususan vita vya kupambana na wavamizi wa Japan. Alisema anataka kwenda kuitembelea Japan na kuishuhudia nchi hiyo mwenyewe, ili kupata ukweli wa historia.

Xu Yan anajifunza upishi katika shule moja mjini Zhengzhou. Katika daftari lake, anaweka kumbukumbu za matamshi ya maneno ya Kijapan yanayotumika sana. Alisema "Hadi nitakapotimiza umri wa miaka 25, nitaweza kulimbikiza pesa za kutosha za kuitembelea Japan."

Mtoto huyo anajiona ni mwenye bahati kwa vile hivi sasa anaonekana ataweza kutimiza ndoto yake. Alisema "Kama nisingefika kituo cha utoaji misaada, ningebadilika kuwa mbaya sana. Ningeweza kuwa kama wengine ambao bado wanazurura mitaani, ningeweza kusema uwongo, kupigana na kuiba."

Mtoto mwingine wa kiume katika familia hiyo bandia anaitwa Zhang Qi, ndoto yake ni kumiliki saloon moja. Hivi sasa amejifunza ufundi wa kunyoa nywele, na anafanya mazoezi katika saloon moja. Wakati wa mapumziko pia ananyoa nywele za watoto wenzake wanaoishi katika familia hiyo.

Li Wen na watoto hao wawili wa kiume wote wanatoka familia ambazo wazazi wao waliachana. Profesa Wang Wanmin alieleza kuwa, asilimia 80 ya watoto waliosaidiwa na kituo cha utoaji misaada kwa watoto waliozurura mitaani, wanatoka familia ambazo wazazi wao waliachana.

Wataalamu wanaona kuwa, tatizo la watoto hao ni matatizo ya familia kuoneshwa kwenye jamii, lakini mpaka hivi sasa China bado haina sheria inayolinda maslahi ya watoto.

Ofisa wa wizara ya mambo ya raia ya China alisema hivi majuzi kuwa, kazi ya kituo cha utoaji misaada kwa watoto waliozurura mitaani inasaidia utungaji wa utaratibu wa kuwalinda watoto hao wa mitaani.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-22