Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao tarehe 22 mwezi juni alitoa hotuba kwenye baraza la kwanza la ushirikiano wa kibiashara kati ya China na Afrika Kusini.
Katika hotuba yake, Bw. Wen Jiabao amesema ili kujenga na kukuza uhusiano wa kiwenzi na kimkakati kati ya China na Afrika, pande hizo mbili zinapaswa kushikilia kwa usawa na uaminifu katika mambo ya kisiasa, kuhimiza kunufaishana katika mambo ya kiuchumi, na kuimarisha mawasiliano katika sekta za utamaduni na jamii, ili kuongeza maelewano na urafiki.
Bw. Wen Jiabao amesisitiza, China na Afrika zinapaswa kushirikiana kwa karibu katika sekta ya siasa na mambo ya kimataifa. Alisema (sauti 1) "China itaendelea kutetea maslahi ya Afrika katika jukwaa la kimataifa, kuunga mkono juhudi za nchi za Afrika katika kulinda mamlaka ya nchi na uhuru na kutimiza amani na utulivu barani Afrika. Ikiwa nchi mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, China inatetea matakwa ya haki ya Afrika yaheshimiwe, na inapinga hali ya nchi zenye nguvu kuzidharau nchi dhaifu na kuwepo kwa vigezo viwili katika mambo ya kimataifa."
Mwaka huu China na nchi za Afrika zinaadhimisha miaka 50 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi. Katika miaka hiyo 50 iliyopita, wananchi wa China na Afrika wamekuwa wakisaidiana katika kazi za kulinda mamlaka na kutetea heshima za mataifa yao, kushirikiana katika kulinda amani ya dunia na maslahi ya nchi zinazoendelea, na kujenga urafiki mkubwa. Bw. Wen Jiabao amesema uhusiano kati ya China na Afrika wenye usawa na urafiki wa dhati ni mfano wa kuigwa wa mahusiano kati ya nchi mbalimbali duniani.
Kuhusu ushirikiano wa sekta za uchumi na biashara, Bw. Wen Jiabao amesisitiza uhusiano wa kunufaishana na kuimarisha mawasiliano kati ya pande hizo mbili. Alisema (sauti 2) "China itatekeleza hatua za kuinufaisha Afrika na nchi nyingine zinazoendelea, hatua hizo ni pamoja na kufuta ushuru wa forodha, kuongeza misaada na kufuta madeni. China inahimiza viwanda vingi zaidi kuwekeza barani Afrika, vile vile China itaipa Afrika teknolojia, kuendeleza biashara na kuzidi kuagiza bidhaa kutoka Afrika."
Bw. Wen Jiabao amesema maendeleo ya China yametoa mustakabali mzuri wa soko kubwa kwa dunia nzima, pia yametoa fursa nyingi zaidi kwa nchi za Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni, thamani ya biashara kati ya China na Afrika iliongezeka kwa kasi, na bidhaa zinazoagizwa na China kutoka Afrika pia zimeongezeka sana. Mwaka jana thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 39.8, ambapo China iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 21.1 za kimarekani kutoka Afrika, kiasi ambacho kilizidi kile kilichosafirishwa na China barani Afrika. Amesema China itafanya ushirikiano na Afrika katika maeneo makubwa zaidi na ngazi ya juu zaidi, ili pande hizo mbili zisaidiane kiuchumi.
Bw. Wen Jiabao aliongeza kuwa, China inatilia maanani ufuatiliaji wa nchi kadhaa za Afrika kuhusu pengo la biashara na masuala mengine kuhusu bidhaa za nguo. Na China inajitahidi kutafuta ufumbuzi wa masuala hayo.
Aidha, katika sekta za utamaduni na jamii, China itaendelea kuiunga mkono Afrika katika juhudi zake za kuendeleza elimu, afya na utamaduni. China itatoa nafasi nyingi zaidi kwa wanafunzi wanaotaka kusoma nchini China na kuzisaidia nchi za Afrika kujenga shule. China pia itaendelea kutuma madaktari barani Afrika, kutoa misaada ya dawa za malaria, kujenga vituo vya kinga dhidi malaria na kufanya ushirikiano na Afrika katika mapambano dhidi ya ukimwi.
Bw. Wen Jiabao alisisitiza kuwa, China inaziheshimu nchi za Afrika zichague zenyewe mifumo ya kisiasa na njia za kujiendeleza kutokana na hali halisi za nchi zao, na China haina nia ya kueneza mitizamo yake ya thamani na njia ya kupata maendeleo barani Afrika. Hasa hasa waziri mkuu alisisitiza kuwa, ushirikiano wa China na Afrika hauzuii ushirikiano kati ya upande wa tatu wa China au Afrika, wala hauathiri maslahi ya upande wa tatu.
|