sauti mnayoisikia hivi sasa ni ya mitambo ya kutia rangi vitambaa iliyoko katika karakana ya kiwanda cha nguo cha Urafiki, ambacho ni kiwanda kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Tanzania na China. Karibu kila mtanzania anajua kiwanda cha nguo cha Urafiki, ambacho kilijengwa katika miaka ya 60 ya karne iliyopita kutokana na msaada wa serikali ya China, na sasa kimekuwa kiwanda cha nguo kinachoendeshwa kwa ubia na pande hizo mbili kwa pamoja baada ya kiwanda hicho kupata mikopo ya nafuu iliyotolewa na serikali ya China.
Katika karakana ya utiaji rangi vitambaa, mitambo inaunguruma kwa sauti kubwa, na mvuke unatoka kwa wingi kwenye bwawa la maji ya rangi, hali ambayo ni vigumu kwa watu kuamini hali ya kuzorota kwa kiwanda hicho. Naibu meneja mkuu wa kiwanda hicho Bw. Yu Kaiming alisema,
"Kiwanda cha nguo cha Urafiki kilikuwa karibu kufungwa mwaka 1995, ndani ya karakana hakukuwa na sauti ya mitambo, wengi wa wafanyakazi wa kiwanda hicho walipata likizo bila malipo kutokana na kiwanda kuingia hasara kiasi cha dola za kimarekani zaidi ya milioni 10. Kiwanda kilishindwa kutoa mshahara kwa wafanyakazi wala kulipa kodi kwa serikali, na kuwa mzigo usiobebeka kwa idara ya fedha ya serikali ya Tanzania."
Kiwanda cha nguo cha Urafiki kilijengwa kwa msaada wa serikali ya China mwaka 1966 kutokana na ombi la rais wa kwanza wa Tanzania hayati Mwalimu Julias K. Nyerere. Kiwanda hicho kilistawi sana katika kipindi fulani baada ya kuanza kazi mwaka 1968. Bw. Yu Kaiming alisema, kiwanda cha nguo cha Urafiki kilizorota baada ya kutekelezwa utaratibu wa soko huria nchini Tanzania katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, ambapo mfumo wa zamani haukuweza kuendana na hali mpya, pamoja na uendeshaji kazi usio mzuri, kuchakaa kwa mitambo, teknolojia iliyopitwa na wakati na kupungua kwa soko la bidhaa.
Ili kufanya ua hilo la urafiki lililopandwa na viongozi wa kizazi kilichopit wa nchi mbili za China na Tanzania lisinyauke, na kutokana na ombi la idara husika ya serikali ya Tanzania, mwaka 1995 serikali ya China iliamua kupeleka kikundi cha wataalamu kusaidia viongozi wa kiwanda cha nguo cha Urafiki kufanya mageuzi ya utaratibu. Badala ya kufuata mtindo ule wa zamani wa kutoa msaada wa kiuchumi, serikali ya China iliamua kufuata njia ya ubia kati ya pande hizo mbili na kubadilisha jina la kiwanda cha nguo cha Urafiki kuwa kiwanda cha ubia, ambayo upande wa China unamiliki wingi wa hisa za kampuni hiyo. Kiwanda cha nguo cha Urafiki kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Tanzania na China kilianzishwa rasmi tarehe 2 mwezi Okatoba mwaka 1996, na ilianza shughuli zake za biashara tarehe 1 mwezi Aprili katika mwaka uliofuata.
Injinia mkuu wa kiwanda hicho Bw. Yao Juan alisema, kiwanda kilianza kazi upya baada ya kuasisiwa kampuni ya nguo kutokana na mikopo nafuu ya serikali ya China.
"Fungu la kwanza la mkopo wa Yuan za Renminbi milioni 100 lilitumika katika kuanzisha upya kazi za uzalishaji mali za kiwanda, na fungu la pili la Yuan milioni 135 lilitumika kwa marekebisho ya teknolojia. Hususani marekebisho ya matumizi ya nishati, maji, hewa moto na umeme, kisha kwa karakana ya utiaji rangi vitambaa na ufumaji wa nguo."
Baada ya kuboresha usimamizi wa kazi, uzalishaji mali, udhibiti wa matumizi na marekebisho ya teknolojia, kiwanda cha nguo kilikuwa na nguvu tena, na kilipata faida katika mwaka wa kwanza, pato la kiwanda lilikuwa karibu Shilingi za Tanzania bilioni 1, kiasi hicho ni kama dola za kimarekani laki moja na elfu 50, na kuwa moja ya kampuni kumi zilizochukua nafasi za kwanza kwa ulipaji kodi nchini Tanzania. Kustawi kwa kampuni ya nguo ya Urafiki kulistawisha sekta nzima ya nguo ya Tanzania.
Meneja mkuu wa kiwanda hicho Bw. Yu Kaiming alisema, mwezi May mwaka 1998, rais wa zamani wa Tanzania Bw. Benjamin William Mkapa aliwakaribisha yeye na balozi wa China nchini Tanzania kwenda kula chakula cha jioni Ikulu, ambapo waziri wa viwanda na biashara wa wakati huo Bw. William Shija alipongeza mafanikio ya ushirikiano wa Tanzania na China, alisema, kiwanda cha nguo cha Urafiki ni mfano wa urafiki kati ya nchi hizo mbili, na alitumaini serikali ya China kuanzisha miradi kadhaa mingine kama ya kiwanda cha nguo cha Urafiki.
|