Waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao tarehe 23 asubuhi akiambatana na waziri mkuu wa Tanzania Edward Lowassa alikwenda mahsusi kwenye makaburi wa wataalamu wa China waliojitolea muhanga nchini Tanzania yaliyoko kwenye kitongoji cha Dar es Salaam, mji mkuu wa Tanzania, halafu alikwenda kukagua mahali unapojengwa Uwanja wa michezo wa taifa wa Tanzania unaojengwa kwa msaada wa serikali ya China, na kuwapa pole mafundi na wahandisi wa China na Tanzania.
Akiambatana na waziri mkuu wa Tanzania Bwana Lowassa, waziri mkuu Wen Jiabao aliweka shada la maua mbele ya "Makaburi ya wataalamu wa China waliojitolea muhanga", ambapo alitoa hotuba akisema:
Miaka 30 iliyopita, watu wengi hodari wa China walitumwa na serikali kuja barani Afrika ambako ni mbali sana na nyumbani kwao China, wakishirikiana na wananchi wa Tanzania na Zambia walishinda taabu nyingi kubwa katika ujenzi wa reli ya TAZARA, lakini baadhi ya watu hao walijitolea muhanga na kulala daima kwenye ardhi hiyo iliyoko mbali sana na nyumbani kwao. Tumekuja hapa tunaweka maua kwenye makaburi yao kwa kueleza hisia zetu nyingi za kuwakumbuka.
Waziri mkuu Wen Jiabao alisema, siku nenda siku rudi, wenzao wa taifa la China na wananchi wa Tanzania na Zambia siku zote wanawakumbuka watu hao waliojitolea muhanga kwa ajili ya urafiki kati ya China na Afrika.
Waziri mkuu wa Tanzania Bwana Lowassa pia alieleza heshima na hisia zake za kuwakumbuka watu waliojitolea muhanga kwa ajili ya kujenga Reli ya TAZARA, alisema:
Mchango wa wachina hao umesukuma mbele sana maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Zambia, pia umesukuma mbele maendeleo ya sehemu za katikati na kusini mwa Afrika. Umuhimu wa reli hiyo umezidi ule wa reli ya kawaida, hii ni "reli yetu", ingawa ilijengwa kwa msaada wa wachina, lakini wachina walipotusaidia kuijenga, hawakuichukulia kuwa ni reli ya China.
Kwenye makaburi hayo wamezikwa wataalamu, mafundi na wafanyakazi wapatao 69 wa China waliojitolea muhanga kwa ajili ya ujenzi wa taifa la Tanzania, 47 miongoni mwao walijitolea muhanga katika ujenzi wa reli ya TAZARA. Reli ya TAZARA ni reli inayounganisha Afrika ya mashariki na Afrika ya kusini na kati, huu ni mojawapo kati ya miradi mikubwa zaidi ya seti nzima iliyojengwa kwa msaada wa China katika nchi za nje.
Baadaye waziri mkuu Wen Jiabao alikagua mahali pa kufanyia ujenzi wa Uwanja wa michezo wa taifa wa Tanzania unaojengwa kwa msaada wa China. Uwanja huo ni mradi mkubwa ambao unajengwa kwa ushirikiano kati ya serikali za China na Tanzania, uwanja huo wa michezo utakuwa na viti elfu 60 vya watazamaji, unajengwa kuanzia mwaka 2005, na unatazamiwa kukamilika mwezi Januari mwaka 2007. Waziri mkuu Wen Jiabao aliwapa pole wahandisi na mafundi wa China na Tanzania kwenye mahali hapo, alisema:
Uwanja wa michezo wa taifa wa Tanzania ni mradi mkubwa mwingine wa ushirikiano kati ya China na Tanzania, pia ni mradi wa alama ya msaada wa China kwa Tanzania. Wahandisi, mafundi na wafanyakazi wa China na Tanzania wanafanya ujenzi kwa pamoja na kutoa nguvu kubwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa uwanja huo kwa mpango uliowekwa na kuhakikisha sifa ya mradi.
Wahandisi na mafundi wa China walimwahidi Waziri Mkuu kuwa, watafanya juhudi kubwa kadiri wawezavyo ili kukamilisha vizuri ujenzi wa uwanja huo kwa wakati, na kuchangia zaidi urafiki kati ya China na Tanzania.
Idhaa ya Kiswahili 2006-06-24
|