Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-26 14:58:18    
Vichochoro mjini Beijing

cri

Mjini Beijing kuna msemo unaosema kuwa, "Huwezi kuijua Beijing bila kuingia kwenye vichochoro mjini humo, na utasikitika sana kama utashindwa kutembelea vichochoro mjini Beijing." Mjini Beijing vichochoro vikubwa na vidogo vinapitana na kutapakaa kote mjini kama mishipa ya mwilini mwa binadamu ilivyo, vichochoro vya Beijing ni moja ya mitindo ya ujenzi wa majengo mjini Beijing. Watalii kutoka nje wakitaka kujionea vilivyo utamaduni wa kale na harufu nzito ya maisha mjini Beijing, wanapaswa kutembelea kwenye vichochoro mjini Beijing.

Inasemekana kuwa vichochoro mjini Beijing vilijengwa kuanzia karne ya 13 baada ya Beijing kuamuliwa kuwa mji mkuu wa Enzi ya Yuan, watawala wa enzi hiyo walikuwa watu wa kabila la wamongolia, Hutong yaani vichochoro, neno hili lilitokana na lugha ya kimongolia, katika lugha ya kimongolia, Huto, maana yake ni kisima cha maji, na vichochoro vya Beijing vilivyojengwa mwanzoni vilitapakaa kutokana na sehemu zenye visima vya maji, kwani watu wa wakati huo waliona kuwa lazima kuhakikisha kila kichochoro inakuwa na kisima cha maji. Baada ya kupita mabadiliko na maendeleo katika miaka mia kadhaa iliyopita, Hutong yaani kichochoro kimekuwa neno la ujenzi wa njia nyembamba mijini katika sehemu ya kaskazini nchini China. Vichochoro vya Beijing vingi vinaelekea mashariki kutoka magharibi, kwa kawaida upana wa kichochoro hauzidi mita 9. Zamani majengo yaliyoko kando mbili za vichochoro takribani yote ni majengo ya makazi ya "Siheyuan" yaani jengo moja moja lenye vyumba kwa pande nne, na katikati ya jengo ni ua, hayo ni makazi ya raia ya Beijing yenye mtindo pekee.

Wakazi waliokaa kwa miaka mingi kwenye vichochoro mjini humo, wakisikia sauti kama hiyo, wanajua mara moja mwuzaji wa vitu gani amekuja. Zamani sauti hiyo ilikuwa inasikika kila siku hata kila majira katika vichochoro mjini Beijing, wafanya biashara wa rejareja waliuza vitu mbele ya nyumba za wakazi. Tunaweza kusema, vichochoro si kama tu vilikuwa njia ya kupita kwa wakazi wa kawaida wa Beijing, bali pia vilionesha desturi na mila za maisha ya wakazi wa mji huo.

Vichochoro mjini Beijing ni vingi na hata havihesabiki. Kuna msemo unaosema, "vichochoro maarufu vilifikia 360, na vichochoro vya kawaida ni vingi kama manyoya ya ng'ombe." Majengo yaliyoko kando mbili za vichochoro mjini Beijing yanaonekana kuwa yote ni ya rangi ya kijivu, toka paa hadi kuta, yote yanafanana na hayana umaalum pekee kwa kila moja. Lakini hali halisi ni kuwa, kila kichochoro kina hadithi yake. Mtaalamu wa utafiti wa desturi na mila Bwana Li Mingde alisema, jina maalum la kila kichochoro mjini Beijing linaonesha wazi maisha ya wakazi wa kichochoro hicho katika miaka mingi iliyopita, hata baadhi ya majina ya vichochoro yameonesha matarajio ya wakazi. Bwana Li alisema:

Kichochoro kimoja chenye jina la "Baihuashengchu", maana yake ya kichina ni kichochoro kilichoko ndani ya maua mengi ya aina mbalimbali", jina hili linapendeza. Na vichochoro vingine vilipewa majina ya watu fulani maarufu waliowahi kuishi kwenye vichochoro hivyo.

Bwana Li alituambia kuwa kuna kichochoro kimoja ambacho umbo lake ni kama mwanzi, hivyo ulipewa jina la Zhugan?maana yake ya kichina ni mwanzi; kichochoro kingine kinachoitwa Yudai, maana yake ni ukanda wa jade ambayo yalivaliwa na maofisa wa kasri ya ufalme katika zama za kale, kwani umbo wa kichochoro hicho kinafanana na ukanda huo; na jina la kichochoro kingine linaloitwa Yandaixiejie, maana yake ya kichina ni kichochoro cha mikoba ya tumbaku, kwani zamani kichochoro hicho kilikuwa sehemu ya uuzaji wa mikoba ya kutia tumbaku.

Hivi sasa vichochoro mjini Beijing vimekuwa msingi wa utamaduni wa Beijing, mvuto wake pekee unaowapendeza sana watalii kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje. Mchoraji maarufu wa michoro ya kichina anayejua sana kuchora picha za vichochoro Bwana Kuang Han alisema, alizaliwa na kukua katika sehemu ya kusini ya China, lakini alipoanza kuishi mjini Beijing alivutiwa sana na vichochoro mjini Beijing. Alisema:

Vichochoro mjini Beijing vyenyewe ni sanaa ya aina moja, ambavyo vimepita karne kadhaa, na vinafanana na wazee wenye mikunjo mingi waliopitwa na mabadiliko ya jamii kwa miaka mingi.

Vichochoro vilivyoko karibu na sehemu ya Shichahai mjini Beijing vinawavutia zaidi watalii. Sehemu ya Shichahai iko kwenye kiini cha mji wa Beijing, Sehemu hiyo inaundwa na maziwa matatu ya Qianhai, Houhai na Xihai, kwenye sehemu ya makutano ya Ziwa Qianhai na Ziwa Houhai kuna daraja moja la mawe lenye umbo la tao, daraja hilo dogo linapendeza sana, mandhari ya pembezoni mwake ni nzuri kweli.

Kupanda daraja hilo kwa kutazama sehemu ya mbali ni jambo la kujistarehesha sana, katika siku yenye anga buluu, ukipanda daraja hilo utaona pia sura ya milima iliyoko mbali, hakika utafurahi. Katika sehemu zilizoko pembezoni mwa Shichahai, kuna vichochoro vingi vilivyobaki na kuhifadhiwa kikamilifu, pamoja na nyumba nyingi za Siheyuan, pia kuna mabustani kadhaa ya watu binafsi wa zama za kale, kama vile Gongwangfu, sehemu hizo zinastahili kutembelewa na watu.

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo ya ujenzi wa mji, majumba makubwa yenye ghorofa nyingi yameongezeka zaidi mjini Beijing, ambapo vichochoro vinapungua siku hadi siku. Hivi sasa serikali ya mji wa Beijing inapanga mpango wa kuhifadhi vichochoro kadha wa kadha vyenye mitindo ya kipekee. Ili kuwawezesha watalii waelewe maisha ya wakazi walioishi kwa miaka mingi mjini Beijing, Idara ya utalii ya Beijing pia imeanzisha "utalii vichochoroni", ambapo watalii wanaweza kupanda magari yenye magurudumu matatu yanayoendeshwa na watu kwenda vichochoroni kutembelea, ama kwenda kwenye makazi ya Siheyuan kunywa chai nyumbani kwa wakazi, ambapo wenyeji wa nyumba wanaweza kuwaelezea hadithi juu ya Beijing au maisha ya wakazi wa Beijing.

Bwana Gybter Wein kutoka Ujerumani alisema, mtalii akipanda gari lenye magurudumu matatu linaloendeshwa na mtu ni rahisi kwake kutembelea vichochoroni mjini Beijing. Alisema:

Nilipokuwa India niliwahi kuona gari linalofafana na magari hayo mjini Beijing, magari hayo yenye magurudumu matatu kweli ni mazuri yanayofaa kwenda kwenye kila pembe vichochoroni, kwani gari la taxi haliwezi kuingia kwenye vichochoro mjini Beijing. Vichochoro ni umaalum wa Beijing, vikilinganishwa na majumba marefu makubwa na sehemu zenye maduka mengi, ninapenda zaidi vichochoro mjini Beijing.

Kupanda magari yenye magurudumu matatu yanayoendeshwa na watu kutembelea vichochoro mjini Beijing ni shughuli moja inayopendwa sana na watalii kutoka nchi za nje na sehemu nyingine nchini China.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-26