Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-26 16:48:12    
Tuimarishe mapambano dhidi ya dawa za kulevya

cri

Tarehe 26 mwezi Juni ni "siku ya kupiga marufuku dawa za kulevya duniani". Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku hiyo mwaka huu ni "dawa za kulevya si mchezo wa watoto". "Taarifa ya kupiga marufuku dawa za kulevya duniani mwaka 2005" iliyotolewa na ofisi ya udhibiti wa dawa za kulevya na uvunjaji sheria ya Umoja wa Mataifa inasema, thamani ya biashara ya rejareja ya dawa za kulevya duniani imefikia dola za kimarekani bilioni 322, zikiwa ni 0.9% ya jumla ya mapato ya nchi mbalimbali duniani. Katika mwaka uliopita kulikuwa na watu milioni 200 duniani kwa uchache kabisa waliotumia mara moja dawa za kulevya. Hali ya kupiga marufuku matumizi ya dawa za kulevya bado ina shida nyingi.

Tokea miaka ya 60 ya karne iliyopita, dawa za kulevya zilianza kuenezwa kwa mfululizo duniani. Licha ya dawa za kulevya kudhuru moja kwa moja afya za watu na kuleta tishio kubwa kwa maendeleo ya uchumi, dawa hizo pia zimeongeza matatizo kwa jamii ikiwa ni pamoja na vitendo vya utapeli, matumizi ya mabavu na maambukizi ya Ukimwi. Aidha suala la dawa za kulevya linahusiana na vitendo vya hatia vya makundi ya kimataifa ya kigaidi, kuingiza fedha haramu katika mzunguko wa fedha na biashara ya watu. Takwimu husika zinaonesha kuwa, kila mwaka kuna watu kiasi cha laki 2 wanaokufa kutokana na matumizi ya ovyo ya dawa za kulevya, wakati watu zaidi ya milioni 10 wanapoteza nguvu ya kufanya kazi. Hivi sasa biashara ya dawa za kulevya inahusiana na nchi na sehemu zaidi ya 170, na karibu hakuna hata nchi moja inayoweza kujiepusha na janga hilo.

Mwezi Juni mwaka 1987, umoja wa Mataifa uliitisha mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi yasiyo mwafaka ya dawa za kulevya na biashara ya magendo ya dawa hizo, ambapo ulitolewa wito wa "kuthamini uhai, kutotumia dawa za kulevya!", na kushauri tarehe 26 mwezi Juni wa kila mwaka iwe "siku ya kupiga marufuku matumizi ya dawa za kulevya duniani" ili kufanya suala la dawa za kulevya lifuatiliwe na nchi mbalimbali duniani na kuzuia madhara ya madawa ya kulevya. Mwezi Desemba mwaka huo huo baraza kuu la 42 la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio na kuthibitisha rasmi siku hiyo iwe "siku ya kupiga marufuku dawa za kulevya duniani". Na tokea mwaka 1992, harakati za kuadhimisha "siku ya kupiga marufuku dawa za kulevya duniani" hutoa Kaulimbiu mpya kila mwaka.

Katika miaka mingi iliyopita jumuiya ya kimataifa ilijitahidi kadiri iwezavyo kuzuia kuenea kwa matumizi ya dawa za kulevya na kupiga hatua kubwa. Hususan ni kuwa nchi mbalimbali zilikuwa na maoni ya namna moja katika kuanzisha ushirikiano wa kimataifa, hasa ushirikiano kati ya nchi zinazozalisha dawa za kulevya na nchi zinazotumia dawa za kulevya. Duniani nchi zinazozalisha dawa za kulevya ni nchi zinazoendelea, na nchi nyingi zaidi zinazotumia dawa za kulevya ni nchi zilizoendelea. Hivyo pande hizo mbili zinatakiwa kujitahidi kukomesha uzalishaji wa dawa za kulevya au matumizi ya dawa za kulevya. Katika miaka mingi iliyopita nchi mbalimbali ziliimarisha ushirikiano wa kuzuia dawa za kulevya kwa kusaini mikataba ya pande mbili, ya pande nyingi na ya kikanda, na zilipata mafanikio mengi makubwa katika kuwakamata wahalifu wa biashara ya dawa za kulevya kwa ushirikiano wa idara za kisheria.

China siku zote inazingatia sana kuzuia dawa za kulevya. Katika miaka ya karibuni China ilianzisha "vita ya umma" katika kuzuia kuenea kwa dawa za kulevya, kuvunjilia mbali vyanzo na usafirishaji wa dawa za kulevya, kutoa pigo kubwa kwa wahalifu wa dawa ya kulevya na kuzuia ongezeko la watu wanaoanza kutumia dawa za kulevya. Aidha China inashiriki kwenye shughuli za kimataifa za kuzuia kuenea kwa dawa za kulevya, ukiwemo ushirikiano dhidi ya dawa za kulevya zinazotoka katika sehemu za mpakani kati ya nchi tatu za China, Laos na Myanmar na sehemu ya mpaka kati ya Pakistan na Afghanistan.

Hata hivyo tatizo la dawa za kulevya bado ni janga kubwa duniani kwa hivi sasa, hivyo nchi zote duniani zinatakiwa kuendelea kushirikiana ili kuzuia madhara dhidi ya dawa za kulevya. Mwaka huu Umoja wa Mataifa umetoa Kaulimbiu ya "dawa ya kulevya si mchezo wa watoto", ukiitaka jumuiya ya kimataifa izingatie kutoa elimu ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya kwa watoto ili kutoa mazingira bora kwa watoto.