Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-27 16:40:07    
Vijiji mkoani Jiangsu vyapiga hatua kubwa ya maendeleo

cri

China ni nchi yenye wakulima wengi, na maendeleo ya uchumi na jamii ya sehemu za vijijini yako nyuma sana ikilinganishwa na mijini. Ili kubadilisha hali hiyo, serikali ya China imenuia kuharakisha hatua za ujenzi wa sehemu ya vijiji katika miaka 5 ijayo. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alipofanya mahojiano katika mkoa wa Jiangsu, ulioko kwenye sehemu ya mashariki ya China, alifahamishwa kuwa sehemu za vijijini za huko zimejifunga kibwebwe kuharakisha maendeleo ya sehemu za vijijini kwa kuanzisha maeneo ya ustawishaji na kuharakisha ujenzi wa miji midogo.

Kwanza kabisa tulitembelea wilaya ya Guannan iliyoko kaskazini mwa mkoa wa Jiangsu. Wilaya hiyo iko kwenye eneo tambarare, ni wilaya ya majaribio ya taifa ya mazingira ya kutegemeana kwa viumbe na pia kituo cha uzalishaji wa pamba bora nchini China, hata hivyo maendeleo ya uchumi ya huko bado ni yanakwenda polepole sana. Ofisa husika wa huko Bw. Sun Ming alisema, wazo la jadi la kuweka kipaumbele katika kilimo na kudharau shughuli za biashara ni kitu muhimu kinachokwamisha maendeleo ya uchumi ya huko.

"Tokea muda mrefu uliopita uchumi wa wilaya ya Guannan ulikuwa nyuma. Mwaka 2002, wilaya ya Guannan ilichukua nafasi ya mwisho katika kutumia mitaji ya kigeni, wastani wa pato la mkulima na wastani wa mshahara wa mfanyakazi."

Watu wanatafuta mabadiliko, na mto Guan unaopita kwenye wilaya ya Guannan sasa umekuwa ni rasilimali inayotumika. Maji ya mto huo ni mengi, hivyo ni bora kwa uchukuzi wa majini, tena mto huo unaungana na pwani yenye umbali wa kilomita zaidi ya 160 pamoja na magati mengi yenye kina kirefu cha maji. Hivyo serikali ya huko ikaamua kuanzisha eneo la ustawishaji wa uchumi kwa kutumia ubora wa njia ya usafirishaji na gharama ndogo ya nguvukazi.

Eneo la ustawishaji limevutia viwanda, kampuni na mitaji mingi, kuinua kiwango cha uchumi na maisha ya watu wa huko, na kubadilisha hatua kwa hatua wazo la jadi la watu wa Guannan kupuuza shughuli za kibiashara. Wakulima wengi wa huko wamezoea kwenda kufanya vibarua katika viwanda katika nyakati zisizo na shughuli nyingi za kilimo.

Katika kiwanda kimoja cha nguo wilayani Guannan, mwandishi wetu wa habari aliwaona wafanyakazi wakichapa kazi kwa bidii. Kiwanda hicho kinatengeneza nguo za oda za wafanyabiashara wa nchi za nje. Mfanyakazi bibi Xiao Hongxia alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, miaka mitatu iliyopita alikuwa anafanya vibarua nchini Japan, hivi sasa amerejea kwao na kuwa mmoja wa viongozi wa vikundi vya wafanyakazi wa karakana ya kiwanda. Ingawa anafanya kazi ileile ya zamani, na pato lake si kubwa kuliko lile alilopata nchini Japan, lakini anaipenda sana kazi yake hiyo

"Ni dhahiri kwamba mshahara wa nchi ya nje ni mkubwa, lakini huko kulikuwa na kipingamizi cha lugha, nilitarajia kurejea nyumbani haraka baada ya kupata fedha. Baada ya kurejea nyumbani, naona usimamizi wa kiwanda cha nguo umekuwa mzuri sana kuliko ule wa zamani. Hapo awali tuliweza kupiga soga wakati wa kufanya kazi, lakini hivi sasa karibu ni sawa na katika kiwanda cha Japan, karibu hakuna watu wanaozungumza au kuzunguka-zunguka sehemu nyingine."

Baada ya ujenzi katika miaka kadhaa iliyopita, Guannan imekuwa na eneo la ustawishaji la mjini pamoja na maeneo ya ustawishaji wa uchumi ya kando za mto na ya pwani.

Wasikilizaji wapendwa, wilaya ya Guannan ninayowasimulia ni mfano mmoja tu wa maendeleo ya sehemu ya vijiji ya mkoa wa Jiangsu. Mkoa wa Jiangsu uko kwenye sehemu ya mashariki ya China, na ni moja ya sehemu zilizoendelea sana za vijijini. Mazingira ya kijiografia ya huko ni bora, kuna mito na bandari nyingi pamoja na urahisi wa mawasiliano, hivyo kutumia vilivyo rasilimali na nguvukazi tele za huko ni njia muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa sehemu za vijijini za huko.

Eneo la ustawishaji la viwanda la Suzhou mkoani Jiangsu ni mradi wa ushirikiano wa kimataifa uliotiwa saini na serikali za nchi mbili za China na Singapore, ambao sekta muhimu ni mawasiliano ya habari ya elektroniki, mitambo ya hali ya juu, madawa ya viumbe na aina mpya ya vifaa vya ujenzi. Naibu mkurugenzi wa ofisi ya kamati ya usimamizi ya eneo la ustawishaji la viwanda la Suzhou bibi Yao Wenlai alisema, wakati walipojenga eneo la viwanda walishawishi marekebisho ya muundo wa viwanda vidogo vya tarafa za vilivyoko pembezoni mwa Suzhou ili kuhimiza maendeleo ya miji midogo ya sehemu za vijijini.

"Hivi sasa 90% ya wakulima wamehamia katika makazi ya kisasa. Wakulima wazee wanapewa kiinua mgongo na serikali, na vijana wanafanya kazi katika viwanda baada ya kufaulu mafunzo yao. Licha ya hayo tunawasaidia katika kuwahamisha katika makazi mapya na kuwapatia dhamana ya jamii, hivi sasa serikali inatenga fedha kila mwaka kuwasaidia wakulima maskini ili kupunguza tatizo la umaskini kwa wakulima."

Idara ya usimamizi ya eneo la viwanda la Suzhou inaongeza nafasi za ajira kwa wakulima zikiwa ni pamoja na utunzaji wa miti na majani, kutunza usafi wa mazingira, ulinzi wa usalama na huduma za familia, tena inawahimiza wakulima wajiajiri katika shughuli za biashara.

Kitu kinachovutia zaidi ni kuwa kwa kufikiria kutumiwa kwa mashamba ya wakulima wakati wa kuanzisha eneo la ustawishaji wa viwanda, serikali ya huko inatoa fidia kila mwaka kwa wakulima kwa kiasi cha 10% ya pato la wakulima katika miaka mitatu ya mwisho katika shughuli za kilimo; inatoa uhakikisho wa kimsingi kwa maisha ya vijana wenye umri chini ya miaka 18; na kutoa dhamana ya maisha kwa wazee wanaume waliotimiza umri wa miaka 60 na wazee wanawake waliotimiza umri wa miaka 55. Aidha, serikali ya huko inatoa mafunzo ya kazi kwa wakulima ili kukuza uwezo wa wakulima kufanya kazi viwandani.

Sehemu mbili zilizotajwa hapo awali zilihimiza maendeleo kwa kuwapeleka wakulima wao viwandani. Lakini kijiji cha Huaxi kilichoko sehemu ya kusini ya mkoa wa Jiangsu kilihimiza maendeleo yao kwa kuchukulia kijiji kizima kuwa kampuni moja kubwa, hususan shughuli za uzalishaji wa vitambaa vya sufu, ushonaji wa nguo na ufumaji wa nguo za ndani, kijiji hicho kimeendeleza masoko na kupata wateja wa kudumu kwa kutegemea ubora wa wingi wa viwanda vya nguo vilivyoko kwenye delta ya mto Changjiang. Ofisa wa huko Bw. Sun Haiyan alisema,

"Baada ya kutenganisha utawala wa kijiji na shughuli za uendeshaji wa viwanda. Uchumi unasimamiwa kwa utaratibu mwafaka na makada wanapangwa kwa mpango mmoja, katika mazingira ya namna moja nguvukazi, huduma za umma na ujenzi wa kijiji vinapangwa kwa mpango mmoja."

Hivi sasa kijiji cha Huaxi kimeanzisha kampuni kuu ya kijiji cha Huaxi, ambayo imekuwa na kampuni 9 zilizo chini yake pamoja na viwanda zaidi ya 60, ambavyo pato lake limefikia Yuan za Renminbi zaidi ya bilioni 30.

Idhaa ya kiswahili 2006-06-27