Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-27 18:33:48    
Mjumbe maalum wa China asisitiza kuwa mgogoro kati ya waarabu na Israel utatuliwe kwa njia ya mazungumzo ya amani

cri

Mjumbe maalum wa China anayeshughulikia suala la mashariki ya kati ambaye yuko ziarani Misri Bwana Sun Bigan tarehe 26 alisisitiza huko Cairo kuwa, serikali ya China siku zote inatetea kutatua kisiasa mgogoro kati ya Waarabu na Israel kwa njia ya mazungumzo ya amani.

Siku hiyo asubuhi huko Cairo, Bwana Sun Bigan kwa nyakati tofauti alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Misri Ahmed Abul Gheit, mshauri wa rais kuhusu mambo ya siasa Bwana Osama el Baz na naibu katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu anayeshughulikia mambo ya siasa Bwana Ahemd Bin Helli, ambapo walibadilishana maoni kuhusu hali ya sehemu ya mashariki ya kati, na Bwana Sun Bigan alifafanua msimamo wa kikanuni na mapendekezo ya serikali ya China kuhusu suala la mashariki ya kati.

Bwana Sun Bigan alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema:

Jukumu langu kuu la ziara hiyo ya mashariki ya kati ni kufahamishwa hali halisi ya sehemu hiyo na kujua hali ilivyo ya sasa ya mgogoro kati ya nchi za kiarabu na Israel. Aidha nataka kukutana na kufahamiana na maofisa wa nchi husika wanaoshughulikia suala la mashariki ya kati ili kujenga uhusiano mzuri wa kikazi nao. Zaidi ya hayo nilipokutana na maofisa wanaohusika nilifafanua msimamo wa kikanuni na mapendekezo ya serikali ya China kuhusu suala la mashariki ya kati, kusikiliza kwa makini ujulisho wao kuhusu hali ya mashariki ya kati na maoni na mapendekezo yao kuhusu suala hilo, na kubadilishana nao maoni.

Bwana Sun Bigan alichambua matatizo makubwa yaliyoko hivi sasa kwenye suala la mashariki ya kati, alisema:

Suala la Palestina ni tatizo kuu lililoko katika utatuzi wa suala la mashariki ya kati, kama suala la Palestina halitaweza kutatuliwa kwa haki na kwa njia halali, basi amani haiwezi kupatikana, hivyo naona sasa bado utatuzi wa suala la mashariki ya kati uko mbali, lakini kama pande mbili zinazogongana zote zina matumaini ya kupata amani na maendeleo ya sehemu hiyo na wananchi wake, zikishirikiana na jumuiya ya kimataifa, naona amani itaweza kupatikana.

Bwana Sun Bigan alifika Cairo tarehe 25 kuanzia ziara yake nchini Misri, baadaye atafanya ziara nchini Jordan, Israel na Palestina. Akiwa mjumbe mpya maalum wa China wa kushughulikia suala la mashariki ya kati, ni kwa nini amechagua Misri kuwa kituo chake cha kwanza katika ziara hiyo ya mashariki ya kati? Bwana Sun akifafanua alisema:

Misri ni nchi muhimu sana ya kiarabu, ambayo imeonesha na inaendelea kuonesha umuhimu wake kwa amani ya mashariki ya kati. Ndiyo maana nimefika Misri kuanza kutaka kusikiliza maoni ya serikali ya Misri na kufanya mashauriano nayo. Aidha, China na Misri zina maoni mengi ya pamoja kuhusu utatuzi wa suala la mashariki ya kati, tukibadilishana zaidi maoni na mapendekezo, itatusaidia tufanye juhudi kwa pamoja ili kuhimiza mazungumzo ya amani.

Bwana Sun alipozungumzia hali ya hivi sasa kati ya Palestina na Israel alisema, hali ya hivi sasa ya sehemu ya mashariki ya kati bado ina utatanishi mkubwa, na maendeleo ya baadhi ya hali ya mambo yanawafanya watu wawe na wasiwasi. Alisema tuna matumaini ya dhati kuwa pande zinazohusika zitaweza kuzingatia maslahi ya wananchi wao, ziwe na matumaini ya kutimiza amani ya kikanda, kujenga mazingira mwafaka ili kurudisha mazungumzo ya amani mapema iwezekanavyo. Ndiyo maana pande zinazohusika zinapaswa kuchukua kwanza hatua kuzuia hali ya mambo isizidi kuwa mbaya, kisha kufanya mazungumzo ya amani na kutatua mgogoro kwa njia ya kisiasa. Bwana Sun Bigan alisema, suala lolote linapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo ya amani, hatua ya upande mmoja haitasaidia utatuzi wa suala.

Alisisitiza kuwa serikali ya China inashikilia kanuni za kimsingi, msimamo na mapendekezo wazi siku zote, China ina matumaini ya dhati kuwa sehemu ya mashariki ya kati itatimiza amani ya haki na ya kudumu.

Idhaa ya Kiswahili 2006-06-27