Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-29 16:13:56    
Reli ya Qinghai-Tibet yazungumziwa sana na wakazi wa Tibet

cri

Katika mkahawa wa chai uliopo kando ya barabara ya Jiangsu, mjini Lahsa, ambao ni mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa Tibet, China, wanandugu watano walikuwa wamekaa kwenye meza moja, wakinywa chai huku wakizungumza, ambapo kitu kilichotajwa mara kwa mara kwenye mazungumzo yao ni reli ya Qinghai-Tibet. Reli hiyo itakayoanza kutumika rasmi tarehe mosi, Julai mwaka huu itamaliza historia ya mkoa wa Tibet kutokuwa na usafiri wa reli.

Imefahamika kuwa hapo awali, mambo waliyozungumzia mara kwa mara wakazi wa mkoa wa Tibet yalikuwa magari binafsi, simu za mkononi na mtandao wa Internet.

Kabla ya kufunga safari ya kuelekea Namucuo, mkoani Tibet, mzee Cidan Wangmu wa kabila la Watibet alisisimka sana alipozungumzia reli ya Qinghai-Tibet. Ili kupata nafasi ya kutazama garimoshi, mzee huyo mwenye umri wa miaka 61 na wenzake wanane waliamua njiani kurudi kutoka Namucuo, na kwenda mahali ambapo garimoshi linapita.

Hivi sasa wakulima na wafugaji wanaoishi kando ya reli hiyo wanazungumza sana jinsi watakavyoongeza mapato yao baada ya reli hiyo kuanza kutumika rasmi. Baadhi yao wana mipango ya kuanzisha maduka madogo karibu na vituo vya reli, na wengine wanajadiliana kuzibadilisha nyumba zao kuwa hoteli za kuwapokea watalii.

Idara za serikali pia zinajadili na kutafiti namna ya kuiendeleza jamii na uchumi wa Tibet katika enzi mpya ambayo mkoa huo utaunganishwa na sehemu nyingine kwa reli kwa mara ya kwanza katika historia yake. Reli ya Qinghai-Tibet imetajwa kwenye mikutano mbalimbali na kuchapishwa katika nyaraka mbalimbali za serikali.

Idara ya kuzima moto imetunga mipango ya kukabiliana na hali ya uwezekano wa kutokea kwa matukio mengi ya hatari mkoani Tibet baada ya kuzinduliwa kwa reli. Idara inayoshughulikia hifadhi ya mabaki ya kale inatafiti hatua za kulinda mabaki ya kale yaliyomo ndani ya mahekalu sambamba na kuendeleza shughuli za utalii. Na idara ya utalii inasubiri kwa hamu siku ya kuanza kutumika rasmi kwa reli hiyo, ambayo hakika itahimiza sana sekta ya utalii mkoani Tibet.

Lakini pia kuna watu kadhaa ambao wana wasiwasi kuhusu ushindani mkubwa utakaoletwa na kuanza kutumika rasmi kwa reli hiyo. Bw. Zhao Caifei amefanya biashara ya nguo kwa miaka karibu 20 mjini Lahsa. Alisema biashara yake ilikuwa ni nzuri hapo awali, lakini wafanyabiashara wengi zaidi wataweza kusafirisha nguo kutoka sehemu nyingine nchini China kwa garimoshi, kwa hiyo itakuwa si rahisi kwake kupata faida kubwa.

Hata hivyo sio wafanyabiashara wote wana wasiwasi kama Bw. Zhao. Meneja mkuu wa kampuni ya mitambo ya kilimo ya mji wa Rikaze, mkoani Tibet Bw. Dola, ana imani kubwa na soko la Tibet baada ya kuanza kutumika rasmi kwa reli ya Qinghai-Tibet. Amefanya mikutano kadhaa na maofisa wengine wa kampuni yake, wakijadiliana mbinu za kukabiliana na hali mpya kwenye soko la Tibet baada ya reli hiyo kuanza kazi rasmi. Bw. Dola alisema, "Kutumika rasmi kwa reli kati ya Qinghai na Tibet kutaleta athari kubwa sana kwa soko mkoani Tibet. Mbinu za kukabiliana na hali mpya sokoni huenda zitakuwa jambo muhimu litakaloamua hatma ya viwanda na kampuni nyingi."

Idhaa ya kiswahili 2006-06-29