Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-29 16:11:14    
Serikali ya China yasaidia makabila madogo yenye watu wachache

cri
China ni nchi yenye makabila mengi. Mbali na kabila la Wahan, kuna makabila mengine 55 madogomadogo, na miongoni mwa makabila hayo, 22 yana idadi ya watu isiyozidi laki moja kwa kila moja, kwa hiyo yanaitwa makabila madogo yenye watu wachache. Kwa sababu watu wa makabila hayo wanaishi katika maeneo yaliyopo mbali na miji, wana hali duni ya maendeleo kwa ujumla. Tokea mwishoni mwa karne iliyopita, hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuharakisha maendeleo ya watu wa makabila madogo hayo yenye watu wachache.

Hivi karibuni waandishi wa habari wa Radio China Kimataifa walikwenda sehemu za kusini magharibi na kaskazini mashariki mwa China wanakoishi watu wengi wa makabila hayo, na kushuhudia maisha ya watu hao.

Watu wa kabila la Wanu wanaishi katika mkoa wa Yunnan, kusini magharibi mwa China. Katika mji mkuu wa mkoa huo Kunming, mwandishi wetu wa habari alipanda gari kuelekea Gongshan, wanakoishi watu wengi wa kabila la Wanu. Safari hiyo ilichukua takriban saa 18 kabla ya kuwasili kwenye mji huo, baadaye mwandishi wetu wa habari alitembea kwa miguu kwa zaidi ya saa moja na kufika kwenye kijiji cha kabila la Wanu kiitwacho Jiasheng. Kwa kuangalia kutoka mbali, kijiji hicho kimezungukwa na milima yenye theluji. Ndani ya kijiji hicho, nyumba mpya za matofali zimepangwa vizuri kando ya barabara pana. Picha hiyo inatofautiana na taswira ya umaskini na hali duni ya maendeleo iliyokuwepo kabla.

Katika nyumba ya mwanakijiji Bw. Liu Yanghai, mwandishi wetu wa habari alikuta sebule kubwa na vyombo mbalimbali vya umeme vya nyumbani vikiwemo televisheni, jokofu na mashine ya kufulia nguo. Mkulima huyo alimwambia mwandishi wa habari kwa furaha kuwa, baada ya wanakijiji kuanza kujishughulisha na huduma za utalii, mapato yao yameongezeka sana. Kwa hiyo wanakijiji wengi wamejenga nyumba mpya na kununua aina mbalimbali za zana za umeme za nyumbani. Bw. Liu alikumbusha kuwa, miaka mitano na sita iliyopita hali ya maisha ya Wanu ilikuwa tofauti na hali waliyonayo sasa. Alisema (sauti 2) "Kabla ya kuanza kujishughulisha na sekta ya utalii, tulikuwa hatuna vyanzo vingi vya mapato, ambapo licha ya shughuli za kilimo, tulipata pesa kwa kufuga kuku, na maisha yalikuwa magumu."

Hapo awali mbali na kabila la Wanu, makabila mengine yenye watu wachache pia yalikabiliwa na tatizo la kuwa na mapato kidogo. Na matatizo mengine kama hali duni ya miundombinu yalikuwepo, ambapo vijiji vingi vya makabila hayo havikuwa na huduma za umeme, barabara, shule, zahanati wala maji safi ya kunywa, na robo ya watu kutoka makabila yenye watu wachache walikuwa bado hawajaondokana na tatizo la upungufu wa chakula.

Ili kuboresha hali hiyo, tokea mwishoni mwa karne iliyopita, serikali ya China ilichukua hatua mfululizo za kuyasaidia makabila hayo kupata maendeleo. Kwa mfano, tangu mwaka 2002 hadi mwaka 2004, serikali ya China ilitenga Yuan zaidi ya milioni 100, sawa na dola za kimarekani milioni 12.5, ili kuboresha miundombinu ya vijiji vya makabila yenye watu wachache, kama vile huduma za maji, umeme na barabara. Aidha, idara husika za serikali ziliwasaidia wananchi wa makabila hayo kujishughulisha sekta zinazoweza kuwaongezea mapato. Vile vile shughuli mbalimbali za sayansi na teknolojia, elimu, afya na utamduni zilitiliwa mkazo na serikali katika juhudi za kuhimiza maendeleo ya jamii katika sehemu wanakoishi watu wengi wa makabila hayo.

Mwaka jana China ilitunga mpango wa kuleta maendeleo ya watu wa makabila madogo yenye watu wachache kati ya mwaka 2005 na 2010. Bw. Le Changhong ni naibu mkuu wa idara ya uchumi iliyo chini ya kamati ya mambo ya makabila ya taifa ya China, alifahamisha mpango huo, akisema  "Malengo ya mpango huo ni kuwafanya watu wa makabila madogo waweze kujitosheleza kwa chakula ndani ya miaka mitano, na kupata maendeleo ya uchumi na jamii."

Ofisa huyo alisema katika juhudi za kutimiza malengo hayo, katika miaka mitano ijayo, serikali ya China katika ngazi mbalimbali zitatenga Yuan bilioni 1 kwa jumla katika kuboresha hali ya maisha ya watu wa makabila madogo na kuongeza uwezo wa wananchi hao katika uzalishaji mali.

Kutokana na sera za serikali, maisha ya watu wa makabila madogo yameshainuka kwa udhahiri. Kabila la Wapumi ni miongoni mwa makabila hayo. Katika kijiji kiitwacho Ganzhuhe wanakoishi Wapumi wengi, mwandishi wetu wa habari aliona barabara inayounganisha kijiji hicho na sehemu nyingine imekamilishwa, na kutokana na misaada ya serikali ya huko, wanakijiji wameanza kufuga ng'ombe. Ofisa wa huko anayeshughulikia mambo ya makabila Bi. He Juzhen alieleza kuwa, serikali iliipa kila familia ya Wapumi ng'ombe wawili bila malipo, ikiwashauri wajishughulishe na ufugaji wa ng'ombe ili kuongeza mapato.

Alisema "Hapa kwetu tunaishi katika uwanda wa juu. Tunaona ufugaji ni njia imara ya kupata pesa, kwa hiyo baada ya kushauriana na wakulima, tulitenga Yuan milioni 1 kwa ajili ya ufugaji. Hivi sasa kwa wastani familia moja ya wakulima inaweza kupata kipato cha ziada cha Yuan zaidi ya elfu 1 kwa mwaka."

Idara ya ufugaji ya huko imeandaa mafunzo kwa Wapumi, kuwafundisha namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya ng'ombe pamoja na mbinu za ufugaji. Hatua hizo zinawanufaisha Wapumi. Mwanakijiji Bi. Yang Shuxiang alimwambia mwandishi wetu wa habari, akisema  "Hapo awali maisha yetu yalikuwa ni magumu. Kutokana na misaada ya kamati ya mambo ya makabila madogo, sasa tunafuga ng'ombe na kuongeza uwezo wetu. Nachuma pesa nyingi zaidi, kwa hiyo watoto wangu wawili wanaweza kwenda shule."

Ofisa wa kamati ya mambo ya makabila ya taifa ya China Bw. Le Changhong alieleza kuwa, serikali itazidi kutoa misaada kwa makabila madogo. Alisema "Kwa upande mmoja, kutokana na kuimarika kwa uwezo wa taifa, tutatenga fedha nyingi zaidi katika maeneo wanakoishi watu wengi wa makabila madogo yenye watu wachache zaidi. Na kwa upande mwingine, tutahamasisha maeneo yenye maendeleo ya kiuchumi yatoe misaada kwa maeneo ya watu wa makabila hayo madogomadogo. Aidha tutawahamasisha wananchi wa hali mbalimbali watoe misaada kwa makabila hayo."

Idhaa ya kiswahili 2006-06-29