Wasikilizaji wapendwa, tangu mwakilishi wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia sera za kidiplomasia na usalama Bw. Javier Solana alipoikabidhi Iran mpango mpya wa nchi 6 za Russia, Marekani, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuhusu utatuzi wa suala la nyukilia la Iran, vyombo vya nchi za magharibi vinafuatilia zaidi jibu la Iran, ambapo nchi za magharibi zina haraka ya kutaka Iran itoe tamko, lakini Iran inaonekana haitaki kutoa jibu kwa haraka.
Marekani inaonekana kuwa na wasiwasi mkubwa zaidi, kabla ya hapo rais Bush wa Marekani alisema, Iran inatakiwa kutoa jibu ndani ya wiki chache. Habari zinasema Marekani inatarajia Iran itatoa jibu kuhusu mpango wa nchi 6 kabla ya mwishoni mwa mwezi Juni, na kuongeza kuwa uvumilivu wake una kikomo. Lakini matarajio ya Marekani yameshindikana. Sababu ya nchi za magharibi kuwa na haraka ya kutaka Iran itoe jibu haraka ni kutokana na mambo mawili: Kwanza hazitaki kuipa Iran nafasi ya kufanya marekebisho juu ya mpango, na zinatarajia Iran ikubali kabisa mpango huo; Pili ni kuwa zina wasiwasi Iran itapata nafasi ya kurekebisha mpango na kuwa na nafasi nzuri zaidi katika mazungumzo ya nyukilia yanayoweza kurejeshwa.
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran tarehe 21 alitaja kwa mara ya kwanza wakati wa kutoa jibu. Alisema Iran itatoa jibu kuhusu mpango mpya wa nchi 6 kabla ya tarehe 22 mwezi Agosti. Lakini, baada ya hapo watu waliona kuwa matamko waliyotoa maofisa wa Iran kuhusu suala hilo yanapingana. Gazeti la "Der Stern" la Ujerumani lilitoa habari tarehe 28 zikisema, waziri wa mambo ya nje wa Iran Bw. Manouchehr Mottaki hivi karibuni alipohojiwa na gazeti hilo alisema, Iran huenda itatoa jibu rasmi kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi nane utakaofanyika tarehe 15 mwezi Julai. Lakini Bw. Mottaki aliposhiriki kwenye mkutano wa kwanza wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa tarehe 24 huko Geneva, aliwaambia waandishi wa habari kuwa si haki kuitaka Iran itoe jibu kuhusu mpango wa nchi 6 kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi nane utakaofanyika huko St Petersburg. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bw. Hamid-reza Asefi tarehe 25 alisema, Marekani na nchi za Ulaya zinatakiwa kuwa na subira kubwa zaidi kabla ya Iran kutoa jibu rasmi kuhusu mpango wa nchi 6, hivi sasa Iran inafanya utafiti kuhusu mpango huo, hivyo Iran haikubali kutoa jibu haraka kwa nchi za magharibi kabla ya kuuelewa kwa usahihi.
Watu wanaona kuwa, mbali na tarehe ya kutoa jibu, hata katika suala la namna ya kutoa jibu, matamko ya maofisa wa Iran pia ni tofauti sana. Kuhusu hali hiyo Marekani imesema, itachukulia maneno ya mwakilishi wa kwanza wa Iran katika mazungumzo kuhusu suala la nyukilia la Iran kuwa jibu rasmi la nchi hiyo. Watu wanasema Iran inafanya vitendo hivyo kwa makusudi ili kuona msimamo wa nchi za magharibi. Lakini wachambuzi wengi zaidi wanaona, sababu yake muhimu ni kuwa Iran inaona kutoa jibu kuhusu mpango wa nchi 6 ni suala muhimu, sasa Iran bado inahitaji muda kabla ya kuafikiana kwenye msimamo wa namna moja.
Iran inaona mpango wa nchi 6 ni mzuri kuliko zamani na unaivutia Iran, isipokuwa "kusimamisha kwa muda usafishaji wa uranium" ni sharti linalopachikwa kwa Iran, ambalo Iran haitalikubali kabisa. Endapo Iran itakataa mpango huo, basi Marekani itakuwa na udhuru wa kuunda umoja wa kuipinga Iran duniani, pia itaziweka Russia na China, ambazo zimekuwa zikitarajia kutatua suala la nyukilia la Iran kwa mazungumzo ya kidiplomasia, katika hali ya kufedheheka. Hivyo Iran inafahamu, jibu lililo zuri ni kukubali mpango huo kwa masharti fulani, na kuleta mvutano kati yake na upande wa Marekani na nchi za Ulaya katika duru jipya la mazungumzo. Lakini "masharti" hayo ni yapi? Na kikomo cha usuluhisho cha Iran katika mazungumzo ni kipi? Hayo ni mambo ambayo Iran inapaswa kutafakari na kuwa na msimamo wa namna moja.
Habari zinasema mwakilishi wa Umoja wa Ulaya Bw. Solana atafanya ziara mjini Teheran wiki ijayo, ambapo atakuwa na mazungumzo na maofisa wa Iran kuhusu mpango wa nchi 6. Pengine watu wanaweza kupata baadhi ya majibu kutokana na ziara hiyo.
Idhaa ya Kiswahili 2006-06-29
|