Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-06-29 18:49:34    
Wapanda mlima kuwasaidia watoto wenye shida

cri

Wakati watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanazidi kuongezeka siku hadi siku nchini Tanzania, mikakati mbalimbali imekuwa ikichukuliwa katika kujaribu kuleta unafuu kwa watoto hao. Hivi karibuni makampuni kadhaa yaliandaa harambee ya kuhamasisha kupanda mlima Kilimanjaro huko Tanzania ili kuchangisha fedha za kusaidia watoto hao.

Kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo Watanzania wengi na baadhi kutoka katika mataifa ya kigeni wamekuwa wakipanda Mlima Kilimanjaro katika jitihada za kukusanya fedha za kuwasaidia watoto wanaoishi katika maisha magumu. Watoto hao ni pamoja na yatima waliofiwa na wazazi wao kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. Utaratibu wa kupanda mlima huo kwa ajili ya lengo la kukusanya fedha umekuwa ukiandaliwa na Mgodi wa madini ya dhahabu wa Geita (GGM) ulioko mkoani Mwanza, nchini Tanzania.

Imebainika kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi wa makampuni wanaodhamini mpango huo wa kupanda mlima wanaguswa sana na tatizo la watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu. Hali hiyo, ndiyo inayofanya idadi ya wafanyakazi hao izidi kuongezeka kila mwaka tangu mpango huo ulipoanza kutekelezwa. Mpaka sasa mpango huo umekwishakusanya kiasi cha Sh milioni 410 za Tanzania kutoka kwa makampuni mbalimbali na watu binafsi walioguswa na matatizo hayo na fedha hizo tayari zimefikishwa kwa wahusika.

Katika harambee ya mwaka 2002 kampuni hiyo ilikusanya kiasi cha Sh milioni 40 na mwaka 2003 kiasi hicho kiliongezeka hadi kufikia Sh milioni 100. Mwaka juzi harambee iliwezesha kukusanywa kwa Sh milioni 150 wakati mwaka jana, iliwezesha kukusanywa kwa Sh milioni 120. Pia mwaka huu, jumla ya wafanyakazi 51 wa makampuni mbalimbali walishiriki kwa lengo hilo la kukusanya fedha za kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Waziri Mkuu wa Tanzania Bw Edward Lowassa, ndiye aliyeanzisha harambee ya kupanda mlima huo. Baadhi ya wafanyakazi wageni waliopanda mlima katika harambee ya mwaka huu ni wa kutoka nchi za Australia, Ujerumani, Afrika Kusini na Kenya. Kila mwaka watu karibu elfu 50 wanapanda mlima huo kwa sababu mbalimbali zikiwemo utalii na kutaka kuweka rekodi, lakini watu wengi waliopanda mlima wanasema waliamua kupanda mlima na kushiriki kwenye harambee hiyo kutokana na kuguswa na matatizo yanayowakabili watoto wanaoishi katika mazingira magumu, kama vile kukosa chakula, nguo, elimu na malazi.

Bi Ludigades Shayo ni ofisa wa kampuni hiyo amesema watoto hao wamekuwa wakisahauliwa katika kupatiwa huduma muhimu katika maisha na matokeo yake ni kuishia gerezani au kuwa katika hatari ya kupatwa na magonjwa hatari kama Ukimwi. Alisema ni mara ya kwanza kwake kupanda mlima huo na kwamba hatua hiyo itasaidia kukusanya fedha nyingi za kuwasaidia watoto hao. Bi Shayo ametoa mwito kwa mashirika na taasisi nyingine kutoa michango ili kupanua wigo wa kutoa misaada kwa watoto hao. Mfanyakazi mwingine alisema ni jambo linaloleta faraja kuona ari ya watu kutoa misaada kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu, inaongezeka.

Pamoja na kwamba idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu inazidi kuongezeka, lakini jitihada za pamoja za Serikali na watu binafsi katika kuwachangia watoto hao, zinaleta faraja. Hali hiyo inaonesha jinsi watu wanavyoguswa na tatizo hilo ambalo kwa kiwango kikubwa linatokana na wazazi wa watoto hao kufariki hasa kwa Ukimwi. Mwamko wa wananchi wa Tanzania na wageni wanaoishi katika nchi hiyo kutambua chanzo cha tatizo hilo, kumewafanya wawe katika nafasi nzuri ya kupunguza tatizo.

Wananchi wengine pia wamezipongeza kampuni zinazosaidia kutatua tatizo hilo, wanaona kuwa kampuni hizo mbali na kuangalia faida zake kiuchumi pia zinajitahidi kuhakikisha hali ya kijamii inakuwa nzuri. Kutokana na sehemu ya kusini mwa Afrika kuathiriwa vibaya na tatizo la Ukimwi, harambee za namna hii zinaweza kutoa mchango mkubwa kwenye kupunguza tatizo la maisha magumu kwa watoto yatima ambao wamepoteza wazazi wao kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Idhaa ya Kiswahili 2006-06-29