Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-03 15:39:47    
Mwigizaji mashuhuri wa filamu mwenye asili ya China, Lu Yan

cri

Bibi Lu Yan ni mwamuzi pekee wa Mashariki katika kamati ya waamuzi wa tuzo ya Oscar nchini Marekani, alikuwa mwigizaji nyota wa filamu mwenye asili ya China. Ingawa sasa ana umri wa miaka 79 lakini vyombo vya habari vinamsifu kuwa bado ni "kisura kama zamani".

Bi. Lu Yan alizaliwa mjini Beijing, mwaka 1947 alihamia Honolulu nchini Marekani na mwaka 1956 alijiunga na chuo kikuu kimoja mjini California na kujifunza uigizaji wa filamu. Katika mtihani wa kumaliza masomo alikuwa mwigizaji katika mchezo wa kuigiza "Chumba cha Chai Agosti", uigizaji wake ulisifiwa sana. Tokea hapo alianza maisha ya uigizaji huko Hollywood. Bibi Lu Yan aliwahi kushirikiana mwendeshaji filamu mkubwa aliyepata zawadi ya Oscar Bw. Frank Borzage na mwigizaji filamu mkubwa Bw. Marlon Brando, kutokana na uigizaji wake hodari amekuwa mwigizaji mkubwa wa Hollywood mwenye asili ya China.

Bibi Lu Yan alipokuwa msichana, China ilikuwa haijafunguliwa mlango wake kwa nchi za nje, wageni walikuwa hawaielewi sana China. Alisema, "Nilipokuwa msichana sikuwa na nafasi nyingi za kuigiza filamu kwa sababu nilikuwa Marekani. Wakati huo filamu zote kuhusu China zilikuwa zikieleza mambo kabla ya miaka hamsini hivi. Kwa sababu ya kutoielewa China ilivyo, filamu walizotengeneza Wamarekani zilikuwa za kichekesho, nilitoa mapendekezo yangu walikubali na kusema 'Ok, Ok!' lakini waliendelea na yao wenyewe."

Lu Yan aliigiza kama mama wa mfalme Ci Xi katika filamu iitwayo Mfalme wa Mwisho wa China iliyotengenezwa na Marekani mwaka 1986. Katika filamu hiyo Lu Yan pia alibishana mara nyingi na mwendeshaji wa filamu hiyo wa Italia, Bernardo Bertolucci. Filamu hiyo ilipata tuzo ya filamu ya Oscar mwaka 1987.

Lu Yan alikuwa mwigizaji katika filamu nyingi za Kichina na aliigiza wahusika wengi wasiosahaulika. Kwa mara tatu aliiga mama wa mfalme Ci Xi katika filamu za mambo ya Enzi ya Qing na mara zote tatu alipata tuzo ya "farasi wa dhahabu" za Taiwan. Pia alishiriki katika filamu iliyoongozwa na mwongozaji maarufu Xie Jin iitwayo "Familia ya Mwisho ya Matajiri". Katika muda wa miaka 35 iliyopita, Lu Yan aliigiza katika filamu zaidi ya 200 na amepata tuzo kumi kadhaa za aina mbalimbali. Alipozungumzia tuzo zake alisema, "Nafurahi uigizaji wangu unakubaliwa na watazamaji, lakini ufanisi wangu sio wangu binafsi bali unatokana na msaada kutoka kwa watu wengi, licha ya waongozaji filamu na pia waigizaji wengine."

Lu Yan alifanya kazi nyingi katika maingiliano ya utamaduni kati ya China na Marekani, ili kuwajulisha watu wa nchi mbili filamu na michezo ya televisheni. Alitafsiri filamu ya kikatuni ya "Mickey Mouse and Donadduck" kwa Kichina na inawavutia sana watoto wa China. Aliwasaidia waigizaji wengi wa China kwenda Marekani kushiriki kwenye uigizaji wa filamu ikiwa ni pamoja na Zhang Ziyi na Gong Li. Lu Yan alisema, "Napenda niwe daraja niwafahamishe watu wa Marekani utamaduni wa China, na Marekani ipige filamu nyingi zaidi nchini China, kwa kufanya ushirikiano na watu wa China, ili wapate fursa ya kujifunza kwao."

Alipokuwa nchini China, Lu Yan aliwahi kujifunza opera ya Kibeijing kutoka kwa msanii mkubwa wa opera hiyo Mei Lanfang, usanii wake wa opera ya Kibeijing ni mzuri na mara nyingi alionesha michezo yake jukwaani, na kuwaonesha watu wa Marekani jinsi sanaa ya China ilivyo. Mwaka 1980 alichapisha kitabu chake cha Kiingereza "Michezo Iliyochaguliwa ya Opera ya Beijing", na aliwahi kuifanyia opera ya Beijing mageuzi ya kuimbwa kwa Kichina na itafsiriwe kwa Kiingereza pembeni mwa jukwaa, na izungumzwe kwa Kiingereza ili watazamaji wa Marekani wafahamu zaidi opera yenyewe.

Katika miaka mingi iliyopita, baada ya kuimba kidogo opera ya Beijing alimwuliza mwalimu wake Mei Langfang, kwamba alionaje uimbaji wake, Mei Lanfang alisema, "kila kitu umekigusa lakini bado hujakifikia kiwango kinachotakiwa." Maneno hayo yalimwingia sana akilini, alisema, "uigizaji lazima ufikie kiwango kinachotakiwa". Mama Lu Yan anaishi katika mazingira ya mchanganyiko wa utamaduni wa China na Kimagharibi, lakini hakusahau kwamba yeye ni Mchina, mila, utamaduni, fahari ya taifa la China anaithamini sana katika maisha yake.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-03