Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-04 16:05:59    
Mafanikio kadhaa yapatikana katika kupunguza umaskini duniani

cri

Ili kukaribisha mkutano wa mwaka wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa uliofanyika tarehe 3 huko Geneva, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti mbili kwa mfululizo. Ripoti hizo zinaona kuwa, dalili za kufurahisha zimeonekana katika juhudi za kupunguza umaskini duniani, lakini bado zinakabiliwa na changamoto kubwa. Ripoti hizo pia zimependekeza kuwa, nchi zinazoendelea zinapaswa kutunga sera za mageuzi ya kiuchumi zinazoambatana na hali halisi nchini mwao, ili kuleta ongezeko la uchumi lenye utulivu, na kusaidia kupunguza tofauti za mapato duniani.

Ripoti moja imekadiria kuwa, mwaka 2006 wastani wa ongezeko la uchumi wa nchi zinazoendelea utafikia asilimia 6, na ongezeko la uchumi wa nchi zilizo nyuma kabisa kimaendeleo litafikia asilimia 7. Ripoti hiyo imesema nchi za Asia zimepata mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini. Mambo mengine ya kufurahisha ni kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaosoma shule za msingi duniani, kupunguzwa kwa vifo vya watoto wachanga, kuboreshwa kwa hadhi ya kiuchumi na kijamii kwa wanawake na kuzuia hali ya kutoweka kwa misitu.

Ripoti hiyo imedhihirisha kuwa, licha ya nchi za Asia, nchi na sehemu zinazoendelea za mabara mengine, hasa nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara bado zinakabiliwa na changamoto kubwa katika kutimiza lengo la kupunguza kwa nusu idadi ya watu maskini ifikapo mwaka 2015. Ripoti hiyo imesema, mwaka 2003 watu milioni 800 wanaoishi katika nchi zinazoendelea walikumbwa na njaa. Katika sehemu za Afrika zilizo kusini mwa Sahara, katika miaka kumi hivi iliyopita idadi ya watu walioishi katika hali duni kabisa ya kimaendeleo iliongezeka, kiasi cha vifo vya watoto wachanga ni maradufu ya wastani wa kile cha nchi zinazoendelea, na idadi ya watoto wanaosoma ni chini zaidi kuliko ile ya nchi nyingine zinazoendelea.

Ripoti hiyo imethibitisha umuhimu wa msaada wa maendeleo wa kiserikali kwa kuhimiza maendeleo endelevu ya nchi zinazoendelea, lakini pia imedhihirisha kuwa, nchi zilizoendelea bado hazijatoa msaada wa kutosha kwa maendeleo ya nchi zinazoendelea. Hivi sasa, nchi tano tu zilizoendelea duniani za Denmark, Luxemburg, Uholanzi, Norway na Sweden ambazo misaada ya maendeleo ziliyotoa imezidi asilimia 0.7 ya thamani ya jumla ya uzalishaji bidhaa wao.

Ripoti nyingine kuhusu tofauti za mapato kati ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea imedhihirisha kuwa, kwa ujumla katika miaka 50 iliyopita, hasa katika miaka 25 iliyopita, tofauti za mapato duniani bado ni kubwa sana na zinaendelea kuongezeka. Moja ya sababu muhimu ni kiwango cha mapato ya nchi za viwanda kimeongezeka kwa hatua madhubuti, lakini nchi nyingi zinazoendelea zinashindwa kupata ongezeko la mapato la utulivu.

Ripoti hiyo imesema kwa muda mrefu, baadhi ya watu wamechukulia kuwa, kama nchi zinazoendelea zinafungua soko lao la biashara na la fedha, na kujiunga na utandawazi wa uchumi duniani, uchumi wao hakika utapata maendeleo. Lakini ukweli wa mambo umedhihirisha kuwa mawazo hayo si sahihi. Sababu muhimu ni kwamba, hivi sasa soko la dunia bado sio la haki, uwekezaji wa kimataifa hauwezekani kuingia wenyewe katika nchi zinazoendelea zenye hali duni ya miundo mbinu, upungufu wa watu wenye ujuzi na kutegemea sekta moja. Nchi zinazoendelea bado hazina uwezo wa kukabiliana na changamoto za kupanda kwa bei za rasilimali na vurugu za soko la fedha duniani.

Ripoti hiyo inaona kuwa, kwa nchi zinazoendelea na nchi zinazotaka kubadilisha miundo yao ya kiuchumi, kufanya mageuzi ya kiwango kikubwa kutaleta maslahi ya muda mfupi tu, na wala hakutasaidia kuleta ongezeko la uchumi. Uzoefu wa China na Vietnam umeonesha kuwa, kutekeleza sera za mageuzi zenye utulivu na taratibu kutaleta ongezeko endelevu la uchumi.

Ripoti hiyo imesisitiza kuwa ili kupunguza tofauti za mapato duniani, licha ya kuweka mazingira mazuri ya kimataifa kwa maendeleo, nchi zinazoendelea zinapaswa kutunga sera za kiuchumi na njia ya mageuzi inayoambatana na hali halisi ya nchini, kukuza uchumi unaotegemea sekta nyingi, ili kuongeza uwezo wa kupambana na hali ya kupanda kwa bei za rasilimali na vurugu kwenye soko la fedha duniani.

Idhaa ya Kiswahili 2006-07-04