Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-05 19:09:57    
Makampuni ya kutengeneza dawa ya China yaongeza nguvu katika utafiti wa aina mpya ya dawa

cri

Ingawa nchini China kuna makampuni zaidi ya 6000 ya kutengeneza dawa na idadi hiyo inachukua nafasi ya kwanza duniani, lakini uwezo wa China kutafiti aina mpya ya dawa bado uko nyuma. Makampuni mengi yanatengeneza dawa kwa kutumia hataza za nchi za nje zilizopitwa na wakati badala ya kutafiti aina mpya ya dawa zenye hakimiliki. Ili kuinua kiwango cha utafiti wa makampuni hayo, na kuifanya China iingie kwenye nafasi za juu katika sekta ya utengenezaji wa dawa duniani, China imechukua hatua mbalimbali kuyaunga mkono makampuni hayo yatafiti dawa mpya kwa kujitegemea katika miaka ya hivi karibuni.s

Takwimu zinaonesha kuwa, kila mwaka idara kuu ya usimamizi wa sifa ya chakula na dawa ya China inapokea maombi makumi kadhaa tu ya kuandikisha dawa mpya, hali hii hailingani kabisa na idadi ya makampuni yanayotengeneza dawa nchini China. Ingawa idadi ya makampuni yanayotengeneza dawa nchini China inaongezeka kwa kasi, lakini uwezo wa utafiti wa dawa kwa kujitegemea bado haujainuka kwa kiasi kikubwa. Mkurugenzi wa ofisi ya dawa ya idara ya maendeleo ya vijiji na jamii katika wizara ya sayansi na teknolojia ya China Bw. Yang Zhe alisema, makampuni ya China yalitengeneza dawa kwa kuiga zile za nchi za nje ambazo hataza zake zimepitwa na wakati. Bw. Yang alisema,

"kwa dawa za nchi za nje ambazo hataza zake zimepitwa na wakati, tunaweza kuendelea kuzitengeneza. Lakini kwa kuwa dawa hizo ni za zamani, basi ufanisi wake si mzuri. Kwa kawaida dawa zinaweza kuigwa miaka 10 baada ya dawa hizo kutolewa sokoni."

Kwa nini ni vigumu kwa makampuni ya dawa ya China kutengeneza dawa mpya? Imefahamika kuwa, utafiti wa dawa mpya ni mgumu sana, si kama tu unahitaji fedha nyingi bali unachukua muda mrefu. Kwa kawaida, utafiti wa dawa moja mpya unachukua muda wa miaka 8 hadi 10, gharama za utafiti kwa wastani zinaweza kufikia dola za kimarekani milioni mia kadhaa. Endapo fedha nyingi na muda mrefu ukitumika katika utafiti, si lazima kuwa utakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi. Kwa mujibu wa takwimu husika, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ufanisi wa dawa na matokeo mabaya baada ya kutumia dawa, hivi sasa kwa wasatani dawa moja kati ya kumi zilizofanyiwa tathmini ya matibabu hatimaye inaweza kuuzwa sokoni.

Makampuni ya kutengeneza dawa za China yamepata maendeleo katika miongo kadhaa iliyopita, na uwezo wa utafiti wa mapampuni hayo bado hauwezi kufikia kiwango cha kimataifa. Ikilinganishwa na makampuni makubwa ya kimataifa, makampuni ya China bado yako nyuma kwa ukubwa, mitaji na teknolojia. Gharama kubwa, hatari kubwa na muda mrefu wa utafiti ni vikwazo kwa makampuni ya China kutafiti dawa mpya.

Kutokana na hali hiyo, ili kuhimiza maendeleo ya makampuni ya kutengeneza dawa ya China na kuinua kiwango cha sekta ya utengenezaji wa dawa, katika miaka ya hivi karibuni serikali ya China imechukua hatua mbalimbali za uungaji mkono na utoaji motisha.

Hatua ya kwanza ni kurekebisha uelekezaji wa kisera, kwa mfano kurekebisha na kukamilisha sheria na kanuni husika zikiwemo sheria ya usimamizi wa dawa na sheria ya hataza, na kuweka vizuizi kadhaa kwa vitendo vya kutengeneza dawa kwa kuiga na kuelekeza makampuni ya dawa yafuate njia ya uvumbuzi.

Ya pili, serikali ya China pia imeongeza uwekezaji katika utafiti wa dawa mpya. Makampuni mengi makubwa ya kimataifa yana taasisi zake za utafiti na hutafiti dawa mpya kwa kujitegemea. Lakini China ina hali tofauti, kutokana na mahitaji ya utaratibu wa zamani wa uchumi wa kimpango na vizuizi vya ukubwa wa makampuni, kazi ya utafiti wa dawa mpya inatekelezwa na taasisi kubwa za utafiti za taifa, wala si viwanda vya dawa. Serikali ya China imehamasisha makampuni ya dawa kuwekeza katika utafiti wa dawa mpya kwa kuongeza uwekezaji kwa utafiti wa dawa mpya katika taasisi za utafiti. Naibu mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya vijiji na jamii katika wizara ya sayansi na teknolojia ya China Bw. Sun Hong alisema:

"katika mpango wa 10 wa maendeleo ya miaka mitano, fedha zilizotengwa na wizara ya sayansi na teknolojia katika utafiti wa dawa mpya kwa jumla zimefikia yuani milioni 900, lakini uwekezaji huo pia utahamasisha uwekezaji wa makampuni. Aidha, uwekezaji wa wizara yetu hauhusiani na malipo ya nguvu kazi, katika nchi za nje, asimilia 40 ya uwekezaji kama huo imetumika katika malipo ya nguvu kazi, hivyo uwekezaji wetu umetumika kihalisi katika utafiti wa dawa mpya."

Aidha, serikali ya China pia inafanya utafiti kuhusu kuhamasisha makampuni kutafiti aina mpya za dawa kwa hatua ya sera ya utozaji kodi.

Kutokana na juhudi za serikali ya China, makampuni mengi ya China yameanza kuzingatia utafiti wa aina mpya za dawa. kampuni ya dawa ya Shanghai ambayo ni kampuni kubwa kabisa ya kutengeneza dawa nchini China imeanzisha taasisi za utafiti nchini Marekani na Canada, hivi karibuni imesaini mkataba wa ushirikiano wa utafiti wa dawa na kampuni moja ya Japan. Katika miaka mitatu iliyopita, kampuni ya dawa ya Guangzhou imewekeza yuan milioni 800 katika utafiti wa dawa, ikiwa ni asilimia 7 ya mapato ya jumla. Aidha, shughuli za utafiti wa dawa mpya katika makampuni madogo na ya wasatani pia zinaungwa mkono na mradi wa taifa wa utafiti wa teknolojia ya juu.

Katika utafiti wa dawa mpya, China pia ina raslimali maalum yaani dawa za jadi za China. Kwa upande mmoja, China ina rasilimali nyingi ya dawa za mitishamba, kwa upande mwingine, kutokana na mfumo wa nadharia na mbinu za utafiti wa matibabu ya jadi ya China, inawezekana kupata mitizamo mipya ya utafiti wa aina mpya za dawa.

Kwa mfano, dawa ya kwanza ya kemikali iliyotengenezwa na China kwa kujitegemea inayotiwa Artemisinin ni dawa iliyotengenezwa kwa kutumia wazo la dawa za mitishamba ya jadi. Dawa hiyo ya katibu malaria kwa kasi na kwa ufanisi inasifiwa duniani kuwa alama muhimu katika historia ya utafiti wa dawa za kutibu malaria. Mwaka 2004, shirika la afya duniani liliipendekeza dawa hiyo iwe dawa ya ngazi ya kwanza ya kuzuia malaria na kuieneza kote duniani. Naibu mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Fuxing ya Shanghai iliyotafiti dawa hiyo Bw. Chen Qiyu alieleza,

"vijidudu vya malaria vimekuwa sugu kwa dawa nyingi za zamani barani Afrika, hivyo shirika la afya duniani limeamua kueneza dawa hiyo ya Artemisinin barani humo. Hali hiyo imetoa nafasi nzuri kwa mustakabali wa kampuni yetu."

Hivi sasa makampuni mengi zaidi ya China yameanza kuzingatia utafiti wa dawa za jadi za China, na manufaa makubwa ya dawa za jadi za China pia yamehamasisha juhudi za makampuni ya China kufanya utafiti wa aina mpya za dawa.

Wasikilizaji wapendwa, mlikuwa mkisikiliza maelezo kuhusu Makampuni ya kutengeneza dawa ya China yanavyoongeza nguvu katika utafiti wa aina mpya za dawa. Asanteni kwa kutusikiliza. Kwa herini!