Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-05 19:22:11    
Utatuzi wa mgogoro askari wa Israel aliyetekwa

cri

Hadi hivi sasa mgogoro wa mateka kati ya Palestina na Israel umeendelea kwa zaidi ya wiki moja. Tarehe 4, wakati muda wa mwisho uliowekwa na makundi ya watu wenye silaha nchini Palestina yaliyomteka askari wa Israel ulipofika, Israel iliendelea kukataa masharti yao, na kusema haitashiriki kwenye mazungumzo na makundi hayo. Hapo baadaye makundi ya watu wenye silaha nchini Palestina yalijitoa kwenye mazungumzo yaliyokuwa yanafanyika kati yao na wasuluhishi kutoka Misri kuhusu kumwaachia huru mateka anayeshikiliwa, hivi sasa hali ya mateka huyo haifahamiki. Lakini ni kwanini Israel inashikilia msimamo wake imara? Endapo mgogoro wa mateka huyo hautatatuliwa vizuri, je matokeo yake yatakuwaje? Na je, hivi sasa bado kuna nafasi kwa utatuzi wa mgogoro wa mateka? Mwandishi wetu wa habari akiwa na maswali hayo alifanya mahojiano na Bw. Yin Gang, ambaye ni mtafiti wa idara ya Asia ya magharibi na Afrika katika taasisi ya sayansi ya jamii ya China. Bw Yin alisema sababu ya kukataa kabisa kwa Israel masharti ya makundi ya watu wenye silaha ya Palestina ya kubadilisha mateka wa Israel kwa wapalestina 1,000 waliofungwa ni kutokana na kufikiria mambo matatu,

"Endapo Israel inakubali masharti hayo, basi matukio ya kuteka waisrael yataongezeka, hivyo kamwe Israel haiwezi kukubali; Pili, tukio hilo ni tofauti na matukio ya kuteka watu yaliyotokea hapo awali, safari hii ni mara ya kwanza kwa makundi ya watu wenye silaha nchini Palestina kushambulia wanajeshi wa Israel kwa kutumia mahandaki yaliyochimbwa ardhini; Tatu, kwa kutupia macho mazingira kwa ujumla, kundi la Hamas lilichukua madaraka ya serikali miezi kadhaa iliyopita, ingawa bado halijakubali kutoa ahadi ya kimsingi kutokana na utashi wa jumuiya ya kimataifa, ambapo Israel pia inaonekana kama inataka kuipindua serikali ya Hamas. Makundi ya watu wenye silaha nchini Palestina yalizusha tukio hilo, ambalo limetoa nafasi kwa Israel kujitahidi kadiri iwezavyo kupambana na serikali ya Hamas."

Bw. Yin Gang alisema nia halisi ya makundi ya watu wenye silaha nchini Palestina kuchagua wakati huu muhimu kuzusha tukio la mateka ni kutaka kuvuruga hali ya hivi sasa.

"Kwanza, tukio hilo lilitokea wakati mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw.Abas akiwa na mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert katika hali ya kuelewana. Pili, tukio hilo lilitokea siku moja kabla ya kufikiwa kwa maafikiano ya kusaini 'makubaliano ya waraka wa gerezani' kati ya makundi mbalimbali nchini Palestina, hususan kati ya Hamas na Fatah. Kwa hiyo lengo muhimu la makundi ya watu wenye silaha la kuzusha tukio hilo ni kutaka kuharibu umoja unaoweza kuundwa ndani ya Palestina, na kuharibu mazingira ya mazungumzo yanayoweza kufanyika kati yao."

"Jeshi la Kiislamu" ni moja ya makundi matatu ya watu wenye silaha ya Palestina yaliyoshiriki kwenye tukio la utekaji nyara. Msemaji wa "Jeshi la Kiislamu" tarehe 4 mwezi huu alisema, mazungumzo kuhusu mateka wa askari wa Israel yamemalizika, na hawawezi kudokeza habari yoyote kuhusu hali ya askari huyu ikiwa ni pamoja na kama atauawa au la.

Bw. Yin Gang alisema hali ilivyo sasa inaonesha kuwa, tukio la utekaji nyara lilitokea halikutokana na amri ya waziri mkuu Ismail Haniyeh, wala si uamuzi wa makundi yote ya huko, bali ni uamuzi wa watu wachache, ni kitendo cha watu waliobahatisha, watu waliofanya kazi muhimu katika shughuli hiyo ni viongozi wa kundi la Hamas. Kwa upande mmoja, tukio hilo linaonesha hali yenye matatizo katika mambo ya ndani ya Palestina, kwa upande mwingine linaonesha kuwa endapo jambo hilo likipanuliwa bila vizuizi, basi makundi yatakayohusishwa siyo serikali ya Hamas na makundi ya Palestina, bali ni pamoja na nchi za Misri na Syria na kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kikanda.