Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-06 18:43:46    
Wabuyi wapata maendeleo ya kiuchumi na kuboresha mazingira

cri

Kabila la Wabuyi lina watu milioni 3 hivi, ni moja kati ya makabila madogomadogo hapa nchini China. Wabuyi wengi wanaishi katika mikoa ya Guizhou, Yunnan na Sichuan, kusini magharibi mwa China. Hapo awali Wabuyi walikuwa wanajishughulisha na kilimo tu, kama vile kilimo cha mipunga. Katika miaka ya hivi karibuni, shughuli za utalii na ufugaji zimeendelezwa katika vijiji vya Wabuyi, watu wengi wamepata pesa na maisha yao yameinuka sana.

Mwandishi wetu wa habari alitembelea kijiji cha Wabuyi kiitwacho Shangshui, mkoani Guizhou. Na ametuandalia makala hii.

(sauti 1) Nilipokaribia kijiji cha Shangshui, mto mdogo ndio ulinivutia macho. Mto huo una jina zuri sana, unaitwa Huaxi, maana yake ya Kichina ni mto wa maua. Kando ya mto wa maua, kuwa kiwanja cha mapumziko ambacho kina kibanda cha mapumziko, meza na viti vya mawe ambavyo watu wanaweza kukaa na kucheza chesi, na kuna njia ndefu na nyembamba kwa ajili ya kufanya matembezi. Kwenye kiwanja hicho, wasichana kadhaa wa kabila la Wabuyi wanafanya maonesho ya ngoma kwa wanavijiji wenzao. Wasichana hao wanatoka kikundi cha maonesho cha kijiji hicho. Walisema (sauti 2) "Utaratibu wote tunaoandaa sisi wenyewe. Kikundi chetu kina wachezaji 30, wakiwemo wasichana na wavulana. Wanakijiji wanapenda utaratibu wetu, kwa vile hizo ni ngoma na nyimbo za kabila letu."

Kiwanja hicho cha mapumziko kilijengwa mwaka jana kwa gharama zaidi ya Yuan laki moja, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani zaidi ya elfu 12. Wakulima wakimaliza shughuli zao mashambani au wakati wa jioni kama hali ya hewa ni nzuri, wanakuja kiwanjani kushindana kuimba nyimbo za kienyeji na kucheza chesi. Kutokana na mpango wa kamati ya kijiji hicho, vifaa mbalimbali kwa ajili ya mazoezi ya kujenga mwili pia vitafungwa kiwanjani hapo, ili wakulima waweze kufanya mazoezi.

Nikiagana na wachezaji hao, niliendelea na matembezi. Niliweza kuwaona mabata walikuwa wakicheza mtoni, huku watalii kadhaa wakiwa wameshika mishipi ya kuvulia wakisubiri samaki kwenye ndoana. Mto Huaxi hupita katikati ya kijiji hicho kilichozungukwa na milima. Ofisa wa mji wa Guiyang anayeshughulikia kilimo Bw. Zhang Junfa alisema (sauti 3) "Kijiji chetu cha Shangshui kina mandhari nzuri. Kijiji hicho ni kijiji cha kabila la Wabuyi, ambao ni wapole sana. Unaweza kuhisi ukarimu na upole wao mara baada ya kuingia kijijini."

Mbele ya nyumba ya familia moja ya wakulima, wasichana watatu Wabuyi waliimba nyimbo za kuwakaribisha wageni, nilifuatana nao kuingia kwenye nyumba hiyo. Hiyo ni moja ya familia inayotoa huduma ya utalii, ambayo ni hatua muhimu ya kuongeza mapato ya wakulima wa kijiji cha Shangshui. Kwa mfano, mapato ya familia hiyo kwa mwaka ni karibu Yuan elfu 40, sawa na dola za kimarekani elfu 5.

Niliangalia kwa makini nyumba hiyo ambayo ilifanyiwa ukarabati hivi karibuni. Kwenye nyumba hiyo kuna vifaa mbalimbali vya burudani vikiwemo televisheni, radio kaseti, meza ya biliadi na chumba cha kucheza dansi. Maua na miti ya aina mbalimbali imepandwa kwenye bustani. Mmiliki wa nyumba hiyo Bi. Luo Chun aliniambia, akisema (sauti 4) "Baada ya kwisha kwa majira ya baridi, wageni wanaanza kuongezeka. Wakazi wa mijini wanakuja kula chakula chenye mapishi maalumu ya kijijini, hapa kuna mboga mbichi na hewa nzuri. Sasa nimeshapanda miti ya matunda, kwa hiyo wageni wanakuja kuchuma wenyewe matunda ya aina mbalimbali."

Nilifutana na Bi. Luo Chun tukielekea katikati ya kijiji hicho, ambapo niligundua kuwa, njia zinazounganisha nyumba mbalimbali na barabara kuu zote zimejengwa kwa saruji, kwa hiyo ni safi sana. Bi. Luo Chun alinifahamisha kuwa, hapo awali mazingira ya kijijini hapo yalikuwa machafu, na hivi sasa wanakijiji wanazingatia sana kuhifadhi mazingira kutokana na kuboreshwa kwa maisha yao. Alitoa mfano akisema, mwaka jana vyombo kadhaa vya kushughulikia takataka vilijengwa kijijini, kama vile shimo la kuzalisha gesi ya kinyesi, shimo la kushughulikia takataka na mabomba ya kutoa maji machafu. Mazingira safi si kama tu yanawanufaisha wanakijiji wenyewe, bali pia yanawavutia watalii wengi zaidi.

(sauti 5) Nikisikiliza maelezo ya mama huyo, niliwasili nyumbani kwa Bi. Wang Lu, ambaye ni hodari kwa kufuga nguruwe. Mwanamke huyo alisema mwaka huu anafuga nguruwe zaidi ya 30, na mume wake anajishughulisha na kazi ya uchukuzi. Aliongeza kuwa mwaka jana familia hiyo ya watu wanne ilipata pato la karibu Yuan elfu 40, sawa na dola za kimarekani elfu 5.

Nilifahamishwa kuwa, kwa sababu kijiji cha Shangshui kipo karibu na mji na kina mashamba yenye rutuba, kilimo cha mboga pia ni mbinu ya kuongeza mapato. Kwa mujibu wa takwimu, mwaka 2005 mapato ya wastani ya kijiji hicho yaliongezeka kwa Yuan 1,200, sawa na dola za kimarekani 150 kuliko mwaka 2004.

Ofisa anayeshughulikia mambo ya vijiji Bw. Zhang Junfa alifafanua kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, vijiji vingi vya kabila la Wabuyi vimepata maendeleo, na kijiji cha Shangshui ni kimojawapo. Alisema serikali itazidi kuchukua hatua za kukuza uchumi wa vijiji vyenye watu wa makabila madogomadogo na kuboresha mazingira ya vijiji hivyo.


1  2