Sehemu ya Palestina na Israel ni sehemu iliyojaa hali ya wasiwasi mkubwa, vurugu na mapambano ya kijeshi, ambayo imeleta matatizo makubwa na kutishia usalama wa maisha yao. Hivi karibuni waandishi wetu wa habari wawili walitembelea ofisi ya China iliyoko Palestina, na kusikiliza masimulizi yao kuhusu maisha yao katika mazingira ya kivita.
Kutokana na migogoro ya kivita, ofisi ya China huko Palestina iliondoka sehemu ya Gaza mwaka 2004, na kuhamia Ramallah, mji ulioko kando ya magharibi ya mto Jordan. Ikilinganishwa na sehemu ya Gaza, hali ya Ramallah ni tulivu zaidi, lakini bado mji huo bado unadhibitiwa na jeshi la Israel. Kila siku kuna ndege za kijeshi za Israel zinazofanya upelelezi kwenye anga ya mji wa Ramallah. Magari ya kivita na kijeshi ya jeshi la Israel wakati wowote yanaweza kuingia mjini Ramallah kuwasaka watu wenye silaha wa Palestina. Balozi wa China Bw. Yang Weiguo alisema kuwa wamewahi kunusurika mara mbili.
"Mara ya kwanza ilikuwa ni kwenye uwanja wa mji, kilomita 1 tu kutoka mahali tulipokuwa, wakati ule ilikuwa ni mchana na pale uwanjani kulikuwa na watu wengi, askari wa Israel pamoja na magari ya kijeshi zaidi ya 10, walikuwa wakiwasaka watu wenye silaha wa Palestina, wakatupiana risasi, watu wengi waliuawa au kujeruhiwa. Sehemu ya katikati ya mji ni mahali ambapo tunakwenda mara kwa mara kufanya shughuli au kununua mahitaji, endapo linatokea tukio la dharura kama hilo, ni hatari sana."
Safari nyingine askari wa jeshi la Israel walikuwa wanawakamata watu ndani ya jengo moja karibu na ofisi ya China, magari ya kivita kumi kadhaa yalikuwa yakizunguka mbele ya ofisi ya China kuwasaka watu waliokuwa wanawafuata, wakati mwingine askari wa jeshi la Israel walitoka ndani ya magari na kuwafyatulia risasi watuhumiwa. Viongozi wa ofisi ya China waliona hali hiyo dharura, walitaka wafanyakazi wote wa ofisini wakae nyumbani na kujifungia ili kuhakikisha usalama wao. Maofisa wa kidiplomasia wa ofisi hiyo walitakiwa kwenda sehemu ya Gaza, Jerusalem na Tel Aviv kwa shughuli zao, njiani hupita kwenye baadhi ya vituo vya ukaguzi vya Israel. Kwenye vituo vilivyoko sehemu ya Gaza kuna hatari kubwa, jeshi la Israel na watu wenye silaha wa huko wanatupiana risasi mara kwa mara. Balozi Yang Weiguo alisema,
"Tunapokwenda nje, licha ya kupanda magari yanayokinga risasi, pia tunavaa mavazi ya kukinga risasi, tena tunakuwa macho sana. Kwa kawaida, tunafanya shughuli kwa haraka na kutochelewa kwenye sehemu zenye hatari. Njiani tunaweza kuona barabara na madaraja vilivyoharibiwa kwa makombora au mizinga. Siku moja ilikuwa haijatimia saa 1 baada ya mimi na wenzangu kadhaa kuondoka, mlipuko ulitokea kwenye mita zisizofikia 100 kutoka Ikulu ya mamlaka ya taifa ya Palestina."
Sehemu ya Palestina na Israel ni mahali maarufu sana pa utalii duniani, na ni chimbuko cha dini tatu kubwa duniani, kule kuna mabaki mengi ya kale pamoja na rasilimali nyingi za kihistoria na kiutamaduni. Lakini kwa kufikiria usalama, maofisa wa kidiplomasia wa China walioko Palestina, ni mara chache sana kwenda kufanya matembezi, kama wanatoka huwa wanarejea haraka na kujitahidi kutoendesha gari wakati wa usiku.
Kutokana na hali ya vurugu na migogoro ya kijeshi, sehemu ya Palestina ina upungufu wa chakula, mara kwa mara wanakabiliwa na upungufu wa maji na petroli. Balozi Yang Weiguo alisema,
"Ramallah kuna supamaketi moja tu ya wastani, ambayo tunapata mahitaji ya vitu tunavyohitaji kwa matumizi ya kila siku. Wakati mwingine ukitokea upungufu wa chakula, kitu tunachoweza kufanya ni kuvumilia tu."
Ingawa maofisa wanaoishi kwenye sehemu zenye vurugu na migogoro ya kijeshi, mazingira ya maisha yao hayawezi kulinganishwa na ya wale walioko katika mazingira ya amani, lakini wana moyo wa uchangamfu na kukabiliana na matatizo mbalimbali bila wasiwasi.
|