Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-07 15:40:33    
Uhusiano wa kibalozi kati ya China na Senegal unaendelea vizuri baada ya kurejeshwa

cri

Baada ya China na Senegal kurejesha uhusiano wa kibalozi tarehe 25 Oktoba mwaka 2005, uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unaendelea vizuri, ambapo urafiki wa jadi kati ya watu wa nchi hizo mbili unaongezeka siku hadi siku. Ushirikiano wa kunufaishana kati ya nchi hizo mbili kwenye sekta mbalimbali una mustakabali mzuri.

Mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya China na Senegal yanaimarishwa tangu uhusiano wa kibalozi urejeshwe. Mwezi Januari mwaka huu, waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Li Zhaoxing aliizuru Senegal na kusaini makubaliano kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia kati ya China na nchi hiyo, na kuwapatia msaada wakazi wa huko waliokumbwa na mafuriko kwa niaba ya serikali ya China. Mwezi Aprili mwaka huu waziri mkuu wa Senegal aliitembelea China akiongoza ujumbe wa Chama cha kidemokrasia cha Senegal, ujumbe huo uliona kuwa serikali za Senegal na China zina maoni mengi yanayofanana kuhusu namna ya kuongoza nchi zao, na zina nafasi nyingi za kushirikiana katika sekta za kilimo, nishati na uchumi. Mwezi Juni mwaka huu, naibu mwenyekiti wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bw. Wang Zhongyu aliongoza ujumbe wa China kuitembelea Senegal, rais Abdoulaye Wade wa Senegal alipokutana na Bw. Wang Zhongyu na ujumbe wake alisema, uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaendelea vizuri.

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, rais Abdulaye Wade wa Senegal alifanya ziara nchini China. Licha ya Beijing, pia alitembelea miji ya Shanghai na Shenzhen. Alipokuwa mjini Beijing, rais Hu Jintao wa China, mwenyekiti wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bwana Jia Qinglin na spika wa Bunge la Umma la China Bwana Wu Bangguo kwa nyakati tofauti walikutana na rais Wade. Alipofanya mazungumzo na rais Wade, rais Hu Jintao alibadilishana maoni naye kwa kina kuhusu uhusiano wa pande mbili na mambo yanayozihusu pande zote mbili. Kwenye mazungumzo yao, rais Hu Jintao alitoa mapendekezo manne ya kusukuma mbele shughuli za kirafiki kati ya nchi hizo mbili, yaani kutendeana kwa udhati na kuzidisha uaminifu wa kisiasa, kushikilia ushirikiano wa kunufaishana na kuleta maendeleo ya pamoja; kuimarisha mawasiliano ya utamaduni, na kufanya ushirikiano wa pande nyingi ili kulinda maslahi ya pamoja.

Rais Wade alisema watu wa Senegal na China wana urafiki wa jadi. Kusawazisha uhusiano kati ya Senegal na China ni matarajio ya pamoja ya watu wa nchi hizo mbili. Serikali ya Senegal inatilia maanani kukuza uhusiano kati yake na China, na inapenda kukuza uhusiano wa kirafiki na wa kudumu na China.

Ingawa China na Senegal zilisimamisha uhusiano wa kibalozi kwa miaka 10 hivi, lakini mawasiliano ya kibiashara kati ya pande hizo mbili hayakusimama. Senegal inasafirisha chumvi ya phosphate nchini China kila mwaka, na kuagiza chai, bidhaa za nguo na za viwanda vyepesi kutoka China. Kampuni ya ushirikiano ya kimataifa ya Henan ya China mwaka jana ilisaini mkataba wa kujenga mradi muhimu wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 16 huko Dakar, mji mkuu wa Senegal. Kampuni ya Huawei na kampuni ya Zhongxing mwaka jana zimeingia katika soko la mawasiliano ya simu la Senegal. Mwezi Machi mwaka huu, ujumbe wa wanakampuni wa China ulifanya kongamano na wanakampuni wa Senegal huko Dakar, wakijadiliana kuhusu fursa za ushirikiano kwenye sekta za uchumi na biashara.

Baada ya China na Senegal kuanzisha uhusiano wa kibalozi mwaka 1971, serikali ya China ilikuwa imeipatia Senegal msaada mkubwa bila ya masharti. Uwanja mkubwa wa michezo wa Dakar uliojengwa kwa msaada wa China hadi leo bado ni uwanja muhimu katika maisha ya kijamii ya wakazi wa Senegal. Madaktari wa China hata wanakwenda vijijini ili kuwahudumia wagonjwa. Baada ya kurejeshwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Senegal, serikali ya China imeamua kuijengea Senegal jumba la maonesho ya tamthiliya, hivi sasa mradi huo umeanza kufanyiwa ukaguzi. Isitoshe kampuni ya ujenzi wa uyeyushaji madini ya China imesainiana na serikali ya Senegal kumbukumbu ya ushirikiano kuhusu kuanzisha kituo cha umeme chenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kilowatt 205.

Balozi wa China nchini Senegal Bwana Lu Shaye alisema, kurejeshwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Senegal kumeweka msingi wa kisiasa kwa nchi hizo mbili kufanya ushrikiano katika sekta za uchumi, kilimo, afya, elimu na ujenzi wa miundo mbinu, watu wa nchi hizo mbili wamezidisha maelewano na urafiki kwa kufanya mazungumzo na kuzidisha mawasiliano, na kuandika ukurasa mpya wa uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-07